WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema kila Halmashauri hapa nchini inapaswa kuweka
kwenye mpango wake wa maendeleo kifungu cha ujenzi wa maktaba ya wilaya
ili watu waweze kusoma na kujiendeleza kwa urahisi.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Novemba 16, 2013) wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 19 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi wa Nyaraka cha Bagamoyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho nje kidogo ya mji wa Bagamoyo.
Jumla
ya wahitimu 749 walitunukiwa vyeti kati yao 244 vikiwa ni vya
stashahada na 505 ni vya astahada katika fani za ukutubi na utunzaji
nyaraka.
Alisema
ukutubi ni mojawapo ya fani kongwe hapa duniani japo haiongelewi sana
hapa nchini. “Hili ni eneo linalomgusa kila mmoja wetu, kuanzia mtu wa
kawaida awe mkulima, mvuvi, seremala, mjasiriamali ama yeyote ambaye
anahitaji taarifa mbalimbali zimsaidie katika maendeleo yake. Hali
kadhalika, mwanafunzi, msomi na mwanataaluma yeyote hawezi kufikia upeo
wa masomi na taaluma yake kama hakusoma vitabu na machapisho yaliyoko
katika maktaba ambavyo vinatunzwa mkutubi.
Alisema
kati ya wilaya 133 zilizopo hapa nchini, ni wilaya 19 tu ambazo
zimejenga maktaba katika ngazi ya wilaya. “Hii ni sawa na asilimia 14.2
tu ya wilaya zote. Upungufu huu unasababishwa na tatizo la watu
kutotambua umuhimu wa kuwa na maktaba na katika hili lawama ni lazima
wabebeshwe Wakurugenzi wa Halmashauri,” alisema.
Waziri Mkuu alisema katika ngazi ya mikoa hali si mbaya kwani mikoa 22 kati ya 25 ya Tanzania Bara ina maktaba za mkoa.
“Tunazo Halmashauri 167 lakini ni Halmashauri 19 tu ambazo zina maktaba… nitoe
wito kwa wilaya zote ambazo hazina maktaba zione umuhimu wa kuwa na
maktaba zake. Tukifanikiwa kuwa na maktaba katika kila mkoa na kila
wilaya itatuwia rahisi kuisogeza huduma hiyo katika ngazi ya kata ili
iwe karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Akisisitiza
umuhimu wa fani hiyo Waziri Mkuu alisema mahitaji ya wakutubi hapa
nchini ni makubwa kwani hapa nchini kuna shule za msingi zaidi ya 16,300
na shule za sekondari zaidi ya 4,500 za Serikali na za binafsi.
“Tunawahitaji
zaidi hawa wakutubi katika shule zetu kwani wakiwepo kwenye shule zetu
watakuwa karibu na wanafunzi na wataweza kuwasaidia wanafunzi kupanua
uelewa wao,” alisisitiza.
Aliahidi kufuatilia maombi ya bajeti ya maendeleo ya chuo ili kukisaidia chuo hicho kiwe bora zaidi.
Mapema
akitoa taarifa ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Zuberi Khatibu
alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa licha
ya kuwa udahili umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Mwaka
2007/2008 chuo kilidahili wanafunzi 100 lakini katika mwaka 2012/2013
tulidahili wanafunzi 708 na mwaka huu wa masomo (2013/2014) tumedahili
wanafunzi 821,” alisema.
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dk. Alli Mcharazo, alisema kabla
chuo hicho hakijaanzishwa hapa nchini, wanafunzi waliokuwa wakitaka
kusomea masomo ya ukutubi na uhifadhi nyaraka walilazimika kwenda
Makerere, Uganda.
Alisema
mbali ya uwepo wa chuo hicho, changamoto kubwa inayowakabili ni ufinyu
wa bajeti, uhaba wa miundombinu hasa upungufu wa mabweni na madarasa
kiasi kwamba wanalazimika kuwa na shift mbili za masomo (asubuhi na
jioni) hali ambayo inaathiri utoaji wa elimu chuoni hapo.
Katika
risala yao, wanafunzi wanaohitimu waliomba wapatiwe ajira za moja kwa
moja kama ilivyo kwa walimu au askari, pia waliomba maktaba ya chuo
hicho ipanuliwe kwa sababu ni ndogo na ikiwezekana chuo kiongezewe
kompyuta kwa sababu zilizopo hazitoshi wanafunzi wote kufanya mazoezi
kwa vitendo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, NOVEMBA 17, 2013
0 comments:
Post a Comment