Afisa
Habari wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Asiatu Msuya
akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu majukumu
mbalimbali ya Divisheni ya Mikataba ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa
kitaalam katika masuala ya Mikataba na makubaliano yanayoihusu
serikali,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa.
Mkurugenzi
Msaidizi Divisheni ya Mikataba toka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Bw. Edson Mweyunge akifafanua kwa waandishi wa Habari (hawapo
pichani)kuhusu utendaji kazi na mafanikio ya Divisheni hiyo katika
masuala ya Mikataba,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara
ya Habari (MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI___
Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu ndiyo yenye jukumu la Kikatiba la kuishauri
Serikali kwenye mambo yote ya kisheria ikiwemo masuala ya mikataba
jukumu ambalo linatekelezwa kupitia Divisheni ya Mikataba.
Ili Divisheni hii, iweze kutekeleza majukumu yake, Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha mwaka 2013/2014 kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikijenga uwezo wa wataalam
katika kutoa ushauri wa kisheria, kuhakiki na kufanya majadiliano ya
mikataba mbalimbali ya kibiashara na kimataifa yenye kuihusisha
Serikali, kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Divisheni hii na
kuweza kubaini matatizo kabla na hata baada ya mikataba kusainiwa ili
kuweza kurekebisha kasoro na hatimaye kuwa na mikataba yenye maslahi
kwa taifa.
i. Ofisi
imefanya mafunzo juu ya majadiliano ya Mikataba yaliyojumuisha maofisa
kutoka Wizara na Taasisi za Serikali wadau mbalimbali takribani 30.
ii. Imeweka
utaratibu wa mafunzo ya muda mrefu kwa Mawakili. Kwa mwaka huu Mawakili
wa Serikali wawili wako mafunzo ni kwa ajili ya shahada ya Uzamili
katika maeneo ya mafuta na gesi.
iii. Mwezi
huu ofisi ikishirikiana na Chuo cha Uongozi imewapa mafunzo Mawakili 8
kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya majadiliano katika maeneo
mbalimbali ya Mikataba.
iv. Kuongeza idadi ya Mawakili katika Divisheni hii wakati wowote uwezo ukiruhusu.
Aidha,
katika kipindi cha mwaka 2012/2013 Ofisi imefanikiwa kushughulikia na
kutoa ushauri wa kisheria katika mikataba 330 ambapo mikataba 295 kati
ya hiyo ilihusu manunuzi ya umma na 35 ilihusu masuala ya uwekezaji,
mikataba 58 ya makubaliano (MoU) na mikataba 21 ya makubaliano Baina ya
nchi (Bilateral Agreements). Sambamba na hilo, Ofisi ilihudhuria katika
vikao 185 vilivyohusu majadiliano ya mikataba na mahusiano ya kimataifa.
Katika kutekeleza majukumu haya, ofisi imekuwa ikikumbana na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na:
i. Uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya mafunzo na vitendea kazi
ii. Baadhi ya Taasisi na Idara za Serikali kutokuleta Mikataba au makubaliano yao kuhakikiwa kabla ya kusainiwa.
iii. Ufinyu wa muda kutokana na masuala ya dharura yanayohitaji ushauri wa haraka wa kisheria.
iv. Namba ndogo ya Mawakili wa Serikali wataalam katika maeneo mapya maalum mfano ya gesi, petroli, madini nk.
v. Ofisi
kuhusishwa katika hatua ya kuhakiki mikataba badala ya kuhusika kuanzia
kwenye hatua ya majadiliano yanayohusisha wataalam wa maeneo mengine.
Mfano katika Mikataba ya manunuzi ya Umma.
vi. Mikataba au kazi nyingi kuletwa katika mazingira ya dharura na hivyo kutotoa mwanya wa utafiti wa kina.
KUHUSU MUUNDO MAJUKUMU YA DISISHENI YA MIKATABA.
