Naibu Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Bw.Edwin Mikongoti akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa serikali
wa kukasimu madaraka kwa wakuu wa shule, vyuo na walimu wakuu kuhusu
usimamizi wa utumishi wa walimu ili kuongeza ufanisi,wakati wa Mkutano
uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO).
Katibu
Msaidizi, Idara ya Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma(kulia)
akiwaeleza waandishi wa habari faida za mfumo wa ugatuaji madaraka ikiwa
ni pamoja na kuongeza ufanisi sehemu za kazi.wakati wa mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, katika ukumbi
wa Idara ya Habari(MAELEZO).kushoto ni Katibu Msaidizi, Idara ya
Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Evelyne Omari. Picha na Georgina Misama-Maelezo
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tume ya Utumishi wa Umma
imepewa dhamana ya kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na
Nidhamu zinatekeleza mamlaka waliopewa ya usimamizi na uendeshaji wa
Rasilimali watu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika
Utumishi wa Umma ili kuimarisha Utawala bora na Uwajibikaji.
Idara ya Utumishi wa Walimu
ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya 2002
Kifungu 6(4), Kanuni Na. 6(h) na Na. 35(2)(b) za Kanuni za Utumishi wa
Umma za Mwaka 2003 imepewa Mamlaka ya Kushughulikia Masuala ya Ajira na
Nidhamu kwa Walimu wote walio katika Utumishi wa Umma.
Kwa
Mujibu wa Kifungu 21(2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka
2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.18 ya Mwaka 2007 na kwa Kanuni
Na.118 ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya mwaka 2003, Tume ya Utumishi wa
Umma imepewa uwezo wa kukasimisha madaraka yake kwa Wakuu wa Shule, Vyuo
na Walimu Wakuu. Masuala yanayokasimishwa ni yale ya kiutumishi na
ushughulikiaji wa makosa madogo madogo ya kinidhamu kwa Walimu na
Wakufunzi walio vyuoni, Walimu wa Shule za Sekondari na Shule za Msingi.
Ili
kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya kiutumishi Wakuu wa
Vyuo vya Ualimu/ Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wakuu wa Shule na Walimu
Wakuu wanatakiwa kuwajibika katika kuwaelimisha Walimu taratibu za
masuala ya ajira katika maeneo ya:- Ajira na Usajili; Kuthibitisha
kazini Walimu; Kubadilisha kazi/cheo Walimu; Kupandisha vyeo Walimu.
Aidha
watashughulikia pia makosa madogo madogo ya kinidhamu na kutoa adhabu.
Madaraka yamekasimiwa kwa makosa ambayo kama yakithibitika adhabu zake
kwa mujibu wa Kanuni Na. 118 ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003
zitakuwa ni:- Onyo; Kusimamisha nyongeza ya mshahara; Kufidia hasara au
sehemu ya hasara ambayo mtumishi ataisababishia serikali kutokana na
kukosea au uzembe wake; na Karipio.
Utaratibu wa namna ya Utekelezaji wenye ufanisi wa masuala yote yaliyokasimiwa ni kama ifuatavyo;-
i) Wakuu
wa Shule / Vyuo na Walimu Wakuu watatekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo na itakayokuwa
inatolewa.
ii) Mkuu wa Chuo, Shule au Mwalimu Mkuu atawajibika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu yaliyokasimiwa kwake.
iii) Masuala
yote yatakayoshughulikiwa katika mchakato ulioelezwa, ikiwa ni pamoja
na vielelezo na kumbukumbu zote za vikao zitatakiwa kutunzwa vizuri kwa
matumizi ya baadaye.
iv) Katibu
wa TSD Mkoa atakuwa na wajibu wa kushauri Wakuu wa Shule, Vyuo na
Walimu Wakuu juu ya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo
katika kutekeleza majukumu waliyokasimishwa.
v) Mawasiliano kati ya Mkuu wa Chuo/Shule, Mwalimu Mkuu na Mamlaka nyingine yatakuwa ni kwa njia ya maandishi.
vi) Iwapo
Mkuu wa Shule/Chuo au Mwalimu Mkuu atatenda kosa la kinidhamu (miongoni
mwa makosa madogo madogo) au hatatoa taarifa/atakataa kutoa taarifa au
ataficha baadhi ya taarifa, Katibu TSD Wilaya (Mamlaka yake ya Nidhamu)
ataweza kuchukua hatua kwa kuzingatia Kanuni 43 Sehemu B ya Jedwali la
kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003.
vii) Mafunzo/
Maelekezo kwa Wakuu wa Shule au Vyuo na Walimu Wakuu kwa kushirikiana
na Waajiri yatolewe na pia kuwepo na mafunzo ya mara kwa mara.
Matarajio ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa
kukasimu madaraka kwa Wakuu wa Shule, Wakuu wa Vyuo vya Ualimu / Vyuo
vya Maendeleo ya Jamii na Walimu Wakuu ni kwamba;- Mfumo huu utasaidia
kushughulikia masuala ya kiutumishi ya Walimu kwa haraka zaidi na kwa
ufanisi; Badala ya kila Mwalimu kuacha kufundisha darasani kwa lengo la
kufuatilia masuala yake ya kiutumishi Wilayani, sasa kutakuwa na
utaratibu wa Mkuu wa Shule/Chuo au Mwalimu Mkuu kuona kuwa ni wajibu
wake na kwamba atawajibika iwapo Walimu walio chini yake watakosa kupata
huduma za kiutumishi.
Taarifa
sahihi za Walimu zitapatikana kutokana na Tange itakayoandaliwa
katika ngazi ya Chuo/Shule. Kudhibiti udanganyifu wowote utakaofanywa na
Walimu kama vile vyeti vya kughushi, viwango vya elimu, vyeo
walivyonavyo. Kuhakikisha Walimu wanapata ajira rasmi na kusajiliwa
ndani ya miezi mitatu tangu kuajiriwa.
Kusimamia
vema zoezi la kuthibitishwa kazini na kupandishwa vyeo; Kuchukua hatua
mapema kwa wanaotenda makosa ya kinidhamu; Kuamsha ari ya kazi na
usimamizi wa maadili ya kazi ya ualimu kwa karibu zaidi.
Imetolewa na:
Edwin P. Mikongoti
Naibu Katibu
Tume ya Utumishi wa Umma
Idara ya Utumishi wa Walimu
01 Oktoba, 2013
0 comments:
Post a Comment