Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa |
Mahakama
Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema itatoa uamuzi Desemba 12,
mwaka huu dhidi pingamizi zitakazowasilishwa na upande wa mlalamikiwa
kwa njia ya maandishi dhidi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Kinana anamtaka Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa, kufuta matamshi ya kumkashifu, kumfedhehesha na kumhusisha na
ujangili wa meno ya tembo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke, baada ya kuziamuru
pande zote mbili kuwasilisha majibishano ya kisheria kuhusu pingamizi
hizo.
Jaji
Muruke alisema upande wa mlalamikiwa Mchungaji Msigwa, kupitia wakili
Peter Kibatala, uwasilishe pingamizi lao kwa njia ya maandishi Oktoba
14, mwaka huu na wakili Eric Ng’maryo wa mlalamikaji Kinana ajibu
pingamizi hizo Novemba 11, mwaka huu.
“Baada ya pande zote mbili kuwasilisha pingamizi na majibishano ya
kisheria kwa njia ya maandishi, mahakama hii itatoa uamuzi wake Desemba
12, mwaka huu” alisema Jaji Muruke.
Katika kesi ya msingi, Kinana kupitia wakili Ng’maryo, amemtaka
Mchugaji Msigwa, kufuta matamshi hayo aliyoyatoa Aprili 21, mwaka huu,
katika mkutano wa hadhara wa kisiasa uliofanyika katika uwanja wa Shule
ya Msingi Mbugani, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Wakili huyo wa Kinana, amemweleza Mchungaji Msigwa kuwa hana kinga ya
Bunge kwa matamko yake dhidi ya Katibu Mkuu huyo wa CCM, maana hotuba
yake bungeni ilidhihirisha kashfa aliyoitamka wakati akiwa nje ya Bunge.
“Umma unaamini matamko yako (Msigwa) na hawayachukulii kwamba ni upuuzi
wa mtu asiyekuwa makini au ni ujanja ujanja na porojo za kisiasa,”
ilisema sehemu ya taarifa ya wakili huyo.
Wakili huyo alisema Kinana ana nia ya kumfungulia kesi ya madai
Mchungaji Msigwa ili uchafu alioupaka kwenye jina lake, usafishwe
kisheria na awajibishwe kwa madhara na hasara alizozipata.
Wakili huyo amemweleza Msigwa kuwa kama atakuwa na ujasiri na uungwana
wa kufanya hivyo, basi Kinana ataacha kumfungulia kesi ya madai.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment