Mkuu
wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi toka Baraza la Ushindani (FTC) Bw.
Nzinyangwa Mchany akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya
namna wanavyoshughulikia rufani zinazofikishwa kwenye baraza
hilo,wakati wa mkutano uliofanyika uliofanyika Ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Sheria
Mwandamizi wa Baraza hilo Bi.Hafsa Said.
BARAZA LA USHINDANI (FAIR COMPETITION TRIBUNAL – FCT)
MADA
KUHUSU UMUHIMU WA BARAZA LA USHINDANI KWENYE MFUMO WA USHINDANI NA
UDHIBITI WA SOKO ILIYOWASILISHWA KWA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 23
OKTOBA 2013, KATIKA UKUMBI WA HABARI MAELEZO,
DAR ES SALAAM
Utangulizi
Ndugu
Waandishi wa Habari, mada yetu ya leo inahusu nafasi na umuhimu wa
Baraza la Ushindani kwenye mfumo wa ushindani na udhibiti wa soko hapa
nchini. Katika mada hii tunatarajia kuuelezea mfumo wa ushindani na
udhibiti wa soko ulivyoanza hapa nchini, ushindani ni nini, udhibiti
unaangalia nini na unazingatia nini, nafasi ya Baraza la Ushindani na
umuhimu wake. Hivyo, ili kuweza kuielezea vizuri mada yetu na
kuwawezesha kuandika vizuri, mada hii tumeipanga katika sehemu kuu tatu
kama ifuatavyo:
Mabadiliko ya kiuchumi ya mwaka 1986;
Kuanzishwa kwa Mfumo wa Udhibiti wa soko; na
Nafasi ya Baraza la Ushindani na umuhimu wake.
Mabadiliko ya kiuchumi ya mwaka 1986
Mwaka
1986, katika jitihada za kuboresha na kuimarisha uchumi, Serikali
iliamua kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa uchumi kutoka kwenye mfumo wa
uchumi hodhi (planned economy) na kufuata mfumo wa uchumi wa soko
(Market Economy). Uamuzi huu ulikuwa hususan kwa ajili ya kuleta kiwango
kizuri zaidi cha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu. Mfumo wa
uchumi wa soko unashirikisha kwa kiasi kikubwa sekta binafsi katika
kuzalisha na kusambaza huduma na bidhaa sokoni. Wawekezaji binafsi wa
ndani na nje ya mipaka ya nchi hukaribishwa na kuhimizwa kuwekeza kwenye
sekta za kiuchumi na kijamii. Wawekezaji wanakaribishwa pia kuwekeza
hata kwenye yale maeneo ambayo yalikuwa yanawekezwa na Serikali peke
yake. Aidha, Katika mfumo huu huduma na bidhaa sokoni hutolewa na kuuzwa
kwa ushindani. Katika mfumo huu wa soko, tofauti na ule wa uchumi
hodhi, maamuzi yote makubwa kuhusu uzalishaji na usambazaji wa huduma na
bidhaa sokoni hufanywa kwa kutegemea mwelekeo na nguvu ya soko.
Kuanzishwa kwa Mfumo wa Udhibiti wa soko
Sayansi
ya masuala ya uchumi kwenye nyanja ya ushindani na udhibiti wa soko
inafafanua kwamba; kimsingi ndani ya soko lolote kuna wadau wakuu watatu
ambao ni Serikali, Mwekezaji na Mlaji. Wadau hawa wana utashi na
maslahi tofauti. Serikali utashi wake mkubwa ni kuona kwamba (i)
panakuwepo na huduma na bidhaa bora kwa wingi, (ii) bidhaa salama, (iii)
bei nafuu, (iv) bidhaa za kuaminika na; (v) zinazoweza kuwafikia
wananchi ikiwezekana wote na pia ikiwezekana zitolewe bure. Aidha,
Serikali inataka mapato kwa njia ya kodi ili kujiendesha. Mwekezaji
lengo lake la kwanza ni (i) uzalishaji kwa gharama nafuu (ii) kupata
faida kubwa kwa haraka iwezekanavyo; na( iii) usalama na uhakika wa
mwelekeo wa kisera. Masilahi pamoja na utashi wa Mlaji hayapishani sana
na yale ya Serikali. Mlaji anataka (i) pawepo na huduma na bidhaa bora
kwa wingi, (ii) bei nafuu hata ikiwezekana bure (iii) usalama; na ( iv)
usiri (privacy).
