WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema katika kipindi alichokaa ofisini na
kushughulikia suala la dawa za kulevya amebaini kuwa tatizo la matumizi
ya dawa hizo linakuzwa kwa kiasi kikubwa na hulka ya watu kutaka kupata
utajiri wa haraka.
Ametoa
kauli hiyo jana usiku (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) wakati akizungumza na
Watanzani waishio jijini Beijing, China alipokutana nao kwenye ubalozi
wa Tanzania nchini China. Waziri Mkuu jana alikuwa katika siku ya tatu
ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi
hiyo.
Amesema
wahusika wa biashara hiyo wana siri kubwa na wanakula kiapo kwani wengi
wao wako tayari kufa lakini hawako tayari kuwataja wale waliowatuma
kupeleka mizigo yao.
“Biashara
hii imetawaliwa na usiri mkubwa… watu hawako tayari kutajana. Wako
radhi kufa. Changamoto tuliyonayo ni kuangalia kwa namna gani tunaweza
kupunguza shauku hii ya matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.
Waziri
Mkuu alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Bi. Fatma Matulanga ambaye
yuko masomoni nchini China kutaka kujua ni hatua gani ambazo Serikali
imechukua kuhusiana na suala la vijana 175 waliokamatwa nchini China
yakiwemo makosa ya kukutwa na dawa za kulevya ambayo adhabu yake ni
kifo.
Alisema
kama taratibu zinaruhusu, maafisa walioko ubalozini wafanye jitihada ya
kuonana na vijana hao na kuwasikiliza ili waweze kuona namna gani ya
kupata taarifa sahihi na kama wako tayari kuwataja wale waliowatuma.
Awali,
Waziri Mkuu alielezwa na Bi. Matulanga kwamba balozi aliyekuwepo China,
Bw. Philip Marmo aliahidi kutuma viongozi wa dini kwenye magereza hayo
ili wawasikilize vijana hao na kuona wanaweza vipi kuwasilisha taarifa
zao Serikalini.
Alisema
Rais Jakaya Kikwete aliunda kikosi maalum cha kudhibiti dawa za kulevya
ambacho kimekuwa kikifanya kazi nzuri. Alitoa rai kuwa endapo kuna mtu
ana taarifa zozote ama kuwafahamu watu wanaojihusisha na biashara hiyo,
apeleke taarifa kwenye kikosi hicho nao watafanya uchunguzi wa kina ili
kubaini ukweli na hatua stahiki zitachukuliwa.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania hao wa ughaibuni hatua
mbalimbali za kisiasa na kiuchumi ambazo nchi imepitia katika siku za
hivi karibuni. Pia aliwagusia kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya na
hatua iliyofikiwa.
Katika
ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji
na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah
Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na
Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri
wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia
amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman
Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili,
Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi
wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.
0 comments:
Post a Comment