Dar
es Salaam. Mgogoro ndani ya Chadema umezidi kupamba moto baada ya Kamati
Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo, huku Makamu
Mwenyekiti Taifa, Said Arfi akiandika barua ya kujiuzulu.
Zitto
alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati
Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa kukisaliti chama.
Taarifa zilisema hoja ya
kukisaliti chama pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kupita ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita
na ndiyo sababu ya kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa
chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto
na Dk Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini
wasifukuzwe uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge
wake wa Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
Zitto azungumza
Mara baada ya kumalizika kwa
kikao hicho, Zitto aliliambia gazeti hili, “Sina cha kueleza, kikao
kilikwenda vizuri na taarifa rasmi ya chama kuhusu uamuzi wa kikao
itatolewa baadaye mchana (jana saa nane mchana), tusubiri Kamanda.”
Arfi ajiuzulu
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said
Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, jana aliwasilisha
barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama, akisema; “…kuchoshwa na
unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu
masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya
Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa
marafiki.
Katika barua hiyo anasema
amechochwa na tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa katika uchaguzi wa
ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa kipindi kirefu zimekuwepo
shutuma dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri
Mkuu. Pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam
bado yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa
Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo
mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe?
Huu ni unafiki wa kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo,
Arfi anasema amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja
kwa jina moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
“Aidha
mmechukizwa sana kwa nini nilihoji kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei
kutuchagulia viongozi. Naomba ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo
wangu na utabakia hivyo siku zote kwa chama cha demokrasia kutoruhusu
uongozi wa kiimla kwa kukidhi matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama
kuwa mali binafsi.
Kwa kusema ukweli na kusimamia
ukweli daima itabakia kuwa lengo langu katika maisha yangu siku zote
hata kama itanigharimu maisha yangu.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willbroad Slaa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu barua ya
Arfi ya kujiuzulu uongozi, alisema; “Mimi nimekwishaondoka ofisini.”
Taarifa ya chama
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu
jana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema, Zitto, Dk Mkumbo na
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walikuwa na mtandao
wa kukiua chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za kuwachafua
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk Willbroad
Slaa.
Alisema kuwa kamati kuu ilibaini
kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao
umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, ambao
umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’.
“Kikundi hicho vinara wake wapo
wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba
(M3) na mtu mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa yeye anatumia jina la
M2” alisema Lissu.
Alisema wakati wa kuhojiwa na
Kamati Kuu Dk Mkumbo alikiri kuwa mhusika mkuu wa mtandao huo ni Zitto,
lakini Zitto alikana kuutambua waraka huo licha ya kueleza unamhusu kwa
kuwa umetaja jina lake, kauli ambayo alidai Kamati Kuu haikutaka
kuiamini.
Huku akieleza jinsi watu hao
walivyokuwa wakiwasiliana na kupanga mikakati ya kuimaliza Chadema kwa
siri chini ya ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto, Lissu alisema Naibu
Katibu Mkuu huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na Chama Tawala (CCM)
kuimaliza Chadema.
“Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni
mpango haramu na ambao unaichanachana katiba ya chama chetu. Ni mkakati
wa vita dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Hatuwezi
kunyamazia mkakati huu wa kutumaliza, uvumilivu umefika kikomo,”
alisema.
Uamuzi
Alisema kutokana na hali hiyo
kamati kuu iliamuru wahusika wote wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi
wa chama, kukubaliana kuunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa
sekretarieti ya makao makuu ya chama hicho ili kumtambua mtu wa nne
(M2).
“Kamati
ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa
nafasi zote za Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia
wote wanatakiwa kujieleza ndani ya siku 14 kwa nini wasivuliwe
uanachama na watapewa fursa ya kujitetea,” alisema.
Alisema Kamati Kuu itakutana kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali Mbowe alipinga madai kuwa
Zitto ameondolewa kwa kuwa alikuwa akitaka kugombea nafasi ya uenyekiti
wa chama hicho, akasisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kwa kuwa Chadema
ni chama cha watu, siyo mali ya mtu binafsi.
Mvutano Zitto, Lema
Kwa zaidi ya wiki mbili Zitto amekuwa akilumbana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Alimtuhumu mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho
nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye
Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya
chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya
kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Zitto alijibu kuwa tangu siku
nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa
na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC),
alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za
Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko
mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya
Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa
Idara ya Usalama wa Taifa kuihujumu Chadema.
Pia,
Zitto aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutuhumu vyama
vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu
za Serikali (CAG), huku akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
Chadema ilipinga vikali madai
hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi hiyo.
Vyama vinavyopata ruzuku ya Serikali ni vile vyenye wabunge Chadema,
CCM, UDP, TLP, CUF na NCCR-Mageuzi.
Mvutano kikaoni
Wakati wajumbe wa kikao hicho
wakivutana, Zitto alikuwa njiani akirejea kutoka Sudan Kusini, ambapo
alienda na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Taarifa kutoka ndani ya kikao
hicho zinaeleza kuwa, baada ya kuibuka sintofahamu hiyo, Mbowe
aliwapoza wajumbe wa kikao hicho, akiwaeleza kuwa haitakuwa busara
kumjadili mtu ambaye hayupo.
