WAZIRI
MKUU Mhe. Mizengo Pinda anaondoka Dar es Salaam leo mchana (Jumanne,
Oktoba 15, 2013) kwenda China kwa ziara ya kikazi ya siku tisa kwa
mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa kuanza kesho, Oktoba 16.
Kwa
mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, lengo la ziara ya Waziri Mkuu ni kutangaza fursa za
uwekezaji hapa nchini, fursa za biashara, za utalii na kutafuta mitaji
kwa ajili ya sekta zilizo chini mpango wa matokeo makubwa ya haraka (Big
Results Now Initiative).
Akiwa
China, Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo,
Mhe. Li Keqiang na viongozi wa Serikali ya China katika katika sekta za
uchukuzi, mawasiliano, viwanda, madini na nishati.
Atatembelea
mji wa Beijing na majimbo ya Shenzen, Chengdu na Guangzhou ambako
atakutana na Makamu wa Rais wa China, Rais wa Benki ya Exim ya China,
Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, wakuu wa mashirika makubwa na
kampuni kubwa nchini China na kufanya nao mazungumzo.
Waziri
Mkuu Pinda ataungana na Wakuu wa Nchi watano kwenye ufunguzi wa
maonyesho ya kibiashara ya magharibi mwa China (Western China
International Fair – WCIF) ambako atahutubia washiriki wa maonyesho
hayo. Pia atatembelea maeneo kadhaa ya uwekezaji na kufungua Kongamano
la Uwekezaji baina ya Tanzania na China litakalofanyika Guangzhou.
Vilevile,
Waziri Mkuu anatarajiwa kufungua mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20
kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa
pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya
Tanzania. Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha
utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ).
Waziri
Mkuu ambaye anafuatana na Mawaziri wanne, wabunge wawili, wakuu wa
mikoa watatu, wakuu wa taasisi wa Serikali na wawakilishi kutoka sekta
binafsi, anatarajiwa kukutana na Watanzania waishia China huko Beijing
na Guangzhou.
Tanzania imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na China, nchi kubwa ya Bara la Asia, tangu mwaka 1964.
China yenye ukubwa wa kilometa za mraba 9,596,961 ina wakazi wapatao 1,349,585,838. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika Fedha la Kimataifa (IMF) nchi hiyo ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, OKTOBA 15, 2013
0 comments:
Post a Comment