Dk Sengondo Mvungi.PICHA|MAKTABA
Hospitali ya Millpark ya
Johannesburg, Afrika Kusini, imesema madaktari waliokuwa wakimtibu
aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi
walibaini kuharibika kwa ubongo wake kutokana na kumwagika kwa maji
yanayoutunza ambayo kitaalamu yanaitwa ‘cerebrospinal fluids’ au CCF.
Msemaji wa Hospitali hiyo,
Tebogo Nyembezi alisema Dk Mvungi alicheleweshewa tiba baada ya kupata
tatizo la maji hayo yanayotunza ubongo kumwagika mara baada ya
kujeruhiwa.
Dk Mvungi (61), alipata majeraha
makubwa baada ya kujeruhiwa na watu waliovamia nyumbani kwake Kibamba,
Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu. Alifariki dunia
jana mchana.
“Maji hayo ambayo ni miligramu
50 tu katika ubongo wa mwanadamu ambayo huufanya ubongo uelee
yakimwagika nusu tu, basi mgonjwa yupo hatarini, lakini akiwahishwa na
kupata tiba sahihi anaweza kupona,” alisema Nyembezi.
Alisema iwapo mgonjwa atapewa
tiba sahihi ndani ya saa 48, ubongo wake unaweza kurudi katika hali ya
kawaida, lakini saa hizo zikizidi hawezi kupona kabisa kwa sababu maji
hayo yanapomwagika ubongo hujigonga kwenye mifupa ya sakafu yake na
kuharibika kabisa.
Mtaalamu wa mishipa na neva za
fahamu (neurosurgeon) katika Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Dk
Hariff Najin alisema kazi kubwa ya maji hayo ni kuulinda ubongo pindi
inapotokea ajali ili usidhurike lakini endapo maji hayo yatamwagika nao
huharibika.
“Haya maji yanaufanya ubongo
uelee na usielemee kichwa. Hivyo inapotokea maji haya yakaisha au
kupungua, ubongo hujigonga na kukosa ukinzani na kuharibika,” alisema.
Alisema maji hayo ambayo hufika
hadi kwenye uti wa mgongo yakikosekana katika ubongo, husababisha damu
isitembee kwenye eneo hilo jambo ambalo pia linaweza kusababisha mishipa
katika sehemu ya nyuma ya ubongo kuharibiwa.
Akizungumzia suala hilo,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya
Fahamu Muhimbili (Moi), Profesa Lawrence Museru alisema anachofahamu ni
kuwa Dk Mvungi alipelekwa Afrika Kusini kwa kuwa alipata madhara makubwa
kwenye ubongo na wala si kwa sababu ya kumwagika kwa maji kama
ilivyoelezwa Afrika Kusini.
“Majeraha hayo yalisababisha
damu kuvilia katika ubongo na kusababisha uvimbe ambao kwa kitaalamu
unaitwa ‘traumatic brain injury’ na sisi tulithibitisha vipimo hivyo vya
awali na kumsindikiza mpaka huko,” alisema Profesa Maseru.
Profesa Museru alisema Dk Mvungi
alipata majeraha makubwa kichwani na sehemu nyingine mwilini ambayo
yanaonekana yalisababishwa na kupigwa kwa vitu vyenye ncha kali au
magongo na hivyo kuleta madhara katika ubongo.
Alisema
hawezi kuthibitisha chanzo hasa cha kifo hicho kwani kinaweza kuwa ni
kuharibika kwa ubongo au sababu nyingine zilizotokana na tatizo hilo
(secondary causes).
Naye Dk Mugisha Clement ambaye
alimuhudumia Dk Mvungi alipofikishwa Moi na baadaye kumsindikiza hadi
Afrika Kusini, alisema kitaalamu kumwagika kwa maji yanayolinda ubongo
hakuwezi kuleta madhara kama aliyoyapata mwanasheria huyo, bali tatizo
lilikuwa ni kuvimba na kuvilia damu katika ubongo.
“Maji ya CSF hayakuwa sababu ya
kifo cha Dk Mvungi, sisi tulitambua tatizo la awali kuwa majeraha
yalisababisha kuvimba na kuvilia damu. Kitaalamu haiwezekani maji hayo
yakasababisha madhara makubwa,” alisema.
Kucheleweshwa kwa matibabu
Kuhusu kutokuwapo kwa opereta wa
mashine ya CT Scan inayotumika kupima ubongo siku ambayo Dk Mvungi
alipelekwa Moi, Profesa Museru alisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
Hata hivyo, alisema kukosekana kwake hakukusababisha au kuchochea madhara kwa Dk Mvungi.
“Ni kweli kutokuwapo kwa opereta
ni kosa lakini halikuwa na madhara kwa Dk Mvungi kwa sababu hakuwa
akihitaji upasuaji wa haraka. Lakini ni kosa limefanyika,” alisema
Profesa Maseru.
Alisema
matumizi ya CT Scan ni ya muhimu lakini, hata kipindi cha nyuma ambacho
wagonjwa walipata matatizo katika ubongo bado walitibiwa bila ya kuwapo
ulazima wa kupata huduma ya mashine hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment