Bendera za mataifa mbalimbali zikipepea nusu mlingoti jijini Dar es Salaam kuomboleza kifo cha Madiba. PICHA | FIDELIS FELIX
Pamoja
na kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mandela na wananchi wa
Afrika Kusini, viongozi wa mataifa makubwa duniani wameonyesha kuguswa
na msiba huo kiasi cha kuomboleza kwa namna tofauti tofauti.
India
Hii
inaweza kuwa ni nchi mojawapo ambayo imetangaza siku nyingi zaidi za
maombolezo kwa ajili ya kifo cha Nelson Mandela kutoka nje ya Bara la
Afrika.
Baada
ya kupata taarifa za kifo cha Mandela, Serikali ya India kupitia Waziri
Mkuu wa nchi hiyo, Manmohan Singh aliwatangazia siku tano za maombelezo
na kuamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti katika kipindi hicho cha
maombolezo.
Sambamba na hilo, Singh alimwelezea namna kiongozi huyo wa Afrika alivyokuwa shujaa katika kupinga mfumo wa kibaguzi.
Ufaransa
Kuonyesha
kuwa taifa hili pia limeguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huu, jengo
refu zaidi mjini Paris la Eiffel Tower liliwashwa taa zenye rangi
zilizopo kwenye Bendera ya Afrika Kusini.
Picha
zilizopigwa katika jengo hilo mpaka siku ya jana, linaionyesha likiwa
limenakshiwa na taa zenye rangi tano za bendera hiyo zikiwemo nyekundu,
kijani, nyeusi, njano na nyeupe.
Marekani
Taifa
hili lenye nguvu duniani limeonyesha heshima kubwa kwa Nelson Mandela
kwa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti nchi nzima na kuweka siku
tatu za maombolezo.
Kana
kwamba hiyo haitoshi taa zenye rangi ya Bendera ya Afrika Kusini
zilionekana kung’arisha jengo la Empire state lililopo NewYork na Hoteli
ya Omni iliyopo Dallas.
Mjini
Washington jengo la Ubalozi wa Afrika Kusini lilitawaliwa na taa hizo
pamoja na bendera za nchi hiyo hali iliyosababisha mwonekano wa eneo
hilo kubadilika kabisa.
Pia kiongozi wa taifa hilo Rais Barack Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Graca Machel ambaye ni mjane wa Mandela.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani ilisema kuwa Obama alimpigia simu mama Machel kwa lengo la kumtumia salama za rambirambi.
Canada
Kwa
mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini Canada,
Waziri Mkuu Stephen Harper amewaalika mawaziri wakuu wengine wastaafu wa
nchi hiyo kuungana naye kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mazishi ya
Nelson Mandela.
Australia na Uingereza
Kama
ilivyo kwa nchi nyingine, mataifa haya pia yalitangaza siku za
maombolezo sanjari na kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kuashiria
maombolezo ya kifo cha kiongozi shujaa na mahiri barani Afrika, hayati
Nelson Mandela.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment