Waziri mkuu, Mhe. Mizengo Pinda akiongea na wanahabari jana jijini Arusha. Picha na Ahmed Mahmoud, Arusha
……………………………………………………………………
Arusha.
Serikali za Afrika zimeshauriwa kuridhia mikataba ya utekelezaji haki
za binadamu, ikiwamo kuruhusu mashirika yasiyo ya Serikali na watu
binafsi kuwafungulia kesi viongozi wanaodaiwa kukiuka haki za binadamu.
Akifungua semina ya majaji na
viongozi wa juu wa mahakama za haki za binadamu barani Afrika jana,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Tanzania kwa sasa ni kati ya Serikali
saba Afrika ambazo zimeridhia viongozi wake kufunguliwa mashtaka ya
haki za binadamu. Pia, ni kati ya nchi 26 barani Afrika ambazo
zimeridhia kuanzishwa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika.
Hata hivyo, Pinda aliwataka
majaji na watendaji wa Mahakama za barani Afrika, kuendelea kutekeleza
wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya haki, taratibu na Sheria.
Alisema Tanzania itaendelea kuunga mkono Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika yenye makao makuu yake jijini hapa.
Awali, Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mohammed Chande Othman alisema semina hiyo ina umuhimu mkubwa kwa
viongozi wa mahakama kubadilishana uzoefu juu ya utendaji na kwamba,
kuna mfumo unaofanana katika kutafsiri sheria za masuala ya ukiukaji
haki za binadamu.
Kuhusu mkataba wa kuwafungulia
kesi viongozi wa juu kwa ukiukaji haki za binadamu, Jaji Chande alisema
taratibu zimewekwa kwa kesi hizo kuanzia mahakama za kawaida za kila
nchi kabla ya kufikishwa Mahakama ya Afrika.
Naye Rais wa Mahakama ya Haki za
Binadamu Afrika, Sophia Akuffo alitoa wito kwa nchi zote za Afrika
kuridhia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu.
Pia,
alitaka kutambua haki za binadamu kwenye nchi hizo zinapaswa kuondoa
upungufu katika katiba zao na kuondoa vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binadamu.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment