Mabingwa
wa Tanzania Bara, Yanga wamesema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na
ushindi wa 3-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha
Kamati ya Utendaji, Baraza la Wazee na matawi ya Yanga ya jiji la Dar es
Salaam kilichofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya klabu hiyo jijini
jana, msemaji wa matawi hayo, Bakili Makele alisema mipango ya ‘kumuua
mnyama’ imeshakamilika na wameshahakikishiwa kuibuka na ushindi wa
magoli 3-0 katika mchezo huo mgumu dhidi ya vinara wa ligi.
“Leo
(jana) tumekutana matawi yote ya Yanga ya Dar es Salaam, Baraza la
Wazee na Kamati ya Utendaji kujadili namna ya kumuua Mnyama.
Tumepokea
taarifa kutoka kwenye Kamati ya Utendaji, Sekretarieti na Baraza la
Wazee la Yanga kwamba mipango yote inakwenda vizuri, hakuna matatizo
kwenye timu na hatuna majeruhi hata mmoja. Tunapiga magoli matatu
Jumapili,” alisema Makele.
“Tunaomba nidhamu kwa wanachama na mashabiki wa Yanga siku hiyo.
Tunaomba pia refa na wasaidizi wake siku hiyo wawe makini maana
wapinzani wetu mechi zao ni za penalti. Kila mechi wachezaji wao
wanajiangusha na kupewa penalti zisizo halali,” alisema zaidi Makele,
ambaye pia ni kiongozi wa Tawi la Yanga la Temeke.
Naye
Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali aliahidi ushindi
mnono siku ya Jumapili katika mchezo huo na kubainisha kuwa viongozi,
makocha na wachezaji wameshamaliza kazi na kilichopo kwa sasa wao
wanamalizia kazi ili kunogesha ushindi huo.
“Yanga tuna tamaduni zetu, sehemu yoyote ile ina asili yake, hivyo kwa
hivi sasa sisi wazee kwa pamoja tunaahidi lazima tumchinje mnyama
Jumapili. Uwezo na nia tunayo, hivyo washabiki wa Yanga mje kwa wingi
Uwanja wa Taifa kuishangilia timu yetu” alisema Akilimali.
“Baada ya kufungwa 3-2 na Azam, nilisema kwamba Yanga sasa inaanza ligi.
Watani wetu wanaweweseka kuona ‘speed’ (kasi) yetu ni ya hali ya juu,
tunachoomba ni waamuzi kuchezesha soka kwa kufuata kanuni 17 za mchezo.
Yanga si timu ya kuhurumiwa na marefa, na kama watafuata sheria 17 za
soka, basi lazima tumchape mnyama.
“Watani wetu walitufunga 5-0, sisi (Yanga) hatutawafunga magoli hayo
katika mchezo mmoja bali tutajibu kwa kushinda michezo mitano mfululizo
dhidi ya Simba. Hapo tutaona nani atakayeumia zaidi; aliyefungwa 5-0
katika mchezo mmoja au aliyepoteza michezo mitano mfululizo,” aliongeza
Akilimali.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa kikosi chao
kinaendelea vizuri na mazoezi kisiwani Pemba kujiandaa kwa mchezo huo
utakaochezeshwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka
(FIFA) Israel Nkongo wa Dar es Salaam, ambaye aliwahi kukunjwa na
kupigwa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo wa ligi hiyo
waliyolala 3-1 dhidi ya Azam FC msimu wa 2011/12.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh aliiambia NIPASHE akiwa Pemba baada ya
mazoezi ya jana kuwa wachezaji wote 29 walioidhinishwa kuitumikia Yanga
msimu huu wako ‘fiti’ kwa ajili ya mchezo huo utakaokuwa wa tatu (wa
watani) kwa kocha Mholanzi Ernie Brandts tangu atue Septemba mwaka jana
kuchukua mikoba ya kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyetimuliwa.
Mholanzi huyo aliyetua Yanga akitokea klabu ya ‘maafande’ wa APR ya
Rwanda aliyoifundisha tangu 2010, aliiongoza Yanga kuichapa Simba 2-0
katika mchezo wao wa mwisho wa kufunga msimu uliopita wa Ligi Kuu ya
Vadacom Tanzanbia Bara iliyochezwa Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga
zilieleza kuwa kikosi chao kitaingia Dar es Salaam muda wowote kuanzia
leo jioni kikitokea Pemba tayari kwa mchezo wa keshokutwa.
“Timu itatua Dar es Salaam kwa ndege muda wowote kuanzia kesho (leo)
jioni na itafikia kwenye moja ya hoteli nzuri za jiji hili kuendelea na
kambi,” alisema mmoja wa ‘vigogo’ wa Yanga ambaye aliomba jina lake
lisitiriwe.
SIMBA WAJIBU MAPIGO
Kwa upande mwingine, uongozi wa Simba umesema hautishwi na tambo za watani wao wa jadi na umejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza saa 10:00 alasiri.
Kwa upande mwingine, uongozi wa Simba umesema hautishwi na tambo za watani wao wa jadi na umejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza saa 10:00 alasiri.
Mmoja
wa viongozi ‘wazito’ wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa
kuwa si msemaji wa klabu hiyo iliyoanzishwa 1936, alisema wamejipanga
vizuri kuhakikisha wanaishangaza Yanga kwa kuishushia kipigo kikali
Jumapili.
“Yanga wanaongea kujifurahisha. Katika mpira huwezi kusema unaingia
uwanjani ukijua unashinda 3-0. Timu yetu imeandaliwa vizuri ili iibuke
na ushindi dhidi yao,” alisema kiongozi huyo huku akiweka wazi kuwa
kikosi cha Simba kimeweka kambi yake Bamba Beach. Kigamboni jijini Dar
es Salaam kujiandaa kwa mchezo huo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment