Vyama
vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vimesema vitaweka hadharani kesho
mambo yaliyojiri katika mazungumzo yao na Rais Jakaya Kikwete
yaliyofanyika Ikulu, Jumanne wiki hii.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo juzi walikutana na Rais Kikwete
kuzungumzia kasoro wanazolalamikia kuwamo kwenye Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013.
“Tumepanga kuzungumza na waandishi wa habari Ijumaa (kesho) kuelezea
mambo yaliyojiri katika mazungumzo yetu na Rais Kikwete,” alisema Naibu
Katibu Mkuu CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro.
Naye
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema
ushirikiano wa vyama wamekubaliana kuzungumza baada ya kukutana na
kutafakari yote yaliyojiri kwenye mazungumzo kwa upana na kuandaa
mapendekezo yanayohitajika.
Rais Kikwete juzi alikutana na viongozi wa vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Baadaye, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa kwa
vyombo vya habari ikisema pande mbili hizo zilikubaliana katika
mazungumzo hayo mambo makuu mawili.
La
kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya
kuboresha muswada huo, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta
namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
La
pili, vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa
Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano
na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato wa
mabadiliko ya katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali
wa taifa.
Taarifa hiyo ilieleza katika makubaliano hayo, Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja
na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi ulimalizika kwa pande mbili hizo kukubaliana mambo hayo.
Viongozi, ambao Rais Kikwete alikutana nao juzi kwa mazungumzo hayo
wanatoka vyama vya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment