YANGA wamekodi ndege tatu ndogo kupeleka kikosi chake katika Kisiwa cha Pemba kujiandaa na mechi dhidi ya Simba.
Pambano hilo la watani la jadi
ambalo litachezeshwa na mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa), Israel Nkongo litafanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam Jumapili ijayo.
Yanga, iliondoka jana Jumatatu
asubuhi ikiwa na wachezaji 28 kwenda kisiwani Pemba pamoja na viongozi
na benchi la ufundi lenye watu wanane.
Aliyeongoza kikosi hicho ni Mjumbe wa Sekretarieti ya Yanga, Patrick Naggi, ambaye ni raia wa Kenya.
Wakati Simba wakiwa bado kwenye
kambi yao ya siku zote Bamba Beach, Dar es Salaam, Yanga walitua Pemba
mchana na kuingia moja kwa moja kujifua kwenye Uwanja wa Gombani. Yanga
walianza kujifua saa sita mchana huku kukiwa na jua kali, kuhakikisha
kuwa wanakuwa fiti katika mchezo huo wa Jumapili.
Naggi, ambaye anaandaliwa kuwa
Katibu Mkuu Yanga aliliambia Mwanaspoti kuwa kuanzia leo Jumanne,
kikosi chake kitakuwa kinafanya mazoezi mara mbili kwa siku ili kujiweka
sawa kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa.
“Wachezaji wote tumekuja nao
kasoro Salum Telela, yupo kwenye matibabu maalumu, aliumia tukicheza na
Mbeya City, lakini wengine wote wapo vizuri tunachokifanya ni kuwajengea
uwezo wa uwanjani na kisaikolojia,” alisema Naggi.
Hata hivyo Mwanaspoti jana
Jumatatu jioni lilifuatilia habari za mchezaji huyo na kuarifiwa kwamba
naye amejiunga na wenzake katika msafara huo.
“Mechi ya Simba ni presha kubwa,
hawa ni watani wetu hakuna timu ambayo inapenda kufungwa, kila timu
inataka heshima na ujue kupata pointi tatu kwa Simba zinakuwa tamu zaidi
kuliko za timu yoyote, na inajenga heshima pia.”
Naye Ofisa Habari wa Yanga,
Baraka Kizuguto alipoulizwa kuhusu gharama ambazo Yanga wametumia kukodi
ndege hizo ndogo alisema: “Ndege zimeshughulikiwa na watu wengine
tofauti nje ya viongozi, hakuna yeyote kati yetu anayeweza kujua gharama
halisi zilizotumika.”
Hata hivyo, Mwanaspoti linajua kuwa Yanga imetumia Sh milioni tano kwa ajili ya gharama ya ndege hizo tatu.
Yanga ilipoifunga Simba mabao 2-0 katika mchezo wa kufunga msimu uliopita Mei 18, mwaka huu ilikuwa imetokea kuweka kambi Pemba.
Katika hatua nyingine, Naggi
alisema ratiba ya Ligi Kuu Bara inaumiza timu kwa vile mechi zimefuatana
kitu ambacho kinapoteza morali ya wachezaji.
“Tuna
mechi tarehe 20, halafu tunacheza tena tarehe 23 halafu 26 na tarehe 3
mwezi ujao, kwa kawaida mwili wa binadamu viungo vinakaa sawa baada ya
saa 72, lakini kwa ratiba hiyo kiafya si vizuri, “ alisema.
CHANZO: MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment