Na Baraka Mpenja , Mbeya
HAKIKA
mkubwa ni mkubwa tu!, mpaka sasa mashabiki wa soka jijini Mbeya
wameshashuhudia mechi mbili za ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu wa
2013/2014 ambapo mechi ya kwanza iliwakutanisha Mbeya City dhidi ya
Kagera Sugar, huku ya pili wakicheza na Ruvu Shooting, lakini ujio wa
Mabingwa watetezi, klabu ya Yanga ya Dar es salaam umebadili hali ya
hewa jijini hapa.
Kila
kona ya jiji la Mbeya, gumzo zito limetawala kwa mashabiki wa kandanda
kuzungumzia mtanange huo wa kukata na shoka utakaopigwa siku ya jumamosi
Septemba 14 baina ya Wenyeji Mbeya City na Yanga huku ikiwa mara ya
kwanza kwa wakali hao wa Mbeya kukutana na presha ya timu kubwa na
kongwe katika soka la Tanzania.
Pambano
hilo limevuta hisia za mashabiki wengi ukizingatia Yanga ni klabu kubwa
yenye mashabiki kila kona ya Tanzania, hivyo mechi zake zinakuwa na
msisimko mkubwa kama ilivyo kwa wekundu wa Msimbazi Simba ambao siku
hiyo watakuwa na kibarua kizito mbele ya Mtibwa Sugar, uwanja wa Taifa
jiijini Dar es salaam.
Mtandao
huu umefanikiwa kutembelea mazoezi ya klabu ya Mbeya City yanayoendelea
katika dimba la Sokoine jijini hapa na kujionea mikakati mizito ya
benchi la ufundi kuhakikisha wanashinda mechi hiyo iliyopandisha homa ya
wapenda soka kila kona ya mji.
Akizungumza
katika mazoezi hayo, kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi amesema
vijana wake wanaendela vizuri na wapo katika morali kubwa ya kuwakabili
wanajangwani waliosheheni nyota wengi wakiwemo, Jerryson Tegete, Haruna
Niyonzima “Fabregas”, Didier `Kavu` Kavumbagu, Mbuyu Twite, Frank
Domayo, Nadir Haroub `Canavaro` , n.k.
“Sisi
tunajiandaa na mechi ijayo bila kujali ni Yanga, tukisema tunajiandaa
na Yanga tunaonesha kuwa klabu hiyo ni tofauti na timu nyingine.
Tunawaheshimu sana, ni timu kubwa, kongwe na yenye uzoefu mkubwa, lakini
sisi tumejiandaa kucheza na timu zote 13 za ligi kuu msimu huu wa
ligi”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi
amewataka mashabiki wa Mbeya City kuamini kuwa wanaweza kushinda mechi
hiyo bila kujali ubora wa Yanga, hivyo lazima wajitokeze kwa wingi
kuishangilia timu yao inayovuta hisia za mashabiki wengi jijini Mbeya.
Mbeya
City ni klabu ya wananchi na ina mashabiki lukuki, sasa sijui jumamosi
itakuwaje uwanjani, kwani mwaka jana Yanga ilikuwa na mashabiki wengi
zaidi ya Prisons zilipokutana uwanja wa Sokoine.
Wakati
hayo yakijiri, naye meneja wa uwanja wa sokoine, Modestus Mbande
Mwaluka anaendelea kuufanyia ukarabati uwanja wake kwa kumwagilia maji,
kuweka uzio wa nguvu ili kujihami na hali ya mashabiki kuingia uwanjani
kinyume na taratibu zilizowekwa.
0 comments:
Post a Comment