Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
UONGOZI
wa klabu ya Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wamewataka wanachama na
mashabiki wao kuendelea kujenga imani kubwa kwa kocha wao mkuu ambaye ni
mzawa, Alhaji Abdallah Athumani Seif ` King kibadeni Mputa` kwani anao
uwezo wa kuwafikisha mbali zaidi.
Mwenyekiti
wa klabu hiyo, Alhaji Ismail Aden Rage amesema kuwa mradi wa kuijenga
upya Simba unahitaji muda na imani kwa kocha Kibadeni kwani ndiye kocha
bora pekee hapa nchini kwa muda wote.
“Kiukweli
hakuna kocha yeyote, awe wa kigeni au nyumbani aliyewahi kuifikisha
timu yoyote fainali za kombe la washindi barani Afrika mnamo mwaka 1993
zaidi ya Kibadeni. Pia hakuna mchezaji yeyote aliyefunga mabao matatu
(Hat -Trick) mpaka leo katika mchezo wa watani wa jadi, zaidi ya
Kibadeni mnamo mwaka 1977 ambapo tuliwafunga Yanga 6-0. Kwahiyo Kibaden
ndiye kocha bora na anahitaji muda zaidi kwani anaweza sana”. Alisema
Rage.

Bosi: Mwenyekiti wa Simba Sc, Alhaji Ismail Aden Rage atakuwepo Mkwakwani Tanga kesho kuwaongoza vijana wake
Rage
ambaye ni mbunge wa Tabora mjini (CCM) alisema uongozi wa klabu hiyo
una imani kubwa na kocha wao, na kiwango ambacho Simba walikionesha
kataika mchezo wa jumapili dhidi ya Yanga na kuambulia sare ya 3-3
wakisawazisha mabao hayo kipindi cha pili inadhihirisha ubora wa
Kibadeni, hivyo wanachama lazima wamwamini zaidi.
Rage
ambaye kabla ya mchezo wa Yanga alitamba klabu yake ya Simba ingeifunga
Yanga 6-0, lakini mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika,
mnyama alikuwa nyuma kwa mabao 3-0, lakini walikuja juu na kusawazisha
yote kipindi cha pili.

Mkali wa rekodi Tanzania: Mfungaji wa mabao matatu pekee kwenye michezo ya watani wa jadi (Hat- Trick) , Abdallah Kibadeni
Pia
Rage alisema kuongoza Simba SC ni kazi kubwa kwani kuna watu wana
malengo ya kuendeleza timu na wengine ndani yake wana nia ya kuleta
mambo ya kuharibu timu, hivyo akasisitiza kuwa lazima wanachama,
viongozi na wachezaji waungane kwa pamoja.
Wakati
Rage akisema hayo, nayo Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho
(Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi tatu; ambapo Yanga itaikaribisha Rhino
Rangers katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Coastal
Union inaikaribisha Simba katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Tanzania
Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya
Ashanti United na Simba inarejea uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine
kwa kuikaribisha Kagera Sugar.
Nayo
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa
mechi moja ya kundi A itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment