Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
AZAM
FC imemtupa pembeni Mnyama Simba kukalia usukani wa ligi kuu soka
Tanzania bara baada ya jioni ya leo kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya
JKT Oljoro dimba la Sh. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha, huku shukurani
kubwa zikienda kwa Khamis Mcha `Vialli` aliyefunga bao hilo pekee dakika
ya 67.
Azam
fc wamefikisha pointi 20 wakiizidi Simba SC pointi 2 baada ya kushuka
dimbani mara 10, lakini wanawazidi wanamsimbazi mechi moja kwani wao
wamecheza mechi 9.
Afisa habari wa klabu hiyo, Jafar Idd Maganga ameuambia mtandao wa MATUKIO DUNIANI!
kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu sana ingawa waliingia kwa lengo la kupata
ushindi wa kihistoria kwa maana ya kubarizi kileleni kwa muda
wakisubiri matokeo ya mechi ya kesho.
“Tumekwea
kileleni kwa kufikisha pointi 20, tunarudi Dar es salaam kesho na
kuingia kambini moja kwa moja. Lengo letu ni kuendelea kukalia nafasi ya
juu. Pia kwa niaba ya uongozi wa Azam, nawashukuru sana wachezaji wetu
kwa kuwa wapiganaji wa kweli”. Alisema Jafar.

Huko
Mbeya katika uwanja wa Sokoine, wenyeji wa uwanja huo, klabu kali ya
Mbeya City imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wa jeshi la
kujenga taifa kutoka mkoani Pwani, JKT Ruvu.
Bao
la ushindi wa Mbeya City limefungwa na mshambuliaji hatari, Jeremiah
John dakika ya 36 na kuisaidia timu hiyo kupanda nafasi ya pili nyuma ya
Azam fc ikifikisha pointi 20 lakini wamezidiwa wastani wa magoli ya
kufunga na kufungwa.
Coastal Union licha ya kusajili majembe ya nguvu mambo bado magumu sana
Mechi
nyingine ilikuwa huko Manungu Complex mkoani Morogoro baina ya wenyeji
wa dimba hilo, Mtibwa sugar dhidi ya Mgambo JKT, na dakika tisini za
mchezo huo zimemalizika kwa wanajeshi hao kula kipigo cha mbwa mwizi cha
mabao 4-1 na kuendelea kushikilia rekodi ya kufungwa mabao mengi mpaka
sasa msimu huu.
Mabao
yametiwa kimiani na Shaaban Nditi dakika ya 17, Juma Luizio dakika ya
25 na 60 na Salum Mkopi dakika ya 61, wakati la Mgambo lilifungwa na
Malimi Busungu dakika ya 83.
Baada
ya mchezo huo, Meneja wa klabu ya Mtibwa, David Bugoya ameongea na
mtandao huu na kusema siku ya leo kikosi chao kimepiga soka safi zaidi.
“Ukiiangalia
Mtibwa kwa sasa, kiukweli inapendeza sana, soka lake ni la uhakika.
Tutaendelea kujipanga zaidi ingawa ligi yenyewe ngumu sana”. Alisema
Bugoyo.
Nao
Ashanti United `watoto wa jiji` ambao kwa siku za karibuni wameamka
kutoka usingizini, wamelazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Ruvu Shooting ya
mkoani Pwani.
Mabao
ya Ashanti yalifungwa na Tumba Swedi dakika ya nane kwa penalti na
Mussa Nampaka dakika ya 88, wakati ya Ruvu yote yalifungwa Elias Maguri
dakika za 24 na 49.
Afisa
habari wa Shooting, Masau Bwire ameumbia mtandao huu kuwa walianza
kufunga mabao mawili na baadaye wachezaji wao waliridhika na kujikuta
yanasawazisha.
“Kocha
Charles Mkwasa anaenda kuwaambia wachezaji wake waache tabia ya
kuridhika kabla ya dakika 90, kiukweli tulikuwa tunashinda huu mchezo,
lakini wameshindwa kuwa makini, lazima uzembe huu utupiwe macho na
makocha”. Alisema Masau.
Na
mechi ya mwisho ilikuwa huko Kaitaba mkaoni Kagera ambapo Wageni wa
uwanja huo Coastal Union ya Tanga wameendelea kukalia kiti cha moto
baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wana `Nkulukumbi` Kagera
Sugar. Bao pekee limefungwa na Salum Kanoni kwa penalti dakika ya 58.
0 comments:
Post a Comment