Mamlaka
ya Mapato Tanzania iko katika msuguano na wafanyabiashara katika maeneo
mbalimbali nchini kutokana na mamlaka hiyo kuanzisha mfumo mpya wa
utoaji stakabadhi za kielektroniki kwa kutumia mashine ziitwazo EFD.
Ugomvi mkubwa wa wafanyabiashara
hao unatokana na bei inayodaiwa ni kubwa ya kununulia mashine hizo,
inayofikia Sh800, 000 kwa kila moja. Madai mengine ni kasoro za kiufundi
za mashine hizo na kitendo cha TRA kutumia mzabuni mmoja kuingiza
mashine hizo.
Jana mvutano huo ulipiga hodi
katika eneo maarufu kibiashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo
wafanyabiashara waligoma kufungua maduka kama ambavyo wamekwishafanya
wenzao katika mikoa ya Mbeya na Morogoro.
Pamoja na ufafanuzi wa TRA
kwamba baada ya majadiliano na wafanyabiashara bei za mashine za EFD
zimepungua hadi Sh600, 000 kwa kila moja, bado muafaka kamili
haujafikiwa.Tunaafikiana na ushauri unaotolewa na TRA kwamba mvutano huo
umalizwe kwa amani kwa njia ya mazungumzo na majadiliano baina ya
mamlaka hiyo na wafanyabiashara badala ya njia waliyoichagua ya migomo
na maandamano.
Tunaishauri TRA iendelee kutoa
majibu sahihi na kusisitiza umuhimu wa mashine hizo, huku ikitambua
kwamba hakuna mfanyabiashara anayelipa kodi akicheka, hivyo iwe imara
kusimamia mfumo huo mpya bila kuingiza ujanja ujanja unaoweza
kuikwamisha.
Kinachojitokeza bayana hapa ni
kuwapo mawasiliano hafifu baina ya TRA na wafanyabiashara. Kwa mfano,
wafanyabiashara bado wanadhani ni kampuni moja tu iliyopewa tenda ya
kusambaza mashine hizo, wakati ni kampuni 11 zilizopewa tenda hiyo.
Hakika, tatizo ni mawasiliano na TRA lazima ikiri udhaifu huo na
kuchukua hatua stahiki.
Uanzishaji wa mashine za EFD ni
mkakati sahihi wa ukusanyaji na usimamizi wa kodi, hasa katika maeneo
ambayo TRA haikuwa inayafikia. Ni uamuzi ambao utaliwezesha Taifa letu
kupata fedha za kutosha kujenga miundombinu na kuwaletea wananchi
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Tunashawishika kuamini kuwa,
hata mafanikio ambayo TRA iliyaeleza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya
Mlipakodi ya kuimarika kwa ukusanyaji mapato kutoka Sh4,049.1 trilioni
mwaka 2008/09 hadi Sh7,739.3 trilioni mwaka 2012/13, yamesaidiwa na
mashine hizo.
Kwa muda mrefu tumekuwa
tukikemea uzembe na usimamizi mbovu wa kodi uliosababisha maofisa wa TRA
kuacha fedha nyingi zikilala kwa wafanyabishara wa kati, badala yake
kila kukicha wakawa wanakimbilia makusanyo ya kuokota yanayotokana na
mishahara ya wafanyakazi.
Kwa mfano, tumewahi kushauri
kuwa vinahitajika vyanzo vipya vya mapato, kwa kuwatambua na kuwatoza
wafanyabiashara wa kada ya kati katika maduka, baa, saluni, bucha za
nyama, kumbi za starehe na harusi na maeneo kama hayo.
Mbali na kuongeza mapato, pia
tunadhani Serikali ingefanya juhudi za kuziba matundu na mianya ya
uvujaji wa mapato yake ili kuhakikisha kila kinachokusanywa kinaelekezwa
katika maendeleo ya nchi na wananchi, badala ya kutafunwa na mchwa
wasiojali masilahi ya umma.
Hatuna
shaka kwamba TRA ikijipanga inaweza kukusanya mapato zaidi, hasa
ikisimamia vizuri uamuzi wake wa kutumia EFD nchini kote na kuweka
utaratibu wa kudumu wa kufuatilia kwenye maduka kuona iwapo wanatoa
risiti hizo au la, maana tayari kuna madai kuwa wateja wanatakiwa
kuchagua kati ya kuuziwa bidhaa kwa bei ndogo bila risiti au kwa bei
kubwa na risiti za kielekroniki.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment