Saturday, December 14, 2013

mandela+clipWananchi wa Afrika ya Kusini wakishuhudia mwili wa rais Mstaafu Hayati Mzee Nelson Mandela ulipokuwa ukitoka Ikulu. Picha na mpigapicha wetu 
……………………………………………………………………………..
Pretoria. Maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini wameshindwa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais wa Kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Nelson Mandela kutokana na muda uliopangwa kumalizika.
Kuanzia Jumatano wiki hii hadi jana, mwili wa Mandela aliyefariki dunia Desemba 4 mwaka huu, ulikuwa ukiwekwa katika Ikulu ya Pretoria, iliyopo ndani ya Majengo ya Umoja (Union Buildings), kila asubuhi kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho.
Jana ilikuwa siku ya mwisho ya utoaji wa heshima hizo na hadi muda uliowekwa ulipokwisha saa 11:30 jioni, kulikuwa na maelfu ya watu waliokosa fursa ya kumuaga mpendwa wao huyo.
Dalili za idadi kubwa ya watu kukosa nafasi hiyo adhimu zilianza kuonekana Jumatano na baadaye juzi Alhamisi kwani hadi muda wa kufunga ulipofika jioni, maelfu ya watu walirejea nyumbani bila kupata fursa ya kuaga.
Jana mchana, Serikali ilitoa taarifa kwamba kwa kuzingatia idadi ya watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho, ilikuwa vigumu kwa watu wote kufikiwa.
“Hatuwezi kuahidi kwamba kila mtu ambaye amejipanga hivi sasa kwenye mstari atapata nafasi ya kufika katika Majengo ya Umoja, tunawaomba wananchi wasiende tena huko,” ilisema taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Serikali (GICS) jana na kuongeza:
“Tunawashukuru sana wananchi kwa kujitokeza, lakini sasa tunawaomba wale ambao hawakuweza kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho, wafanye hivyo kwa kutumia njia zao wenyewe.”
Waziri katika Ofisi ya Rais, Collins Chabane, alisema kuwa hakuna jinsi ya kuwasaidia watu watakaokosa fursa ya kuaga na kwamba Serikali pamoja na familia wamejitahidi kiasi cha kutosha.
Serikali ilisitisha utaratibu wa usafiri kwa watu waliokuwa wakienda kuaga kuanza saa 8:00 mchana hali iliyozua mvutano baina ya maelfu ya waombolezaji na vyombo vya usalama.
Wengine waliokuwa wameishapanda kwenye mabasi na kufika Ikulu waliambiwa kwamba hawataweza kufikiwa hali iliyozidisha manung’uniko.
Ulinzi ni mkali na Rais Jacob Zuma jana aliliarifu Bunge kwamba amewaajiri kwa siku 15 Askari 11,894 kutoka Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), ili wasaidiane na polisi katika ulinzi na usalama wakati wa maombolezo na mazishi ya Mandela.
Wakesha viwanjani
Maelfu ya wananchi walikuwa katika makutano ya barabara za kuelekea Ikulu kuanzia saa 10 alfajiri na wengine walisema walilala jirani na eneo hilo ili waweze kupata fursa ya kumuaga Mandela.
Miongoni mwa waliotoa heshima za mwisho ni ujumbe kutoka Venezuela, ambao ulimzawadia Mandela upanga wa dhahabu na kumkabidhi mjukuu wake wa kwanza, Mandla.
Mandla kwa siku tatu mfululizo amekuwa akiketi pembeni mwa jeneza la babu yake, wakati waombolezaji wakiaga na wakati wote ameonekana mwenye mawazo mengi na huzuni kubwa.
Ndani ya kibanda ambamo mwili wa Mandela uliwekwa kulikuwa na ukimya, ambao mara kadhaa ulivunjwa na kelele za vilio na majonzi kutoka kwa watu walioshindwa kujizuia.
Polisi na wasaidizi mara kadhaa walikuwa wakiwasaidia wale waliozidiwa au wale walioanguka baada ya kuona sura ya marehemu Mandela.
Mapema asubuhi, wengi walijipanga pembezoni mwa barabara kutoka Hospitali ya Jeshi hadi Ikulu, wakiimba nyimbo za kumsifu Mandela na wakati msafara uliokuwa ukisindikiza mwili wake ulipokuwa ukipita, wengine walisikika wakisema; “Siyabinga Tata Madiba…” (wakimaanisha ahsante Baba Madiba).
Wengine walionekana wakiwa wamekwea juu ya miti ili kuweza kuuona vizuri msafara huo wa magari zaidi ya 40, huku baadhi ya watu waliokuwa kazini wakionekana kutoka na kupungia msafara huo.
Wakati huo helikopta za SANDF na polisi zilikuwa zikizunguka katika anga la Jiji la Tswane ndani ya Pretoria na wakati mwili wa Mandela ulipoingizwa Ikulu zilizunguka eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa kabla ya kuondoka.
CHANZO: MWANANCHI

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video