Na Boniface Wambura, TFF
Rhino
Rangers na Ashanti United zinapambana katika mechi pekee ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) itakayochezwa kesho (Septemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Wakati
Rhino Rangers ilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita
jijini Tanga dhidi ya Mgambo Shooting Stars, Ashanti United inashuka
uwanjani huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutandikwa mabao 3-0 na
Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
TWIGA STARS YAPANGIWA ZAMBIA AWC
Timu
ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imepangiwa kucheza
na Zambia katika mechi za kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika
kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia.
Twiga
Stars itaanzia ugenini jijini Lusaka ambapo mechi ya kwanza itachezwa
kati ya Februari 13 na 15 mwakani wakati ile ya marudiano itafanyika
kati ya Februari 28 na Machi 2 mwakani jijini Dar es Salaam.
Iwapo
Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia, raundi ya pili ambayo ndiyo ya
mwisho itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe. Mechi ya kwanza
itakuwa Dar es Salaam kati ya Mei 23 na 25 mwakani wakati ile ya
marudiano itakuwa kati ya Juni 6 na 8 mwakani.
Nchi
25 zimeingia katika mashindano huku mabingwa watetezi Equatorial
Guinea, makamu bingwa Afrika Kusini na Cameroon iliyoshika nafasi ya
tatu katika fainali zilizopita zikiingia moja kwa moja katika raundi ya
pili.
Wakati huo huo MABINGWA ARS KUPONGEZWA DAR
Timu
ya mpira wa miguu ya wasichana ya Airtel Raising Stars (ARS) ya
Tanzania imeandaliwa hafla ya kuipongeza kwa kunyakua ubingwa katika
mashindano ya Afrika yaliyofanyika nchini Nigeria.
Hafla
hiyo ya kuipongeza pamoja na kupata chakula cha mchana itafanyika leo
(Septemba 24 mwaka huu) saa 6 mchana kwenye hoteli ya Kilimanjaro
Kempinski na kuongozwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Timu
hiyo iliyorejea nchini jana (Septemba 23 mwaka huu) usiku katika mchezo
wa fainali ya mashindano hayo iliifunga Kenya. Kwa upande wa wavulana,
timu hiyo ilitolewa na Zambia katika hatua ya nusu fainali.
Michuano
hiyo ilishirikisha timu kutoka nchi za Burkina Faso, Chad, Congo
Brazzaville, Gabon, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Kenya,
Madagascar, Malawi, Niger, Nigeria, Tanzania, Uganda na Zambia.
Kombaini
ya timu hizo zilizokuwa chini ya makocha Rogasian Kaijage na Abel
Mtweve iliundwa baada ya mashindano ya Airtel Raising Stars
yaliyohusisha wasichana na wavulana wenye umri wa chini ya miaka 17 na
kufanyika jijini Dar es Salaam wiki ya kwanza ya Septemba mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment