
Hayo
yamebainika jana jioni (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) wakati Makamu Rais wa
Bodi ya Tumbaku ya China, Bw. Yang Peisen alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika nyumba
ya wageni ya Serikali ya Diaoyutai jijini Beijing, China. Bodi hiyo ya
Tumbaku (State Monopoly Tobacco Administration – STMA) ndicho chombo cha
juu cha maamuzi kuhusiana na zao hilo.
Akizungumza
na Bw. Peisen na msafara wake pamoja na baadhi ya viongozi kutoka
Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu aliwasihi waangalie uwezekano wa
wafanyabiashara wa China kujenga kiwanda cha kutengeneza bidhaa za
tumbaku katika maeneo ya Songea na Tabora ambako Tumbaku inalimwa kwa
wingi ili kuwasaidia wakulima wa maeneo hayo na mikoa ya jirani.
“Ndoto
yangu ni kuona kampuni za China zinakuja kujenga kiwanda Tanzania,
mkilifanya hili mtakuwa mmetusaidia sana kuondoa umaskini miongoni mwa
wakulima na utakuwa ndiyo ukombozi kwa wakulima wetu,” alisema Pinda.
Alisema
sasa hivi kuna kiwanda kimoja tu cha kutengeneza sigara ambacho kiko
Dar es Salaam na kwamba mahitaji ya kiwanda ni madogo kuliko kiasi cha
tumbaku inayozalishwa nchini hali inayowafanya wakulima wahangaike
kutafuta masoko.
Kwa
upande wake, Bw. Peisen alisema vikwazo vya kiufundi ambavyo vilikuwa
vikizuia tumbaku ya Tanzania isiingie katika soko la China hivi sasa
havipo kwani mwaka jana walituma timu ya wataaalamu kuja Tanzania ili
kupata sampuli za tumbaku na kuangalia jinsi zao hilo linavyopakiwa
(packaging).
Alisisitiza haja ya zao hilo kuwa na ubora unaostahili ili liweze kupata soko katika nchi hiyo.
Naye,
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bw. Wilfred Mushi ambaye
yuko kwenye msafara wa Waziri Mkuu, alimhakikishia Bw. Peisen suala la
ubora wa tumbaku na kusisitiza kuwa soko la China ni muhimu kwa Tanzania
kwani kwa sasa wanauza katika nchi za Ulaya tu na wakati mwingine soko
la huko linayumba na hivyo kumwingizia hasara mkulima.
Alisema
China ni taifa linalolima kwa wingi tumbaku; lakini pia watu wake
wanavuta sana sigara hivyo bado wanahitaji bidhaa hiyo kutoka nje ya
nchi. “Tukipata soko la China kutakuwa na ushindani wa magharibi na
mashariki na wakulima wetu watapata bei nzuri,” alisema Bw. Mushi.
Alisema
makampuni matatu kutoka Tanzania yalishajaribu kuomba kuuza bidhaa hiyo
nchini China lakini yaligonga mwamba kutokana na ukiritimba ambao STMA
ilikuwa imeweka. Aliyataja makampuni hayo kuwa ni Tanzania Tobacco Leaf Company (TLTC), Alliance One na Premium America.
Katika
ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji
na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah
Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na
Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri
wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia
amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman
Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili,
Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi
wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 19, 2013
0 comments:
Post a Comment