Na Baraka Mpenja , Mbeya
HATIMAYE
pambano lililosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa kandanda nchini baina
ya Makamu bingwa Azam fc, `wana lambalamba` dhidi ya mabingwa watetezi
wa ligu kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga ya Dar es salaam
limemalizika kwa wanajangwani kula ngumi za uso baada ya kukubali
kichapo cha risasi 3-2 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Azam
walioingia uwanjani wakitokea katika matokeo ya sare ya 1-1 na Ashanti
United ndio walikuwa wa kwanza kutinga katika nyavu za Yanga katika
dakika ya 1 ya mchezo huo kupitia kwa John Bocco `Adebayor`.
Yanga
waliokuwa na machungu ya kukabwa koo na timu mbili za Mbeya, Mbeya City
na Prisons baada ya kutoka nazo sare uwanja wa sokoine walisawazisha
bao hilo katika dakika ya 50 Kupitia kwa Didier Kavumbagu `Kavu` na
ndipo mchezo ukawa wa vuta ni kuvute na kushuhudia timu zote zikicheza
kwa kiwango cha juu.
Yanga
walikosa nafasi kadhaa za kufunga kutokana na washambuliaji wake kukosa
umakini, hali kadhalika wenjeji wa kipute cha leo, Azam fc.
Yanga
waliandika bao la pili kupitia kwa Mganda aliyekuwa Lebanon kufanya
Majaribio na sasa amerejea Jangwani, Hamis Kiiza, `Diego` katika dakika
ya 66 baada ya kumalizikia kazi nzuri ya Simon Msuva.
Azam
wenye makazi yao Mbande Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam
walisawazisha bao hilo kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya beki ya
Yanga kuunawa mpira eneo la hatari kutoka na mshambuliaji raia wa Ivory
Coast , Kipre Herman Tchetche kukwamisha gozi kimiani.
Baada
ya mwamuzi kuonesha dakika mbili za nyongeza, vijana wa Ernie Brandts
walihamishia makazi katika lango la Azam wakitafuta bao la ushindi,
lakini walifanyiwa hujuma na vijana wa Sterwart John Hall ambao
walifanya shambulizi kali na kuandika bao la tatu na la ushindi kupitia
kwa mshambuliaji wa Joseph Kimwaga aliyeingia kuchukua nafasi ya Farid
Mussa na kuachia shuti kali nje ya 18 na kumwacha kipa wa Yanga Ally
Mustapha `Bartez`.
Matokeo
ya leo yametonesha kidonda kwa wanajangwani baada ya kuonja uchungu wa
kipigo kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi kuu msimu wa 2013/2014,
wakati huo huo wakikabiliwa na wimbi wa sare tatu kabla.
Kocha
wa Yanga, Ernie Brandts amebaki mdomo wazi kwani awali alitamba kuibuka
na ushindi mbele ya matajiri wa Azam kutokana na kurejea Dar es salaam
katika dimba bora lenye kapeti la ukweli.
Brandts
alisema amechoshwa na Uwanja wa sokoine ambao alisema sio bora kabisa
na baada ya kurudi Dar, kikosi chake kitacheza mpira wake.
Hata
hivyo lazima ukweli usemwe, Yanga wamecheza vizuri sana na wameonesha
kuwa imara, lakini hesabu zao zimekuwa mbovu hasa dakika za lala salama
kwani walikuwa wanashambulia na kupanda bila kuweke tahadhari langoni
mwao.
Timu
zote zilikuwa zinashambuliana kwa zamu, lakini Azam walikuwa na bahati
zaidi kwani hata bao lao la kwanza lilifungwa mapema na kuashiria kuwa
siku njema huanza asubuhi.
Kwa
upande wa Azam, muda mfupi kabla ya mechi walikuwa na kikao na viongozi
wao pamoja na benchi la ufundi, ambao wachezaji walikiri kuvurunda na
kuahidi ushindi katika mchezo wa leo, na hatimaye wamekalimisha ahadi
yao na bila shaka Azam Cola zitapanda kwa uzuri leo.
Katika
mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu
Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani
Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Jerry
Tegete/Hamisi Kiiza dk58 na Haruna Niyonzima.
Azam
FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins
Atudo/Said Mourad dk56, Himid Mao, Farid Mussa/Joseph Kimwaga dk72,
Kipre Balou, John Bocco, Humphrey Mieno na Brian Umony/Kipre Tchetche
dk52.
Mchezo
mwingine wa mzunguko wa tano wa ligi kuu umepigwa huko CCM Mkwakwani
jijini Tanga na kushuhudia wenyeji wa Uwanja huo, Coastal Union `Wagosi
wa Kaya` wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting Stars.
Bao pekee katika ushindi hauo limefungwa na kiungo mwenye uwezo mkubwa
wa kucheza soka aliyesajiliwa kutoka Simba Sc, Haruna Moshi `Boban`
dakika za lala kwa buriani yaani dakika ya 82.
Kipute
kingine kilikuwa huko Azam Complex ambapo wenyeji wa uwanja huo, JKT
Ruvu wamelala kwa bao 1-0 kutoka kwa JKT Oljoro na kuendelea kuonesha
kuwa ushindi wa mechi tatu za mwanzo ilikuwa nguvu za soda.
PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY
0 comments:
Post a Comment