STRAIKA
wa Simba, Mrundi Amisi Tambwe, amewaambia Yanga kuwa wanamtafuta ubaya
na atawakomesha Jumapili, timu hizo zitakapoumana Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Tambwe, ambaye ni kinara wa
mabao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu hadi sasa, anaongoza kwa
kutikisa nyavu mara nane na hiyo Jumapili atakuwa na kazi ya
kuinyamazisha Yanga ambayo viongozi wake wametoa ahadi nzito za
kushinda.
Akizungumza na Mwanaspoti,
Tambwe alisema: “Yanga itambue kuwa sisi ndiyo tunaongoza ligi na
tunawazidi kwa kila kitu. Kwa upande wangu niko vizuri, ninamwomba Mungu
anipe afya njema hadi Jumapili ili niwafunge mabao na kuwafunga midomo
yao.
“Wanapaswa kufahamu kuwa mpira
hauchezwi kwa maneno ila ni dakika 90 za uwanjani, kama wakishinda ndiyo
wazungumze na sisi tukifungwa tutanyamaza.
“Kwa upande wangu kama straika,
maneno ya Yanga hayanitishi kwani mimi ni mchezaji mkubwa na simwogopi
yeyote, wachezaji wote wanaocheza ligi hapa viwango vyao vinalingana,
hakuna jipya.”
Kuhusiana na madai kuwa mara
nyingi mechi hiyo huwa pia na mambo ya kishirikina, Tambwe mwenye mabao
nane mpaka sasa alisema: “Siogopi kitu ushirikina, kwangu uchawi wa soka
ni mazoezi na maandalizi tu.”
Akiizungumzia safu ya ulinzi ya
Yanga yenye akina Kelvin Yondani ‘Vidic’ na Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
alisema: “Kama nilivyosema simwogopi yeyote.”
Kwa upande wao mabeki hao kwa nyakati tofauti wameahidi kumdhibiti Tambwe wakisema hatafanikiwa kuwapita.
Naye Kocha Mkuu wa Simba,
Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ alisema: “Nipo kambini kwa ajili ya kuandaa
timu yangu iweze kishinda na sijui ya wengine.”
Beki wa kati wa Simba, Mrundi
Kaze Gilbert, ametamka kuwa, safu yao ya ulinzi ipo kamili na mechi
dhidi ya Yanga watahakikisha wanakaba kila kitu hadi kivuli.
Kaze anacheza beki ya kati
pamoja na Joseph Owino raia wa Uganda ambapo katika mechi hiyo na Yanga,
kazi yao kubwa itakuwa ni kupambana na washambuliaji wa kati wa Yanga
akina Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Jerry Tegete.
“Mechi hiyo ni ngumu, lakini safu yetu ni imara kuhakikisha hatutoi nafasi yoyote.
Hatutakariri
majina ya wachezaji siku hiyo, bali tutakaba kila kitu, si unajua
unaweza kusema nitadili na mtu fulani lakini madhara yanaweza kutokea
mahali pengine, tutacheza kwa kufuata maelekezo ya kocha,” alisema.
CHANZo: MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment