Hatimaye
vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la
Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo
kuvamiwa na wanamgambo.
Milipuko
ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo
asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea
kukamilisha operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.
Serikali
imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa
katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara
ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la
Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna
mateka aliyesalia
Wakati
huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo
watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke
muingereza.
Kwenye
mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina
Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19
ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota.
Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana
alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.
Haijulikani
idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo , lakini maafisa wa
usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.
Kundi
la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza
kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.
“magaidi
hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo
hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,”
alisema Ole Lenku
Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu
jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate
ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo
hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka
kukomboa jengo hilo.
CHANZO: BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment