Na Francis Godwin Blog
JESHI la polisi mkoa wa Iringa limewakamata watu wawili akiwemo dereva wa tenki la mafuta lenye namba za usajili T 247 BHP wakisafirisha shehena ya vipodozi maboksi 779 vikiwa vimewekwa ndani ya tenki hilo la mafuta kutoka nchi za kusini mwa Tanzania kuelekea jijini Dar es Salaam .
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi alisema kuwa lori hilo lenye namba za usajili T 247 BHP likiwa na tela lenye namba T 598 BMK ni mali ya kampuni ya World OIL Ltd ya Jijini Dar es Salaam lilikuwa likiendeshwa na Mohamed Sadru (23) mkazi wa Mbezi Temboni jijini Dar es Salaam .
Mbali ya dereva huyo pia jeshi hilo linamshikilia mfanyabiashara aliyekuwa akisafilisha mzigo huo Bw Kassim Kaifa (23) mkazi wa jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika na mzigo huo.
Kamanda Mungi aliwaeleza wanahabari leo kuwa mtego wa jeshi la polisi uliweka baada ya kupokea taarifa kutoka kwa rai wema kuhusiana na lori hilo kutumika isivyo kwa kusafirisha vipodozi hivyo.
Alisema kuwa taarifa kuhusiana na lori hilo kusafirisha vipodozi badala ya mafuta waliitapata kutoka jana na mtego wa kulikamata lori hilo umefanikiwa majira ya saa 9 alfajiri ya leo
Hata hivyo alisema kuwa sehemu kubwa ya vipodozi hizo ni vile ambavyo vilipigwa marufuku na serikali kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa afya ya watumiaji wa vipodozi hivyo.
Alisema kuwa jeshi la polisi limefanikiwa kumata vipodozi hivyo kwa kushirikiana na mamlaka ya chakula na dawa ,wakala wa barabara mkoa wa Iringa na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)
Kamanda huyo alisema kuwa watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika na kuwa ni mapema kwa sasa kuitaja thamani ya vipodozi hivyo na nchi ambayo lori hilo lilikuwa likitoka kutokana na sababu za kiusalama.
|
0 comments:
Post a Comment