HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
Jumla
ya Askari mia moja (100) waliofuzu usaili wa awali wa ajira ya uaskari
wanatarajiwa kuanza rasmi mafunzo maalum ya mbinu za medani kwa miezi
mitatu katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu.
Askari
watakaofuzu vema mafunzo hayo ndio watakaoajiriwa na shirika katika
utaratibu mpya ulioanzishwa na shirika wa kuandaa mafunzo hayo kwa
askari hawa waliopitia mafunzo ya uaskari katika Jeshi la Kujenga Taifa
na Chuo cha Wanyamapori Pasiansi Mwanza.
Aidha,
shirika linaendelea kuchunguza na kuchukua hatua za kinidhamu na
kisheria kwa wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na vitendo vya
ujangili kwa kushirikisha vyombo vya dola. Uchunguzi bado unaendelea
kufanyika kwa baadhi ya wafanyakazi na utakapopatikana ushahidi wa
kisheria kwa wote wanaojihusisha na mitandao ya ujangili hatua kali za
kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.
Mafanikio
kadhaa yameweza kufikiwa na shirika katika kukabili ujangili ambapo
uimarishwaji wa doria za magari na miguu pamoja na matumizi ya mbwa
katika hifadhi nchini umepunguza kwa kiwango kikubwa vitendo hivi ambapo
katika kipindi cha miezi sita iliyopita ujangili uliokuwa umeshika kasi
katika Hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara uliweza kudhibitiwa kwa
asilimia 100 ambapo hakuna tembo aliyeuawa ndani ya hifadhi hizo tangu
mwezi Februari hadi leo.
Vile
vile, Shirika limeanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujangili na
matukio ya dharura (Rapid Response Team). Kikundi hiki kina Askari 40
ambao wamepewa mafunzo maalumu ya ujasiri na ukakamavu wa hali ya juu
kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ujangili katika kipindi cha
miezi sita iliyopita ambapo mafunzo hayo yalifanyika katika Hifadhi ya
Ruaha.
Mafanikio mengine yaliyoweza kufikiwa na shirika katika muda wa miezi sita iliyopita ni pamoja na
i. Ukamataji
wa majangili 1,116 katika hifadhi kwa kipindi cha Aprili –Juni 2013.
Hifadhi ya Serengeti pekee iliweza kukamata majangili 248.
ii. Katika
kipindi cha Aprili-Juni 2013, Askari wetu waliweza kukamata silaha za
moto 85 toka kwa majangili. Silaha hizo ni pamoja na Civilian Rifle (7),
muzzle loaders/magobore 60 Automatic Rifle (5) na shortgun 13. Aidha,
silaha za kienyeji zipatazo 795 zilikamatwa na pia kufungua waya
zinazotumika kutega wanyama 25,422.
iii. Askari wa hifadhi waliweza kukamata mbao 2,245 na nguzo 1030 kwa kipindi hicho katika hifadhi zake.
iv. Askari
waliweza pia kukamata mifugo (ng’ombe) 6,650 waliokuwa wakichungwa
ndani ya hifadhi bila vibali. Wenye mifugo hiyo walitozwa faini stahili.
Kwa
ujumla hali ya ujangili ndani ya maeneo ya hifadhi imedhibitiwa kwa
kiwango kikubwa ambapo kama tulivyosema awali shirika litaendelea
kuchukua hatua za kinidhamu mara moja pale itakapobainika kuhusika kwa
watumishi wake katika vitendo hivi kama ambavyo limeshachukua hatua za
kufukuza kazi na kuandika barua za onyo kali kwa baadhi ya maafisa
wake..
Mwisho,
katika siku za usoni shirika linatarajia kubadili mfumo wake wa
utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa mfumo wa kamili wa kijeshi
(paramilitary system) kwa watumishi wote ili kuweza kukabili kwa umakini
janga la ujangili nchini.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
22.09.2013
0 comments:
Post a Comment