Na Mwandishi Wetu
MAASKOFU
wa makanisa mbalimbali nchini wametoa baraka zao za Tamasha la Krismas
linalotarajia kufanyika Desemba 25 mwaka huu, kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam na baadaye kufanyika katika mikoa minne hapa
nchini.
Viongozi
hao wa makanisa nchini Tanzania kwa nyakati tofauti wameahidi kuliombea
Tamasha la Krismas ili liwe la mafanikio yaliyotarajiwa kwa utukufu wa
Mungu.
Wanasema
tamasha hilo ni muhimu hasa katika nyakati hizi za uasi mwingi ambapo
dunia imekengeuka na kutenda matendo yanayomchukiza Mungu, kama vile
vitendo vya ugaidi, uuzwaji wa madawa ya kulevya na mauaji ya watu wasio
na hatia, hivyo tamasha hilo ili kurejesha utukufu wa Mungu mioyoni mwa
watenda mabaya.
Tamasha
la Krismasi ni muendelezo wa Tamasha la Pasaka lililoasisiwa tangu
mwaka 2000 kwa lengo la kufikisha neno la Mungu kwa wananchi kwa njia
muziki wa sifa na kuabudu.
Hatua
ya kuandaliwa kwa Tamasha la Krismasi ni baada ya kuwepo kwa matokeo
mazuri ya kupungua kwa matukio mbalimbali ya uhalifu na ukiukwaji wa
kanuni hapa nchini, hiyo ni kufuatia Tamasha la Pasaka ambalo mwaka huu
lilikwenda na kauli mbiu ya utii wa sheria pasipo shuruti.
Utofauti
wa Tamasha la Krismasi na Tamasha la Pasaka ni kwamba tamasha hili
waimbaji wote wataimba moja kwa moja ‘live’ lakini maudhui yatabaki kuwa
yale yale kama ya tamasha la Pasaka kumwabudu na kumtukuza Mungu kwa
njia ya uimbaji.
Makamu
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Magnus Mhiche
anasema Mungu amempa mzigo mzito Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex
Msama ambao anatakiwa awagawie waumini mbalimbali.
Sambamba na hilo Askofu Mhiche anampongeza Msama kwa hatua hiyo ya kuandaa matamasha ya kumtukuza na kumsifu Mungu.
Anasema
tamasha hilo si la dhehebu moja bali ni la Watanzania wote hivyo ni
vema kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuweza kuomba kwa pamoja kupitia
nyimbo.
Pia
Askofu Mkuu wa Kanisa la Oasis of Healing, Prosper Ntepa, pamoja na
kuliombea tamasha hilo aliwapongeza waandaaji wa tamasha hilo, Kampuni
ya Msama Promotions kwa kazi nzuri wanayoifanya katika uandaaji wa
matamasha makubwa ya kumuabudu Mungu hapa nchini.
“Msama
Promotions wanajitahidi katika uandaaji wa matamasha ya kumtukuza
Mungu, tunazidi kumuombea afanikishe tamasha la krismas ambalo
linatarajia kufanyika kwenye mikoa mitano hapa nchini,” alisema Askofu
Ntepa.
Askofu
Ntepa pamoja na kutoa pongezi kwa Msama alitoa wito kwa waimbaji
kutunga na kuimba nyimbo zenyemaudhui ya ujumbe mzito wenye tafsri
halisi ya krismass,na mlengo wa kumtukuza na kumuabudu Mungu kwa njia ya
sifa.
Askofu
Ntepa anasema ili kufanikisha hilo waimbaji wanatakiwa kujitambua kwa
jamii kwamba wanatakiwa kuwa mfano ambao utasaidia kufikisha neno la
Mungu ambalo baadhi ya waimbaji wanashindwa kwa sababu mbalimbali
ikiwemo tamaa ya pesa.