Uzoefu
huo wa kisayansi unabainisha kuwa bila kuwa na wadhibiti huru katika
sekta zile ambazo ili uzalishe ni lazima uwekeze kwa kiwango kikubwa
(hususan za miundombinu, maji, mawasiliano, nishati) haitawezekana
kupata uzalishaji wa kuaminika na endelevu. Panatakiwa pawepo chombo
chenye nguvu na mamlaka ya kisheria kitakachokaa katikati ili kuweka
usawa wa masilahi ya hao wadau wakuu watatu kwenye soko. Katika kuweka
usawa wa masilahi hayo hapana budi kutenganisha bayana majukumu ya
kisera, ya kiudhibiti na ya kibiashara na pawepo na usahihi wa nafasi na
mgawanyo wa majukumu hayo bila ya kuwa na muingiliano.
Halikadhalika,
kuna sekta ambazo ili uzalishe si lazima uwekeze kwa kiwango kikubwa
sana kama zile za miundombinu. Katika sekta hizi ushindani ni mkali
sana, nazo zinatakiwa kuwa na muangalizi au msimamizi huru mwenye
mamlaka na nguvu ya kisera na kisheria. Msimamizi huyu atasimama kama
muamuzi (referee) huru wa ushindani sokoni ili soko lisiwe huria au
holela na kuleta migongano na mivutano ya kimasilahi. Soko likiachwa
bila muamuzi kamwe malengo ya kisera yaliyokusudiwa hayatafikiwa. Hivyo,
Serikali ikaamua kutenganisha majukumu ya kisera, kiudhibiti na
kibiashara ili kuleta ufanisi katika utendaji wa soko.
Hali
ya soko kuwa huria na holela ilianza kujitokeza hapa nchini katikati ya
miaka ya themanini (1980) mwanzoni mwa kipindi cha mara baada ya
mabadiliko ya uchumi. Lakini Serikali iliazimia kuweka mfumo thabiti wa
usimamizi wa ushindani sokoni pamoja na udhibiti kwenye sekta za
miundombinu, huduma za maji, nishati na mawasiliano. Hivyo kuanzia
mwaka 1994 na kuendelea Serikali ilifanya mabadiliko makubwa ya
kiudhibiti (regulatory reforms) na kuanzisha mamlaka mbalimbali za
udhibiti. Kwa kutumia Sheria zilizopitishwa na Bunge, Serikali
ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(SUMATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA), na
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA). Aidha
mwaka 2003, Bunge lilipitisha Sheria ya Ushindani. Serikali kupitia
Sheria hii ya Ushindani Na 8/2003 iliunda vyombo vitatu muhimu ambavyo
ni (i) Tume ya Ushindani (FCC), (ii) Baraza la Ushindani (FCT) na (iii)
Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji (NCAC).
Madhumuni
hasa ya uanzishaji wa vyombo hivi vyote ni kusimamia biashara ili
zisifanyike kiholela, kuhakikisha panakuwa na ufanisi katika ugawaji na
utumiaji wa rasilimali zilizopo na kuongeza kiwango cha uwekezaji,
kukuza ubunifu (inovation), kuongeza tekinolojia, kuhakikisha ustawi wa
mlaji na pia kuona kwamba soko na uchumi kwa ujumla vinakuwa na ufanisi.
Madhumuni haya ndio yanayotoa maana halisi ya udhibiti wa uchumi wa
soko.
Nafasi ya Baraza la Ushindani na umuhimu wake
Majukumu
ya Mamlaka za udhibiti yanatofautiana kulingana na aina ya sekta,
lakini kimsingi mamlaka hizo zinaangalia viwango vya mashariti ya
uwekezaji, gharama za huduma, viwango vya bei za bidhaa na huduma,
viwango vya ubora, usalama, mwenendo wa wawekezaji kulingana na masharti
ya leseni pamoja na kutoa au kufuta leseni husika n.k. Tume ya
Ushindani (FCC) inasimamia ushindani sokoni na jukumu lake kuu ni
kuangalia uzingatiaji wa Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na Sheria ya
Alama ya mwaka 1963 (Mechandise Marks Act of 1963) kuhusiana na
uingizaji wa bidhaa bandia sokoni. Kimsingi ushindani unaohusika hapa
unaeleweka kama ni ule mchakato ambao wazalishaji au wasambazaji wa
bidhaa na huduma mbalimbali wanaufuata kwa kufanya jitihada, kwa uhuru
na kwa masilahi yao kuwavutia wateja ili kutimiza malengo yao ya
kiuchumi kwa mfano kupata mauzo, faida na sehemu ya soko (market share)
la hiyo bidhaa au huduma husika. Sera ya Serikali kuhusiana na
ushindani ni kuwa na ushindani wa dhati na wa haki na kuchukua hatua
zinazorekebisha tabia potofu ya vyombo vya kibiashara sokoni.
Mfumo
wa udhibiti ulioanzishwa unazingatia misingi ambayo ni uhuru na
majukumu yasiyo na muingiliano, uwazi, uwajibikaji (accountability),
kuaminika (predictability), na ushirikishaji wa wadau. Uwajibikaji
unamaanisha kwamba, pamoja na Mamlaka ya udhibiti kuwa huru hainabudi
kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia misingi ya udhibiti. Ufanisi wa
udhibiti wa sekta au ushindani kwenye soko unapatikana pamoja na mambo
mengine, kwa kuhakikisha kwamba maamuzi au amri za mdhibiti zinapokosa
utoshelevu, umakini au kutofuata sheria kwa makini zinaweza kupingwa
mbele ya mahakama maalumu iliyo huru kwa njia ya rufaa.
Hivyo,
Serikali ilianzisha Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal)
ikiwa ni mahakama maalumu ya rufaa za maamuzi au amri za Tume ya
Ushindani na mamlaka za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi
ya mawasiliano zilizotajwa kwenye aya zilizotangulia. Kwa hiyo Baraza
la Ushindani ni ngazi ya juu na ya mwisho katika mfumo wa ushindani na
udhibiti na umuhimu wake ni:
Kuwa
ngazi thabiti ya rufaa inayosikiliza kesi kwa haraka na ufanisi
katika mfumo wa ushindani na udhibiti ili uzalishaji na usambazaji wa
huduma na bidhaa sokoni usicheleweshwe na milolongo mirefu ya kesi
katika mahakama za kawaida;
Kuwa
mahakama maalum (specialized) ambayo itajikita na kuelekeza rasilimali,
jitihada na nguvu zake zote katika kusikiliza na kuamua kesi za rufaa
za ushinani na udhibiti tu kwa namna ya kipekee inayopunguza baadhi ya
taratibu za kimahakama;
Kuharakisha mchakato wa usikilizaji wa rufaa za ushindani na udhibiti wa soko kwa kufuata taratibu na ujuzi maalum;
Kuwa
nyenzo ya mwisho ya kurekebisha au kuthibitisha maamuzi na amri za Tume
ya Ushindani na mamlaka za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na
matumizi ya mawasiliano zilizotajwa kwenye hii mada;
Baraza
ni alama ya uhakika (provide assurance) wa ulinzi na uteteaji wa
ushindani unaozingatia haki na kumlinda mlaji pamoja na mlalamikaji
mmoja mmoja.
Hivi
sasa Baraza limekamilisha maandalizi ya kusikiliza kesi kumi na moja
(11) kati ya kumi na sita (16) zilizokamilisha taratibu za usajili. Kesi
hizo zinatarajiwa kusikilizwa kwa wiki mbili mfululizo kuanzia tarehe
28 Oktoba 2013, mbele ya Mhe: Jaji Raziabegum Sheikh (Mwenyekiti)
na Jopo la Wajumbe wa Baraza Dkt. Malima M.P Bundara, Bw. Gregory
Ndanu, Bw Onesmo Kyauke, Bibi Nakazaeli Tenga, Prof. A.F. Mkenda na Bi
Salma Maghimbi. Kesi hizo zitakaposikilizwa na kutolewa
maamuzi zitachangia katika kurudisha ufanisi wa utendaji wa sekta husika
ambao ulikuwa umekwamishwa na vipengele vilivyopingwa mbele ya Baraza,
na hivyo kuwezesha sekta hizo kuendelea kutoa mchango wake wa maendeleo
ya kiuchumi na kijamii. Kwa hiyo Baraza linawasihi wadau wake wote,
wafanyabiashara na walaji kwamba waikumbuke hiyo nafasi ya Baraza katika
mfumo wa ushindani na udhibiti wa soko, watambue umbuhimu wake na
wasisite kulitumia pindi wanapohitaji kutatua migogoro yao katika soko
kwa ujumla na kwenye sekta zilizotajwa.
Nzinyangwa E. Mchany
MKUU WA KITENGO CHA MASUALA YA UCHUMI
Simu 0754 720007
0 comments:
Post a Comment