Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
MAANDALIZI ya kombe la Mapinduzi linalotarajia kuanza kutimua vumbi januari mosi mwakani yanakwenda vizuri na timu zote zilizothibitisha kushiriki zinatarajia kuwasili desemba 31 mwaka huu.
Msemaji wa kamati ya mashindano , Farouk Karim amesema kuwa timu za Tusker fc, AFC Leopard za Kenya, KCC, URA za Uganda , Simba sc, Yanga, Azam fc na Mbeya City za Tanzania bara tayari zimeshathibitisha kushiriki na kamati ya maandalizi imeshakamilisha taratibu za kuzipokea.
SIMBA imepangwa kufungua pazia la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kucheza na AFC Leopards ya Kenya Januari Mosi wakati Yanga wakishuka dimbani siku inayofuata kuikabili Tusker FC.
Karim amesema mgeni rasmi katika mechi ya ufunguzi itakayopigwa januari mosi majira ya saa mbili usiku katika uwanja wa Aman kisiwani Unguja baina ya Simba sc dhidi ya AFC Leopard ya Kenya atakuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Italia, Cesare Prandelli.
Pambano la Simba na Leopards litatanguliwa na mechi kati ya wenyeji KMKM na KCC ya Uganda litakalopigwa saa 10 jioni kwenye uwanja huohuo.
“Ninavyozungumza na wewe muda huu, Prandelli yupo hapa Zanzibar mapumzikoni na tayari amekubali kufungua michuano hii yenye maana kubwa katika miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar”. Alisema Karim.
Karim alisema katika michuano ya mwaka huu viwanja viwili vitatumika ambavyo ni Gombani kisiwani Pemba na Aman Kisiwani Unguja.
“Uwanja wa Gombani upo katika hali nzuri na unavyojua una nyasi za bandia. Uwanja wa Aman umefanyiwa ukarabati mkubwa na hivi sasa wataalamu kutoka China wapo hatua za mwisho kabisa kukamilisha shughuli yao”. Alisema Karim.
Mratibu huyo alitoa wito kwa wadau, wapenzi wa soka visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi kwani kamati ya mashindano inategemea mapato ya milangoni kufanikisha mipango.
“Michuano hii inagharimu zaidi ya shilingi milioni 600, hatuna fedha hizo, tunategemea mapato ya milangoni, hivyo mashabiki kufika kwao kwa wingi ndio mafanikio yetu”. Aliomba Karim.
Aidha ameziomba taasisi na makampuni ya bara na visiwani kujitokeza kufanya matangazo katika michuano hiyo ili angalau wapate pesa za kuendeshea michuano hiyo.
Michuano iliyopita, Azam fc walitwaa ubingwa, lakini mwaka huu kuna changamoto mpya hasa kutokana na uwepo wa timu za Dar Young Africans na Mbeya City ambazo hazikushiriki.
Mechi zote za hatua ya makundi na robo fainali zitafanyika kwenye viwanja wa Gombani Pemba na Aman Unguja, wakati nusu fainali na fainali zitapigwa kwenye Uwanja wa Aman.
Katika michuano iliyopita Simba waliishia nusu fainali baada ya kuondolewa na Azam FC kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 2-2 hata baada ya kuongezwa dakika 30.
0 comments:
Post a Comment