UTANGULIZI
Divisheni
ya Mikataba ni moja ya Divisheni katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Divisheni hii ya Mikataba ilianzishwa mwaka 2011, baada ya
Serikali kufanya mabadiliko ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kugawanya iliyokuwa Idara ya Madai na Sheria za Kimataifa;
Idara ambayo ilikuwepo tangu kuanzishwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria
mwaka 1976.
MUUNDO DIVISHENI.
Divisheni
hii inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na wakurugenzi wasaidizi wawili
ambao wanaongoza sehemu mbili za divisheni; “Contracts” na “Treaties”.
Divisheni ina mawakili wa Serikali ishirini (20)
LENGO LA DIVISHENI
Lengo
kuu la Divisheni ya Mikataba ni kutoa ushauri wa Kitaalam kuhusu
masuala ya Mikataba na makubaliano yanayoihusu Serikali. Katika
kutekeleza jukumu hili, divisheni kwa ujumla inafanya kazi zifuatazo;
i. Kuandaa na kushauri juu ya mikataba na Makubaliano mengine yanayoihusisha Serikali,
ii. Kutoa ushauri wa Kisheria kwa Serikali kuhusiana na makubaliano ya Kikanda,
iii. Kutoa
ushauri wa kisheria kwa Serikalki kwenye majadilano ya mikataba
yanayoihusisha Serikali au katika mikataba na makubaliano na majadilano
mengine ambayo Serikali ina manufaa,
iv. Kutoa ushauri wa kisheria kwa Idara na taasisi za Serikali kwenye mikataba na makubaliano mengine ambayo Serkali ina manufaa.
Aidha
kama tulivyosema awali, Divisheni hii imegawanyika katika sehemu mbili.
Kila moja ya sehemu hizi ina kazi maalum inazozitekeleza. Sehemu ya
mikataba ya kibiashara (Contracts) inafanya kazi zifuatazo:
i. Kutoa
ushauri wa kisheria kweye majadiliano ya mikataba na makubaliano
mengine ya kibiashara ambayo yanayoihusisha serikali mfano Madini,
miundombinu nk.
ii. Kutoa ushauri wa kisheria kwenye mikataba na nyaraka nyingine za kisheria ambazo zinaihusisha au Serikali ina manufaa.
iii. Kufanya utafiti wa kisheria kuhusu masuala yanayohusu mikataba ya Serikali.
iv. Kutoa ushauri wa Kisheria kwa idara na taasisi za Serikali kuhusu utekelezaji wa Mikataba yenye manufaa kwa Serikali.
v. Kuhakiki na kushauri juu ya mikataba ya manunuzi.
vi. Kuandaa
maoni ya kisheria pale ambapo kuna masharti ya awali katika utekelezaji
wa mikataba ya mikopo kutoka taasisi mabali mbali za kifedha.
vii. Kushauri
shirika la ubinafsishaji (CHC) kwenye mambo ya ubinafsishaji wa
makampuni yaliyochini yake na utekelezaji wa mikataba yake.
viii. Kushauri juu ya mikataba yote ya Serikali kabla ya kusainiwa.
Divisheni hii sehemu ya “ Treaties” inafanya kazi zifuatazo”
i. Kupitia na kutoa ushauri wa kisheria juu ya mikataba ya kikanda, bilateral na multilateral.
ii. Kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali kwenye mikataba na majadilano ya Mikataba ya Kimataifa ,
iii. Kutoa
ushauri wa kisheria kuhusu mahusianao na kazi za taasisi za jumuiya ya
kimataifa mfano; Umoja wa Mataifa, EAC, SADC, katika masuala ambayo
yanahitaji kutoa msimamo wa Serikali.
iv. Kufanya utafiti wa kisheria kuhusu mikataba ya Kimataifa.
v. Kutoa ushauri wa kisheria kwa Wizara, Taasisi za Serikali na kwa umma kuhusu masuala ya makubaliano ya kimataifa.
vi. Kushauri Wizara na taasisi za Serikali kuhusu mikataba ya kimataifa inayohitaji ridhaa ya bunge kabla ya kusainiwa,
vii. Kushauri Wizara na Taasisi zinazojitegemea kuhusu utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa.
0 comments:
Post a Comment