Nchini Afrika Kusini, hakuna eneo la kivutio cha kitalii linalotembelewa na wageni wengi kama Kisiwa cha Robben. Umaarufu wa eneo hili umekuwa ukiongezeka mwaka mpaka mwaka.
Lakini hakuna shaka kwamba, kiini cha kutembelewa sana kwa kisiwa hiki ni kutoka na kuwa kituo maalumu cha kuwafunga wapigania uhuru wa Afrika Kusini wakati huo, akiwamo Nelson Mandela.
Mandela, Rais wa kwanza Mwafrika nchini Afrika Kusini, ndiye mhimili wa kivutio cha utalii kwenye jela ya wafungwa wa kisiasa iliyojengwa ndani ya kisiwa hicho.
Kati ya wafungwa wengi wa kisiasa waliowahi kufungwa kwenye jela ya Robben, alikuwamo Govan Mbeki, baba mzazi wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyempokea madaraka Mandela, Thabo Mbeki. Ni Mandela pekee ndiye aliyekaa hapo muda mrefu.
Mpiganaji Mandela aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela, alitumia miaka 17 kwenye jela hiyo kati ya miaka 28 aliyosota kabla ya kuachiwa huru mwaka 1990.
Kufariki kwa Mandela wiki iliyopita, kumechochea kwa kiasi kikubwa kuongezeka umaarufu wa Kisiwa cha Robben kinachoendelea kuwa na historia ya pekee kwa aina yake duniani.
Jela ya kisiwa hiki, pia aliwahi kufungwa mwasisi wa Chama cha Pan Africanist Congress (PAC), Robert Mangaliso Sobukwe na mwanaharakati mwingine wa ANC, Walter Sisulu.
Mwanaharakati mwingine aliyekuwa akipinga ubaguzi wa rangi wakati huo, Jeff Masemola ameweka historia kwa kuwa mfungwa wa kwanza kuhuhumiwa kwenda jela maisha.
Mbali na kufungwa Jela ya Robben, Mandela pia alitumikia kifungo kwenye Magereza ya Pollsmoor (1982–1988) na Victor Verster (1988–1990) kabla ya kuachiwa huru pamoja na wafungwa wengine.
Rais wa mwisho mzungu Afrika Kusini, F. W. de Klerk ndiye aliyemtoa Mandera katika Gereza la Victor Verster.
Umaarufu wa Robben Island hauishii hapo tu, kwani kisiwa hicho ni kitovu cha makazi ya ndege aina mbalimbali zaidi ya 100, wakiwemo ndege aina ya Penguin wa Afrika wanaofikia idadi ya 140,000.
Kisiwa hiki chenye historia ndefu tangu wakoloni wa Uholanzi walipoingia kwa mara ya kwanza katikati ya miaka 1600, kiko umbali wa kilomita 6.9 kutoka Bloubergstrand, Cape Town.
Kisiwa cha Robben, kina urefu wa kilomita 3.3 Kaskazini kwenda Kusini na upana wa kilomita 1.9, huku eneo lote likiwa na kilomita 5.07.
Mwanzo wake:
Kisiwa Robben hakikutumika tu kama sehemu muhimu ya jela kwa watu waliopinga utawala wa Makaburu, bali pia kilikuwa ngome ya jeshi wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliyopiganwa mwaka 1939-1945.
Imeelezwa kuwa, Kapteni Bartolomeu Dias ndiye mzungu wa kwanza kugundua kisiwa cha Robben alipotia nanga mara ya kwanza mwaka 1488, kabla ya Waholanzi na Waingereza kuwasili na kuweka makazi katika karne ya 15.
Kisiwa hiki pia kilikuwa kituo muhimu cha wagonjwa wa Ukoma (Leprosy), wenye matatizo ya akili (Mentally disabled) na magonjwa yasiyotibaka kirahisi katika miaka hiyo.
Makaburu waliamua kukifanya kisiwa hiki kuwa sehemu kuwaweka wagonjwa hatari katika miaka mwanzoni mwa 1840, huku wakiendelea kufanya utafiti wa tiba ya magonjwa hayo.
Katika kipindi hicho, wafungwa wanasiasa na watu wengine walikuwa bado wakitunzwa kwenye jela, huku ikikosekana kabisa tiba ya ukoma, magonjwa ya akili na mengine ya hatari katika miaka ya 1800.
Imeandaliwa na Joseph Kapinga
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment