Na Baraka Mpenja
Tel: 0712461976 au 0764302956
“Hawa
vijana ni kama mahindi machanga yanayochipukia, wasikatishwe tamaa hata
kidogo. Kile walichopata dhidi ya Msumbiji sio mafanikio hata kidogo,
ndio kwanza wanajengwa kwa mafanikio ya baadaye. Nawaomba Watanzania
waisapoti timu hii kwani itakuja kufanya kazi nzuri”. Ni maneno
aliyetamka Kocha wa Tanzanite Rogasian Kaijage kabla ya mchezo wa jana
dhidi ya Afrika kusini.
Hatimaye
alichokuwa anasema kilitimia jana uwanja wa Taifa, jijini Dar es
salaam, baada ya kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa
miaka 20, maarufu kwa jina la Tanzanite kukubali kulala kwa mabao 4-1
dhidi ya Afrika kusini `Basetsana` kwenye mchezo wa raundi ya pili ya
mchujo ya kufuzu kombe la Dunia mwakani nchini Canada.
Amogelang
Motay alikuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika kusini kutikisa nyavu za
Tanzanite kufuatia kuwazidi ujanja vijana wa Tanzanite waliowatoa
Msumbiji raundi ya kwanza kwa mabao 15-1.
Tata
Mandela amewatoka lakini duuuh!: Afrika kusini wakiwa na majonzi
makubwa katika mchezo wa jana, walifanikiwa kuandika matokeo
yanayoonekana pichani juu dhidi ya Tanzanite. (Picha na Blog Lenzi ya
Michezo)
Baada ya kufungwa bao hilo, Tanzanite walipiga hesabu nzuri na kusawazisha dakika ya 13 kupitia kwa nyota wake Theresa Yohana aliyepiga shuti umbali wa mita 30 na kutingisha nyavu za Afrika kusini.
Kama
unajua, unajua tu!, mnamo dakika ya 17, Afrika kusini waliandika bao la
pili kupitia kwa Shiwe Nogwanya na lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi
cha pili Afrika Kusini waliendelea kulisakama lango la Tanzanite na
dakika ya 61, walitumbukiza gozi kimiani kupitia kwa Mosili Makhoali na
kufanya ubao wa Matangazo wa uwanja wa Taifa kusomeka 3-1.
Wimbo
ukiimbwa: Hakika ilikuwa huzuni sana uwanja wa Taifa kufuatia kuimbwa
kwa wimbo wa kuomboleza kifo cha kiongozi wa zamani wa Afrika kusini,
Nelson Mandela aliyefarika dunia.
Afrika
kusini walionesha ukomavu mkubwa na uzoefu wao ,dakika ya 78
walikamilisha idadi ya mabao 4-1 baada ya kufunga kupitia kwa Mosil
Makhoali.
Matokeo
hayo ni mabaya kwa Tanzanite, kwani wanatakiwa kufanya kazi kubwa ya
kufunga mabao 5-0 huko Afrika kusini endapo watahitaji kusonga mbele.
Kwa
uwezo wa vijana wa Afrika kusini, umakini wao, uzoefu wao inaonekana
safari ya Tanzanite ndio imeishia hapo, ingawa katika mpira wa miguu
chochote kinaweza kutokea.
Kama
Afrika kusini wameweza kufunga mabao 4-1 ugenini, kwanini Tanzanite
wasifunge matano Ugenini, inawezekana katika matokeo ya mpira wa Miguu.
Kikosi cha Afrika kusini. (Picha kwa hisani ya blog ya Lenzi ya Michezo)
Afrika
kusini waliingia katika mchezo wa jana wakiwa na majonzi ya kufiwa na
Rais wao wa kwanza, Mzee Tata Nelson Madiba Mandela, lakini walionekana
kutotaka kushindwa hata kama wapo wakati mgumu wa majonzi.
Uwanjani
uliimbwa wimbo maalumu wa Maomboleza wa kumkumbuka Tata Madiba Mandela,
Kiongozi mweusi aliyetukuka kwa kupinga ubaguzi wa rangi.
Matokeo
sio `Ishu` sana kwa Tanzanite, na ndio maana kocha Kaijage alisema
vijana wake ndio kwanza wameanza safari ya kutafuta mafanikio.
“Vijana
hawa wanahitaji kupewa moyo. Najua wazi, Wanzania wengi tunahitaji
mafanikio ya haraka, kwa hili naombeni mnielewe vizuri kuwa, Tanzanite
ni kama mahindi machanga yanayochipukia, yanahitaji kupaliliwa,kuwekewa
mbolea ili yazidi kukua na kuzaa. Lazima waungwe mkono jamani!”. Alisema
Kocha Kaijage.
Hawa
ndio waliwafunga Msumbiji 15-1, lakini jana mambo yalikuwa magumu sana
baada ya kukutana na wajanja wa soka. (Picha kwa Hisani ya Blog ya Lenzi
ya Michezo)
Kaijage alikiri wazi kuwa mchezo ungekuwa mgumu sana kutokana na Afrika kusini kuwa na kiwango cha juu zaidi.
“Wengi
waliamini kuwa wenzetu wapo katika majonzi na ingeathiri mchezo.
Binafsi nilikuwa najua kuwa watashindana sana kutafuta matokeo mazuri.
Tumezidiwa na kufungwa bao nyingi nyumbani, Lakini watu wa mpira wanajua
kuwa mambo kama haya yanatokea”. Alisema Kaijage.
Awali
wakiwa kambini Ruvu mkoani Pwani, Tanzanite walichanganywa na dada zao
wa Twiga Stars ili kuwapa uzoefu, zoezi hilo linaonesha matunda kwani
vijana wanaendelea kuimarika na kuwa na moyo wa kukubali kazi yao na
kushindana.
Mtifuano!:
Vijana wa Tanzanite walipambana sana, lakini uwezo mkubwa wa Afrika
kusini uliwabeba na kupata matokeo ya 4-1. (Picha kwa hisani ya Blog ya
Lenzi ya Michezo)
Pia
mgeni rasmi katika mchezo wa jana, waziri wa habari, vijana, utamaduni
na michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara aliwataka vijana wa
Tanzanite kutokufa moyo kwani mpambanaji kamwe hakati tamaa.
Mukangara
aliwaomba vijana kusahau matokeo hayo na kwenda kukaa chini kujipanga
kwa mechi ya marudiano, huku akiliomba benchi la ufundi chini ya kocha
mkuu Rogasian Kaijage kuhakikisha linaweka mikakati ya kushinda ugenini
na kusonga mbele.
Wakati
Tanzanite wakileta machungu kwa Watanzania, kaka zao wa Kilimanjaro
Stars jana waliwapa raha na burudani kubwa mashabiki wa soka baada ya
kuwatoa mabingwa watetezi wa kombe la Mataifa ya Afrika mashariki na
kati, CECAFA Challenge, Uganda The Cranes, kwenye mchezo wa robo fainali
ya kwanza ya michuano hiyo, uwanja wa Manispaa Mombasa.
Stars walishinda kwa penati 3-2 baada ya dakika tisini kumalizika kwa sare ya 2-2.
Sasa
Kili Stars inajiandaa na mchezo wa nusu fainali Desemba 10 mwaka huu
dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo, Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee
stars.
0 comments:
Post a Comment