Na Baraka Mpenja wa
Tel: 0712461976/0764302956
TIMU
ya Taifa ya Tanzania bara, The Kilimanjaro Stars imefanikiwa kufuzu
hatua ya nusu fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika mashariki na kati,
CECAFA Challenge 2013 baada ya kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi, na
wababe wake mfululizo kwa mechi za hivi karibuni , Uganda The Cranes
kwa mikwaju ya penati 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya ngwe ya dakika
90 kwenye uwanja wa Manispaa, Mombasa.
Katika
mchezo huo, Uganda walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza dakika
ya 16 kupitia kwa mshambuliaji wake anayekipiga klabu ya Gor Mahia ya
Kenya , Dani Sserunkuma , baada ya kupokea krosi ya Khamis Friday Kiiza
aliyemtoka beki wa Stars, Erasto Nyoni na kuachia shuti la chini
lililompita kipa mkongwe anayecheza Gor Mahia pia, Ivo Philip Mapunda.
Mrisho
Khalfan Ngassa `Anko` aliisawazishia Kili stars bao hilo dakika mbili
baadaye kufuatia kuwazidi ujanja mabeki wa Uganda, akimalizia mpira
murua uliochongwa na jembe la TP Mazembe, Mwana Ally Samatta.
Pia
Samatta aliangushwa nje kidogo ya eneo la hatari na Ngassa kwa mara
nyingine alipewa majukumu ya kupiga mpira na bila kufanya makosa
aliachia shuti lililotinga moja kwa moja nyavuni.
Hadi
mapumziko, Kili stars walikuwa mbele kwa mabao 2-1, huku kipinidi cha
pili kikisubiriwa kwa hamu kuona nani ataibuka na ushindi.
Wamefuta
uteja: Leo hii Kilimanjaro Stars wameondoa unyonge baada ya kuwashinda
Waganda kwa penati 3-2 na kutinga hatua ya nusua fainali ya CECAFA 2013
Kipindi
cha pili kilipoanza, majanga yaliikumba Stars baada ya kiungo wake
mahiri, Salum Abubakar `Sure Boy` kuoneshwa kadi nyekundu baada ya
kumfanyia madhambi Sserunkuma.
Dakika
ya 73, mabeki wa Stars walifanya makosa na kumruhusu Martin Mpuga
kusawazisha bao hilo akiunganisha mpira wa kona uliochongwa na Godfrey
Walusimbi.
Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 2-2 na ndipo sheria ya mikwaju ya penati ilipotumika.
Mtu wa kasi: Mrisho Ngassa ameifungia Stars mabao mawili ndani ya dakika 90
Kipa Ivo Mapunda alikuwa shujaa baada ya kuokoa mikwaju miwili ya penalty ya Dani Sserunkuma na Khalid Aucho wa Uganda .
Mbali na kuokoa penalti hizo mbili, Uganda walipoteza penalti nyingine moja baada ya Godfrey Walusimbi kupiga na kukosa.
Khamis
Kiiza na Emannuel Okwi ndiyo wachezaji pekee walioifungia Cranes
penati katika mchezo wa leo ambao Uganda waliingia kwa ujasiri wa
kuibuka na ushindi kufuatia kuwa na rekodi nzuri dhidi ya Stars.
Penati
za Stars zilifungwa na nahodha Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’na
Erasto Nyoni, wakati Mbwana Samatta na Amri Kiemba walikosa.
Waganda wameshikwa pabaya sana
Hata
hivyo, mshambuliaji wa Stars anayekupiga TP Mazembe ya DRC Kongo,
Mbwana Ally Samatta ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa Robo Fainali hiyo
ya Kwanza ya CECAFA Challenge.
Samatta
amepewa tuzo hiyo inayoambatana na zawadi ya king’amuzi na kifurushi
cha GOtv kufuatia kuwa chanzo cha mabao yote mawili ya Stars
yaliyofungwa na Mrisho Khalfan Ngassa.
Aidha
Samatta amepewa tuzo hiyo na kuwa mchezaji wa pili wa Kili Stars
kuibuka kidedea katika tuzo hiyo kwani katika mchezo wa kwanza wa Stars
hatua ya makundi dhidi ya Zambia uliomalizika kwa sare ya 1-1, kiungo
Salum Abubakar `Sure Boy` aliteuliwa kuwa mchezaji bora.
Jembe la TP Mazembe: Mbwana Samatta ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa robo fainali ya kwanza ya CECAFA leo hii
Kwa
matokeo ya leo, Kili stars wanarudia kuingia nusu fainali kama mwaka
jana nchini Uganda, wakati The Cranes wamelitema kombe lao na kuliacha
Mombasa Kenya na kurejea kufanya yao Kampala.
Fainali
nyingine imepigwa jioni ambapo wenyeji Kenya wameshuka dimbani
kukabiliana na Rwanda na kushuhudia Harambee stars wakiibuka na ushindi
wa bao 1-0 na kuwafungashia virago Amavubi.
Bao
pekee la beki wa Azam FC ya Dar es Salaam, Joackins Atudo kwa penalti
dakika ya 56 limewapeleka Kenya mbele ya safari ya kuusaka Ubingwa wa
CECAFA katika ardhi yao 2013.
Kwa
matokeo hayo Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itamenyana na wenyeji,
Harambee Stars katika Nusu Fainali ya Kwanza ya Kombe la Mataifa ya
Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Desemba 10, mwaka huu Uwanja
wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Hongera
Kilimanjaro Stars kwa kuwaondolea maumivu Watanzania ambao kwa muda
mrefu sasa wamekuwa wanyonge kwa Waganda kila wanapokutana katika
michuano mikubwa.
Safari
bado ni ngumu, lazima vijana wakaze mwanzo mwisho kuhakikisha wanatwaa
kombe hilo kama walivyofanya kwa mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya
Kocha Mdenmark, Jan Poulsen Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment