Naibu
Kamishna wa Madini toka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ally
Samaje (KULIA) Akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu uanzishwaji wa
Mradi wa Uchimbaji Madini ya Urani eneo la mto Mkuju, Wilaya ya Namtumbo
Mkoani Ruvuma, wakati wa Mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam
katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara
ya Habari (MAELEZO) Bw. Assa Mwambene.
Picha na Georgina Misama-Maelezo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Utangulizi
Kulingana
na shughuli za utafutaji madini zilizofanywa miaka ya nyuma hadi sasa
zimebainisha madini ya urani kuwepo katika maeneo mbalimbali ya nchi
yetu. Maeneo hayo ni pamoja na Mto Mkuju (Namtumbo); Madaba (Liwale);
Bahi (Dodoma); Gallapo (Babati); Milima ya Uluguru (Morogoro); na Itigi
(Manyoni). Madini hayo yanaweza kugundulika katika maeneo zaidi kutokana
na shughuli za utafutaji zinazofanywa pamoja na taarifa zaidi za
kijiolojia zinazoendelea kutayarishwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania.
Hata hivyo, hadi sasa eneo la Mto Mkuju ndilo limeonekana kuwa na
mashapo ya madini ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara. Pamoja na
matokeo ya awali kuonesha kuwa yapo madini ya urani yanayoweza kuchimbwa
kibiashara bado utafutaji zaidi unahitajika ili kupata mashapo zaidi
yatakayoweza kuchimba kwa muda mrefu.
Mradi wa Urani wa Mto Mkuju
Kulingana
na utafiti wa kina wa madini ya urani uliofanywa katika eneo la mradi
huu umegundua mashapo yanayoweza kuchimbwa kibishara. Hadi sasa kiasi
cha tani milioni 175.8 za mashapo (Measured, Indicated na Inferred) ya urani kimegunduliwa. Kiasi hicho ni sawa na pound milioni 115.8 (kilo milioni 52.5) za urani kwa grade ya 298.8 U3O8ppm. Kulingana na mashapo haya uhai wa mgodi kwa sasa ni miaka 12.
Mradi
wa Mto Mkuju unamilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, Kampuni
tanzu ya URMZ ya Urusi. Kampuni ya URMZ ni Kampuni ya Serikali ya
urusi. Mradi wa Mto Mkuju uko ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous (Selous Game Reserve). Pia eneo hilo ni Sehemu ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Mwezi Julai, 2012, World Heritage Committee
iliyoko chini ya UNESCO ilitoa idhini ya kuondoa eneo la Mradi wa Mto
Mkuju kwenye Eneo la Urithi wa Dunia ili uchimbaji wa urani uweze
kufanyika. Hata hivyo, eneo hilo litaendelea kuwa ndani ya eneo la
Hifadhi ya Wanyamapori la Selous.
Kutokana
na hatua hiyo, uchambuzi wa masuala ya mazingira ulikamilika mwezi
Oktoba, 2012 ambapo Hati ya Mazingira (Environmental Impact Assessment
Certificate) ilitolewa na Baraza la mazingira la Taifa (NEMC). Baada ya
hatua hizo kukamilika, Wizara ya Nishati na Madini ilitoa leseni ya
uchimbaji madini ya urani tarehe 05 Aprili, 2013. Leseni hiyo inaruhusu
shughuli za uchimbaji kufanyika katika mradi huo. Majadiliano kuhusu
mkataba wa kuendeleza uchimbaji madini kuhusu mradi huo yanaendelea.
Uchimbaji wa madini ya urani katika mradi wa Mto Mkuju utafanyika hadi hatua ya yellow cake.
Baada ya hapo urani hiyo itasafirishwa kwenda nje ya nchi katika maeneo
ambayo urutubishaji wa madini hayo kwa matumizi mbalimbali kama vile
kuzalisha umeme, kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya,
Kilimo, Ujenzi na Mifugo utafanyika.
Manufaa
mbalimbali yanatarajiwa kutokana na uchimbaji wa urani katika mradi huo
ikiwa ni pamoja na mrabaha (Dola za marekani zaidi ya milioni 190);
Kodi (Dola za Marekani zaidi ya milioni 363); PAYE (Dola za marekani
zaidi ya milioni 50). Mapato mengine ni pamoja na Kodi ya zuio
(Withholding taxes), gawio (dividend), Import duties, Service levy
kwenye Halmashauri ya Namtumbo, n.k. Hata hivyo, mapato haya yatatokana
na hali ya bei ya urani katika soko la dunia. Manufaa mengine ni ajira
kwa watanzania zaidi ya 690.
Udhibiti wa shughuli za urani
Tungependa
kuwahakikishia Watanzania na wananchi wanaoishi karibu na maeneo
yaliyogundulika kuwepo na madini ya urani kwa kiwango cha kuchimbwa
kibiashara, kwamba Serikali imechukua hatua kadhaa za kuweka mazingira
wezeshi kwa ajili ya shughuli za utafutaji, uchimbaji na usafirishaji
nje ya nchi madini ya urani. Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-
- Kuwepo kwa Sheria za Madini, 2010 ambapo madini ya urani na madini mengine yanayotumika kuzalisha nishati, mfano makaa ya mawe yanatambuliwa kama kundi pekee la energy minerals. Tofauti na madini mengine, sheria imezuia utoaji wa leseni ya biashara ya madini (Dealer Licences) kwa madini ya urani kutokana na unyeti wa madini hayo.
- Kuwepo kwa Kanuni maalum za the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 zimetungwa (GN. 407 dated 22/10/2010) kuhakikisha kuwa kampuni zinazowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani zinafuata maelekezo maalum yanayohusu utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini hayo. Vilevile, Kanuni hizo zinaelezea majukumu ya mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za TAEC na NEMC, na Wizara zinazosimamia rasilimali za Maji na Madini. Madhumuni makuu ni kuhakikisha kuwa shughuli hizo haziathiri usalama, afya na mazingira yetu na uhusiano wetu na jumuia za kimataifa, ikiwa ni pamoja na IAEA.
- Kuwepo kwa Sheria na kanuni chini ya Tanzania Atomic Energy Commission (TAEC) ambazo zinahakikisha kuwa kunakuwepo na uthibiti wa viwango vya mionzi ambavyo vinaweza kuathiri binadamu. Aidha, watahakikisha kuwa ufungaji katika mapipa na usafirishaji wa urani unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyokubalika.
- Kanuni za Usalama, Afya na Mazingira Migodini zilizotungwa kwa GN Na. 408 ya tarehe 22/10/2010 zimehifadhi kanuni namba 187 – 190 zilizokuwa kwenye kanuni za mwaka 1999 zinazokusudia kusimamia usalama wa shughuli za utafutaji wa madini ya urani na mengineyo yenye mionzi ayonisha. Kanuni hizo zimeweka mfumo wa kushirikisha jamii inayozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa madini hayo.
Taarifa Potofu kuhusu urani
Wapo watu mbalimbali hasa Wanaharakati kama vile Mtaalam wa Uranium Network Organization
ya Ujerumani Bw. Gunter Wippel ambao wamekuwa wakieneza taarifa potofu
kuwa uchimbaji wa madini ya urani nchini Tanzania utasababisha madhara
mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
a) Kansa ya ini;
b) Kuzaliwa watoto wenye viungo pungufu au zaidi; na
c) Kubadilika kwa DNA.
Madai hayo sio ya kweli ukizingatia kuwa Tanzania baada ya kuyachimba madini hayo na kuyasafisha kwa kiwango cha yellow cake
haitaendelea na hatua zinazofuata za kurutubisha madini hayo na
kuyafikisha katika kiwango na mfumo wa kuwezesha kuzalisha umeme ama
kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo, Ujenzi na
Mifugo. Hatua hizi za urutubishaji na matumizi yake katika kutengeneza
vifaa hivyo zitafanyika katika nchi zilizoendelea kama vile Japan,
Ufaransa, Urusi, n.k. Katika hatua hizo ndipo huzalishwa mabaki (highly enriched uranium wastes) ambayo yasipodhibitiwa kwa kiwango cha kuridhisha huweza kusababisha madhara yanayoongelewa.
Uchimbaji na usafirishaji wa madini ya urani katika hali ya yellow cake
hayana madhara kwa kiwango hicho kinachoelezwa na Wanaharakati. Madhara
yanayoweza kujitokeza katika shughuli hizo za uchimbaji na usafirishaji
ni madhara ya kawaida kwa kila eneo ambapo shughuli za uchimbaji madini
yawe ya dhahabu, urani, chokaa ama makaa ya mawe huweza kujitokeza. Ni
madhara ya kiusalama kama vile ajali ama mazingira kuchafuliwa na
kemikali ikiwa wawekezaji na Serikali watazembea katika usimamizi wa
shughuli hizo.
Madhara
pekee maalum kwa shughuli za uchimbaji urani ni wizi unaoweza kutokea
wa mapipa ya urani wakati wa usafirishaji na hivyo uzagaaji wa madini
hayo nje ya mkondo wa Serikali na udhibiti wa Kimataifa kupitia Shirika
la IAEA. Ndio maana katika usafirishaji wa madini hayo, Taasisi ya TAEC,
Jeshi la Ulinzi, Usalama wa Taifa, Idara ya Polisi na Idara ya Madini
watahusika kwa pamoja kuhakikisha madhara kama hayo hayatokei na
yakitokea hatua za haraka kudhibiti madhara hayo zinachukuliwa.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
0 comments:
Post a Comment