Tel: 0712461976 au 0764302956
Maafande wa JKT Ruvu wameanza mazoezi ya kujiwinda na mzunguo wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi Januari 25 mwakani.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Greyson Haule amesema hawajaanza kambi rasmi kwasababu hawajakamilisha baadhi ya taratibu kati ya benchi la ufundi na viongozi wa klabu.
“Kuna baadhi ya wachezaji hawajaripoti mazoezini, tunarajia wote kuwasili leo jumatatu tayari kwa kuunganisha nguvu ya pamoja katika maandalizi. Lengo ni kurekebisha makosa yetu na ikumbukwe mzunguko wa kwanza baadhi ya wachezaji walienda mafunzo ya jeshi na ndio maana tulihangaika sana”. Alisema Haule.
Haule aliongeza kuwa JKT Ruvu ilianza ligi vizuri na kuongoza ligi kwa muda, lakini baadaye ikageuka daraja la kuchukulia pointi kwa timu nyingine, hivyo wanajipanga kusuka kikosi chao upya.
“Unajua timu kama Simba, Yanga, Azam fc zimeshajua utamu wa mashindano, timu za jeshi bado hazijaonja utamu wa mpira, lakini siku ikifika zikaonja, zitakuja kufanya vizuri sana. Kikosi kipo sawa, kuna baadhi ya wachezaji viongozi wamewasajili kwa mujibu wa mapendekezo yetu”. Alisema Haule.
Kocha huyo alisisitiza kuwa mashabiki waziunge mkono timu zote za jeshi katika harakati zao za soka kwani zote zinatoka baba mmoja na mama mmoja.
“JKT Ruvu, Ruvu shooting, JKT Oljoro, Mgambo JKT zote ni timu zenye mama mmoja na baba mmoja, unapoamua kuwa shabiki wa mojawapo ni busara ukashabikia zote. Tukipata sapoti kama Mbeya City FC, na sisi tutaonesha ushindani mkubwa na kubadili mfumo wa utemi kwa Simba na Yanga”. Alisema Haule.
Aliongeza kuwa Viongozi wa serikali mkoani Mbeya, viongozi wa chama cha soka na mashabiki wote wameweka nguvu ya pamoja kuishabikia timu yao na kuipa masaada mkubwa na ndio maana kwa mazingira hayo Mbeya City imegeuka kuwa tishio.
0 comments:
Post a Comment