Aidha
Askofu Ntepa anasema ili Msama kufanikisha hilo inatakiwa kuchagua
waimbaji ambao wana dhamira ya kweli ya kufikisha ujumbe wa neno la
Mungu kwa waumini wengi zaidi.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa
la Living Water Centre, Onesmo Ndegi alitumia fursa hiyo kumpongeza
Msama kwa kufanikisha tamasha hilo ambalo ni mfano wa kuigwa kwa sababu
linafikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa maelfu ya Watanzania.
Askofu
Ndegi alisema yeye pamoja na viongozi wenzake wa dini pamoja na waumini
wake wanaungana na kumuombea Msama kwa sababu ni wajibu kama ilivyo
agizwa kwenye Biblia, kwani tamasha hilo ni ibada tosha kwa waliookoka
ingawa jamii inapata burudani na kumsifu Mungu kupitia nyimbo.
“Mimi
na kanisa langu nawaunga mkono Msama Promotions zaidi na nazidi
kuwaombea kufanikisha Tamasha la Krismasi kwa sababu wengi watashiriki
ibada ipasavyo,” alisema Askofu Ndegi.
Mwangalizi
Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima anasema jambo
lolote la kumuimbia na kumuabudu Mungu kupitia nyimbo ni jema.
Gwajima
anawashambulia wale wote watakaotumia tamasha hilo kama sehemu uiba
fedha kwani anaamini fedha zitakazopatikana kwenye tamasha hilo
litasaidia jamii mbalimbali ya Watanzania kama ilivyoagizwa na mwandaaji
ambaye ni Msama.
“Tamasha
la Krismasi ni sehemu ya mahubiri kwani kila anayehubiri anatakiwa
kuyatekeleza yale anayoyahubiri na si vinginevyo,” anasema Gwajima na
kuongeza;
“Namuombea Msama na kampuni zake kufanikisha matamasha yake ambayo ni sehemu stahili katika kumtukuza na kumuabudu Mungu,”.
Mchungaji
Christopher Mlaponi wa (TAG) Kinondoni Revival aliipongeza Msama
Promotions kwa sababu wao ndiyo waandaaji wakuu wa Matamasha ya
Kimataifa ya muziki wa injili kwa hatua waliyofikia.
Mchungaji
Christopher, anasema kampuni hiyo inastahili pongezi kwa kuanzisha
Tamasha la Krismasi kwa kuwa lina manufaa makubwa katika jamii hasa
katika siku hizo za sikukuu ya Krismasi.
Anasema
jambo la busara kwa kampuni hii kuanzisha matamasha ya muziki wa injili
kwa siku kama hizi ambapo aliwataka waumini kuitumia siku hiyo
kusheherekea Krismasi kwa kumtukuza Mungu kwa kushiriki katika tamasha
hilo na si kufanya vitendo viovu.
“Hii
siku siyo ya kula na kunywa, au kufanya anasa hapana, isipokuwa watu
wanatakiwa kwenda makanisani asubuhi kama inavyohitajika wakirudi
wajumuike katika Tamasha la Krismasi kwani wanapata neno la Mungu
kupitia nyimbo za injili” anasema .
Anasema hiyo siku hutokea mara moja kwa mwaka hivyo Wakristo wanatakiwa wamtukuze na kumuimbia Yesu kwenye tamasha hilo.
Naye
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama anasema tamasha hilo ni
muendelezo wa Tamasha la Pasaka, hivyo wadau wajiandae kupata ibada
stahiki kwa waumini mbalimbali watakaofika uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam na wengine wa mikoa minne hapa nchini ambayo ni Morogoro,
Dodoma, Tanga na Arusha.
“Tamasha
la mwaka huu litashirikisha waimbaji mbalimbali wa Tanzania na nje,
lengo likiwa ni ibada ambayo itawafikia waumini wote,” anasema Msama.
Msama
anawataja waimbaji waliothibitisha kushiriki katika tamasha hilo ni
pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro na Eiphreim
Sekereti huku waimbaji wengine wanaendelea na mazungumzo kwa ajili ya
kuthibitisha kushiriki.
0 comments:
Post a Comment