Na Baraka Mpenja
MICHUANO
ya kombe la Mataifa ya Afrika mashariki na kati, CECAFA Challenge
imezidi kushika kasi leo nchini Kenya ambapo wenyeji Kenya wameungana na
Wahabeshi wa Ethiopia kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuifumua
Zanzibar Heroes mabao 2-0, Uwanja wa Afrah, Nakuru.
Alikuwa
ni Beki wa Azam fc, inayoshiriki ligi kuu Tanzania bara, Joackins Atudo
aliyekuwa wa kwanza kuandika bao la kwanza dakika ya 6 na baadaye
mshambuliaji wa AFC Leopards ya Kenya, Allan Wanga akaandika kimiani bao
la pili dakika ya 60.
Kwa
matokeo ya leo, Zanzibar inabaki na alama zake tatu na sasa wapo mguu
ndani-nje kwani watasubiri hatima ya kwenda robo fainali katika nafasi
mbili za `Best Losers`.
Kwa
Harambee Stars mambo yamejipa yenyewe kwa kutinga robo fainali kwani
wametimiza alama 7 baada ya awali kuwalaza Sudan Kusini mabao 3-1 na
kutoka suluhu na Ethiopia.
Mchezo
mwingine wa kundi A uliopigwa mapema uliwakutanisha Sudan kusini dhidi
ya Ethiopia na kushuhudia dakika tisini zikikamilika kwa wahabeshi
kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, uwanja wa Afrah mjini Nakuru, Kenya.
Mabao
ya Ethiopia yalifungwa na Yousuf Yassin aliyetokea benchi kipindi cha
pili na kufunga bao la kwanza dakika ya 54 baada ya kupokea pasi nzuri
ya Manaye Fantu kutoka upande wa kulia na Biruk Kalbolre aliyeingia pia
kipindi cha pili na kufunga goli muhimu dakika ya 82.
Sudani
Kusini sasa linakuwa Taifa la kwanza kutoa mkono wa `Bai Bai` katika
michuano ya mwaka huu bila hata kupata pointi moja, kwani walifungwa
mechi zake mbili za mwanzo, 2-1 dhidi ya Zanzibar na 3-1 kutoka kwa
wenyeji Harambee stars.
Kesho
shughuli inaendelea kwa timu za kundi B, ambapo Timu ya Taifa ya
Tanzania bara, Kilimanjaro Stars itajitupa uwanjani katika mchezo muhimu
sana dhidi ya Burundi na Zambia watakabiliana na mabaharia wa Somalia.
0 comments:
Post a Comment