“Mbowe alipendekeza kuwa ajenda
hiyo iwekwe kando na itajadiliwa baadaye kutokana na Zitto kutokuwepo
katika kikao hicho,” zilieleza habari hizo.
Baadaye Zitto alituma ujumbe
ambao ulitangazwa kwa wajumbe wote, kwamba alikuwa njiani kurejea
Tanzania, kwamba akifika moja kwa moja atakwenda katika kikao hicho.
Zitto awasili, mzozo waibuka
Kama vile alikuwa akisubiriwa
yeye, mara baada ya kufika katika ukumbi huo saa 2:23 usiku huku
akisindikizwa na walinzi wanne, mvutano mkali uliibuka katika ukumbi huo
na mara kadhaa walinzi wa chama hicho, Red Brigade walionekana kukaa
tayari mlangoni kuzuia vurugu kama ingetokea.
Gazeti hili lilikuwa nje ya
ukumbi huo na mara kadhaa lilisikia sauti za malumbano za baadhi ya
viongozi wa chama hicho, akiwamo Zitto, Mbowe na Lema.
Wakati wakitoa maelezo kwa
nyakati tofauti Lema na Zitto walishutumiana huku kila mmoja akimtaja
mwenzake kuwa anatumia vibaya nafasi yake na mitandao ya kijamii.
“Tatizo lake ni kutumia mitandao
ya kijamii kueleza mambo ya chama wakati akijua siyo utaratibu, ugomvi
wangu naye kwa kiasi kikubwa uko hapo,” alisikika akisema Lema.
Kuna wakati yaliibuka malumbano makali huku sauti za juu zikisikika kutoka ndani ya ukumbi huo, kati ya Zitto, Lema na Mbowe.
Taarifa kutoka ndani ya kikao
hicho zinaeleza kuwa Dk Mkumbo alikumbwa na rungu hilo baada ya
kubainika kuwa alikuwa ameanda taarifa za siri ambazo zilikutwa katika
kompyuta mpakato (laptop) ya Mwigamba ambayo alinyang’anywa baada ya
kudaiwa alikuwa anasambaza taarifa za kuhujumu chama hicho.
Kikao hicho kilimalizika saa
10:00 alfajiri huku maamuzi hayo yakifanywa siri na Mbowe alipoulizwa
kuhusu kuwepo kwa taarifa za Zitto na Dk Mkumbo kuvuliwa uongozi,”
alisema , “Taarifa zitatolewa baadaye mchana.”
Wasomi wazungumza
Akizungumza na gazeti hili jana,
Profesa Gaudence Mpangala alisema Chadema ni chama kikubwa kinachoweza
kushinda uchaguzi mkuu ujao hivyo kinapaswa kuwa na viongozi
walioshikamana na kuwa na nia moja.
Aliongeza kuwa endapo wapo
viongozi wanaoonekana kwenda kinyume na viongozi wenzao na kwenda
kinyume na misimamo ya Chama, kinayo haki ya kufanya maamuzi ya namna
yoyote yenye lengo la kukinusuru.
“Chadema ni chama kikubwa
kinachoweza kushika dola…kinahitaji mshikamano mkubwa kwa viongozi wake
na kuhakikisha hawatokei wasaliti….kama ni kweli waliosimamishwa ni
wasaliti ni halali kabisa” anasema Profesa Mpangala.
Naye aliyekuwa Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha SAUT, Dk Charles Kitima alisema wakati umefika kwa vyama
vya siasa kutambua kuwa uwepo wa demokrasia ndani ya vyama vingi vya
siasa nchini ni kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima alisema kuwa na
mitazamo tofauti siyo usaliti ni demokrasia na kusema endapo mtu au
kiongozi anafanya kitendo cha kuvunja katika ya nchi huyo moja kwa moja
anakuwa mkosaji.
Mbunge wa Jimbo la Wawi (CUF),
Hamad Rashid anasema matukio ya kufukuzana na kutuhumiana baina ya
viongozi yanayofanywa na watendaji mkuu wa vyama vya upinzani
yatasababisha upinzani uzidi kudidimia na kudumaa.
Alisema vyama vya siasa vimekuwa
na usultani wa kuonekana kuwa vinapaswa kuongozwa na baadhi ya watu, na
wengine wenye uwezo na mawazo mapya na yasiyopendwa na wakubwa
anatafutiwa mbinu ya kuondoka.
Rashid alisema hali hiyo
inasababishwa na kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi ndani ya vyama
vya siasa, ambapo anasema vyama haviongozwi kama taasisi na badala yake
vinaongozwa kama mali za watu.
“Hili
linalotokea Chadema sasa ni matokeo ya mfumo mbovu wa uongozi ndani ya
vyama vya siasa nchini….vingi haviongozwi kama taasisi.” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment