Rais Jakaya Kikwete PICHA|MAKTABA
Rais Jakaya Kikwete ameitaka
Wizara ya Nishati na Madini kuacha urafiki wa dhambi na baadhi ya
wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo makubwa na badala yake wazingatie
sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumza katika siku yake ya
mwisho kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo wilayani Geita
katika Kijiji cha Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema kilio cha
wachimbaji wadogo hivi sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba sawa na
wachimbaji wakubwa hivyo kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria kwa
kuwafutia umiliki wenye maeneo ambayo hawayafanyii kazi.
“Mkiyatwaa watapiga kelele,
acheni wapige kelele lakini timizeni sheria. Masele (akimwangalia Naibu
Waziri Nishati na Madini Stephen Masele) na wenzako lazima mzingatie
sheria. Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji wadogo wachimbe.
Acheni kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye alieleza
kufurahishwa kwake na wachimbaji wadogo kuanza kuchimba kisasa alisema
sheria ya umilikaji wa maeneo ya utafiti na uchimbaji wa madini
inaelekeza kuwa iwapo mwombaji akija kuomba tena (renewal) leseni ya
eneo alilopewa anapaswa kulipunguza kwa asilimia 50 ili wapewe wengine
na vivyohivyo anapokuja kwa mara ya pili, pia anapaswa kupunguziwa eneo
lake kwa asilimia 50.
“Pamoja na kwamba sheria ipo
wazi, ukiwauliza wizara kwa nini hawafanyi hivyo, hawana maelezo wapo
kimya, sijui wanaingia kigugumizi gani kutimiza sheria hii.
Wanaposhindwa kufanya haya ni hasara kwa taifa maana haya madini
hayachimbwi, wangezingatia sheria hii na kuchukua maeneo haya wangewapa
wengine wakachimba leo tusingekuwa na kelele za wachimbaji wadogo,”
alisema. Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote
mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni
watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na
maendeleo kwa nchi.
Aidha, aliitaka wizara hiyo kuwa
makini wakati wa kutimiza matakwa ya sheria hiyo ya umiliki wa maeneo
ya uchimbaji, akitahadharisha kuwa wamiliki wengine wanaweza kubadili
majina pindi watakaponyang’anywa maeneo yao.
“Wana tabia ya kubadili majina,
mkimnyang’anya atakuja upya. Kama alikuwa anaitwa Kikwete & Sons
sasa atakuja tena anajiita SK lakini ndiye huyohuyo, tazameni sana.
Najua, mnayajua mengi maana na ninyi ni wabia wao lakini ninachotaka ni
kuzingatia na kusimamia sheria,” alisema.
Akizungumzia Mgodi wa Mzawa
alioutembelea, Rais Kikwete alisema amejionea jambo kubwa na la
kushangaza kiasi cha kusema kwamba iwapo angeishia kusimuliwa mambo hayo
na watu bila ya kufika, asingeamini kama Watanzania wanaweza kuendesha
migodi kama huo.
Alisema Serikali inathamini
mchango wao na kuwataka kujiandikisha Tume ya Uwekezaji ili nao waweze
kuomba msamaha wa mafuta na zana mbalimbali kama ilivyo kwa wawekezaji
wakubwa wa nje.
Awali,
Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano wa kuwapatia wachimbaji
wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa wanavyotumia havina tofauti na vile
vya wachimbaji wakubwa.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment