
JUMLA
ya watoto 137 na wajawazito 19 hufariki dunia kila siku nchini Tanzania
kwa matatizo yanayotokana na uzazi. Vifo vya watoto pekee wanaopoteza
maisha kutokana na matatizo hayo kwa mwaka hufikia 50,000 kwa nchi
nzima.
Takwimu
hizi za kusikitisha zimetolewa jana jijini Dar es Salaam na Meneja
Mradi wa mpango wa ‘Wajibika Mama Aishi’, Bw. David Lyamuya toka Taasisi
ya Utepe Mweupe katika semina ya wahariri na waandishi wa habari
waandamizi.
Lyamuya
alisema mbali na idadi hiyo kubwa ya akinamama pamoja na watoto
kupoteza maisha yapo matukio mengine ya vifo ambayo hayaingizwi kwenye
takwimu, hali inayoonesha huenda vifo hivyo ni zaidi ya takwimu halisi
zilizopo.
Alisema
kuna kila sababu kwa mamlaka husika kwa kushirikiana na jamii kulivalia
njuga suala hilo ili kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinakoma. Aidha
alisema licha ya uhimizaji wa wajawazito kuhudhuria klini bado idadi
kubwa hasa vijijini wanajifungulia nyumbani kutokana na umbali mrefu wa
sehemu zinapotolewa huduma za afya.
“…Sisi
tumefanya utafiti katika Mkoa wa Rukwa kuangalia hali ya upatikanaji
huduma za afya kwa wajawazito. Yapo maeneo mama aliyefikia hatua ya
kujifungua (mwenye uchungu) hutakiwa atembee kilomita 94.5 ndiyo
anakutana na kituo cha afya, sasa mtu aliye na hali kama hiyo hawezi
kutembea umbali mkubwa kiasi hicho hivyo hulazimika kujifungua
nyumbani,” alisema Lyamuya.
Aidha
aliongeza kuwa taasisi ya Utepe Mweupe (The White Ribbon Alliance) kwa
sasa inaendesha kampeni ya miaka mitatu ya “Wajibika Mama Aishi” ikiwa
ni moja ya hatua ya kushawishi kila mmoja kuwajibika kuhakikisha
anakabiliana na vifo vya akinamama na watoto vinavyotokea hasa wakati wa
kujifungua.
Hata
hivyo aliwataka wanahabari kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutoa
mchango wa kuvishavishi vyombo husika na wanajamii kwa ujumla kupambana
na vifo vya akinamama na mtoto.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
0 comments:
Post a Comment