Askofu Godfrey Mdimi Mhogolo wa Kanisa la Anglikana,Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) akihubiri mbele ya mamia ya waumini wa kanisa hilo jana wakati wa Ibada ya Krismas. Picha na Israel Mgussi.
……………………………………………………..
Geita. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Damian Dallu amesema viongozi wengi wamekuwa wakijidanganya kwa kuwa wabinafsi na wenye kujirundikia mali na kutojali watu maskini kwa kuamini kufanya hivyo watajitengenezea mazingira ya kufurahisha nafsi zao.
Akihutubia kwenye ibada ya Krismasi iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Geita, askofu huyo aliwataka Watanzania kuacha ubinafsi na kupendana huku akisisitiza kuwa;“Ukiona mwenye madaraka anajifirikia mwenyewe na kusahau shida zinazowakabili watu maskini basi huyo siyo kiongozi wa watu.”
Askofu Dallu alisema siku zote kiongozi ni mtu wa kuwajali watu na anapaswa kuwajibika kwao, lakini kama inatokea kiongozi anaweka masilahi yake mbele huyo kiongozi hafai,” alisema Askofu Dallu.
“Mali haitawaletea furaha kamwe. Hata ikitokea mahali kuna mali mfano hapa Geita tuna dhahabu, Mtwara wana gesi na watu wanatumia madaraka yao kuwataka watu wa Mtwara watenganishwe na Watanzania wenzao kwa ajili ya gesi,” alionya.
Alisema kuwa na ubinafsi wa kujirundikia mali kamwe hauwezi kumletea furaha binadamu mbali ya kuwa chanzo cha vurugu na mitafaruku.
Alitolea mfano nchi za Uarabuni namna zilivyobarikiwa kuwa na mali ya asili kama mafuta lakini hata hivyo pamoja na neema hizo bado nchi hizo zinakabiliwa changamoto ya ukosefu wa amani.
Askofu Dallu alisema kuwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongaza watu wanatumia vibaya nafasi zao ikiwa ni pamoja na kuharibu rasilimali za nchi kwa kushiriki kuhamasisha watu kuwa na utengano.
Alisema viongozi wengi wanatumia mamlaka ili wapate kutawala rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi bila kuwahurumia Watanzania wenzake.
Pia alikemea vitendo vya baadhi ya viongozi na jamii nzima kuharibu na kutumia vibaya rasilimali za nchi kwa kuua tembo na kuangamiza vivutio vya nchi kwa masilahi binafsi.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment