“Waziri hana mamlaka ya kumwondoa mkurugenzi wa halmashauri, taasisi, shirika na katibu wa wizara yake kutokana na kubanwa na mfumo.” Makamba.
…………………………………………………………………………….
Mwanza. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema ipo haja ya kubadili mfumo wa watendaji serikalini ili wanapoboronga nao wajibishwe na mawaziri.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Makamba alisema mfumo uliopo sasa, hauwapi nguvu mawaziri ili kuwawajibisha watendaji pale wanapokosea na badala yake unawabana wenyewe hivyo kuendelea kuwa kitanzi kwao.
“Mimi ni waziri, akikosea katibu nawajibishwa huyu anabaki, mimi siwezi kumwajibisha hivyo wanafanya lolote na sisi tunalazimishwa kuwajibishwa kisiasa kwa makosa ya watendaji,” alisema.
“Baada ya Kamati ya Maliasili Ardhi na Mazingira iliyo chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli kuomba kwa Spika kutumia ushahidi kwa kuweka kanda za video ili kuonyesha kilichotokea kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili, hali ilichafuka ndani ya kikao cha Bunge na kila mmoja akawa na hisia na wengine kuanza kububujikwa na machozi na wabunge kuchangia hoja za kutaka mawaziri kuachia ngazi, hawakuangalia kiini cha tatizo, waliwabana mawaziri tu,” alisema.
Alisema Serikali kupitia mamlaka za juu, inapaswa kuangalia mfumo uliopo kwa lengo la kuubadilisha na kuingiza mapendekezo na mfumo mpya kwenye Katiba Mpya kuhusu uwajibikaji wa mawaziri na watendaji wakuu kwenye wizara, taasisi, idara, halmashauri na mashirika ya umma ambao ni wataalamu mbalimbali kuwajibishwa na mawaziri husika endapo kutaonekana utendaji wao haukidhi ama kwenda kinyume na maadili na sheria zilizopo.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment