Hospitali ya Wilaya ya Pangani ni moja ya Vituo vya kutolea huduma za matibabu ambazo zilitembelewa na Waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma.
Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Luhende Singu (kulia) akifafanua jambo kuhusu mradi wa akina mama wajawazito wasio na uwezo unaoendeshwa na NHIF mkoani Tanga.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Dk. Dennis Ngaromba akitoa maelezo mafupi kuhusu mradi unaoendeshwa na NHIF wilayani humo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya waandaji wa vipindi vya elimu kwa umma wakimwangalia motto aliyezaliwa hospitalini hapo na mmoja wa wanufaika wa mradi wa NHIF.
Washiriki wakivuka kwenye kivuko kuelekea Kituo cha Afya cha Mwera ambacho ni miongoni mwa vituo vinavyotoa huduma kupitia mradi huo.
…………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Pangani
MRADI wa kusaidia akina mama wajawazito wasio kuwa na uwezo unaoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Benki ya watu wa Ujerumani (KfW) katika mikoa ya Tanga na Mbeya umesaidia kuongeza mwamko wa akina mama kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mwamko huo umetokana na elimu kubwa inayoendelea kutolewa na NHIF kwa walengwa, lakini pia huduma zinazotolewa kwa akina mama hao baada ya kuandikishwa katika vituo vinavyoendesha mradi huo.
Hayo yalibainika katika ziara ya mafunzo iliyofanywa na Waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma vinavyorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo Mwenyekiti wa Mkutano huo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Ziara hiyo ilihusisha Hospitali ya Wilaya ya Pangani, Kituo cha Afya cha Mwera na Kituo cha Afya Makorola.
Akitoa maelezo ya mradi huo unavyotekelezwa katika wilaya ya Pangani, Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Dennis Ngaromba alisema kuwa mbali na mradi huo kuwa na manufaa makubwa kwa wajawazito lakini pia umekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato katika hospitali hiyo na vituo mbalimbali vinavyotoa huduma kwa akina mama hao.
Alisema kuwa mama mjamzito atahudimiwa kupitia mradi huo baada ya kufika kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za matibabu na kujiandisha ambapo atapewa kitambulisho cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kumwezesha kupata matibabu katika hospitali yoyote mpaka atakapojifungua.
“Baada ya mama kujifungua atahudumiwa na mtoto wake kwa muda wa miezi mitatu na baada ya hapo mama na familia yake atalipiwa gharama za kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huduma ambayo ataitumia kwa muda wa mwaka mmoja,” alieleza Dk. Ngaromba.
Kutokana na mradi huo, alisema kuwa kwa sasa akina mama wilayani Pangani wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito lakini pia kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za matibabu.
Wakizungumzia faida za mradi huo akina mama ambao walikuwa wamelazwa hospitalini hapo kwa huduma ya kujifungua, waliupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa mradi huo na kuongeza kuwa umekuwa ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa wanapewa huduma bila ya wao kugharamia kitu chochote.
Kwa upande wa waandaji vipindi kutoka katika wizara mbalimbali na Taasisi zake, walifurahishwa na mradi huo na kuwataka watoa huduma kuunga mkono juhudi za Mfuko huo kwa kutoa huduma nzuri kwa walengwa kwa kuwa umeonesha una mafanikio makubwa na una malengo ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito vilivyokuwa vikisababishwa na kushindwa kugharamia huduma za matibabu.
Katika hospitali ya wilaya ya Pangani, jumla ya akina mama wajawazito 2,000 wameandikishwa katika mradi huo ambao wananufaika na huduma za ada ya kujiandikisha, gharama za vipimo, gharama za dawa, gharama za kulazwa, upasuaji mdogo na mkubwa na unaofanywa na madaktari bingwa, mazoezi ya viungo, miwani ya kusomea na huduma za meno.
Naye Ofisa Mwandamizi Mawasiliano wa NHIF, Luhende Singu alisema kuwa Mfuko unaendelea na program mbalimbali za kuhamasisha akina mama wengi zaidi kuchangamkia huduma hizo.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kujiunga na NHIF na CHF ili wawe na uhakika wa matibabu wakati wowote lakini pia kwa watoa huduma kutumia fursa za mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili kuboresha huduma za afya katika vituo vyao.
0 comments:
Post a Comment