SERIKALI
imetengua tamko lilitolewa Machi 19, mwaka huu na Waziri wa Maliasili
na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki la kupunguza ukubwa wa pori tengefu
la Loliondo kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi kilometa za mraba 1,500.
Uamuzi huo umetangazwa juzi jioni (Jumatatu, Septemba 23, 2013) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati
akizungumza na wakazi wa kata nane za Tarafa ya Loliondo katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenya uwanja wa michezo wa Wasso, wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha.
Waziri
Mkuu alisema Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kufanya vikao pamoja
na mawaziri aliombatana nao na kukubaliana kuwa wakazi hao waendelee
kuishi kama ilivyokuwa awali kabla tamko halijatolewa na Balozi
Kagasheki.
“Nilikuja
wilayani Ngorongoro ili nijionee hali halisi ya vijiji vinavyodaiwa
kuondolewa. Nilitaka nione kuna miundombinu ya aina gani katika eneo
husika na hasa huduma za jamii. Nimeona hali ya malisho, umbali uliopo
kutoka vijijini hadi eneo tajwa, miundombinu iliyopo, niliuliza idadi ya
kaya zilizopo… kuna kijiji nimeambiwa kina watu zaidi ya 9,000… kwa
kweli nimeamini tembea uone!”
“Tumefikia
uamuzi kwamba wakazi wa kata hizi zote, muendelee na utaratibu wenu wa
awali wa namna ya kuendeleza eneo la Loliondo kana kwamba hilo tamko
halipo,” alisema Waziri Mkuu na kuamsha makelele ya shangwe miongoni mwa
wakazi wa Loliondo ambao wengi wao ni Wamasai.
Aliwataka
waendelee na kamati za mahusiano ya kijamii zilizokuwepo baina ya
vijiji na wawekezaji ziimarishwe. Pia alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha
aweke utaratibu wa kuitisha vikao kila baada ya miezi mitatu ili wadau
wote wakae na kukosoana kila inapobidi.
Mara
baada ya kuwasili Loliondo Jumapili asubuhi (Septemba 22, 2013)
akitokea Arusha, Waziri Mkuu aliamua kutembelea vijiji vyote ambavyo
viko kwenye ushoroba (corridor) wa kilometa za mraba 1,500 kando ya
hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na Pori tengefu la Loliondo ambavyo
wakazi wake walitakiwa kuhamishwa ili kulinda mazalia ya wanyamapori,
kutunza mapito ya wanyama na vyanzo vya maji.
Vijiji
hivyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Kertaloo, Oloipir, Olorian Maiduguri,
Losoito Maaloni na Arash. Alibakiza kijiji kimoja tu cha Piyaya kwa
sababu kiko umbali wa km. 50 kutoka Arash na jua lilikuwa
limekwishazama.
Waziri
Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo
ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za
Ngorongoro, Loliondo na Sale kabla ya kuhutubia mkutano huo aliamua
kukutana na wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia
zilizopo Loliondo pamoja na wazee wa kimila (Malaigwanan) na kusikiliza
maoni yao kuhusu suala hilo.
Mbali
ya kero hiyo ya wakazi kuhamishwa ili kupisha ushoroba, kero nyingine
ambazo Waziri Mkuu alizipokea zilihusu ukosefu wa maji, ajira wa vijana
na ukosefu wa barabara ya kudumu. Ili kutatua suala la barabara, Waziri
Mkuu leo anaondoka Loliondo kwa njia ya barabara kupitia mto wa Mbu hadi
Arusha ili ajionee hali ya barabara hiyo ambayo ni miongoni mwa ahadi
za Rais Jakaya Kikwete.
Mawaziri
aliokutana na kufanya kikao nao jana asubuhi ni Bw. William Lukuvi (OWM
– Sera Uratibu na Bunge), Prof. Anna Tibaijuka (Ardhi na Maendeleo ya
Makazi), Bw. Jumanne Majaliwa (Naibu Waziri TAMISEMI – Elimu), Bw.
Lazaro Nyalandu (Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), Dk. Binilith
Mahenge (Naibu Waziri wa Maji), Bw. Benedict Ole Nangolo (Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi) na wabunge wa CCM ambao ni wajumbe wa Kamati ya
Mwigulu. Nao ni Bw. Christopher Ole Sendeka, Bw. Lekule Laizer na Mary
Chatanda. Wengine ni wataalamu wa wilaya ya Ngorongoro na kutoka
Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 25, 2013.
0 comments:
Post a Comment