WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itahakikisha kuwa ardhi ambayo
Watanzania wamepewa na Mungu haibadiliki na kuwa chanzo cha upotevu wa
amani nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Septemba 10, 2013) wakati akifungua
mkutano wa kimataifa wa siku tatu unaojadili haki na amani katika
masuala ya ardhi Tanzania ulianza jana jijini Dar es Salaam.
“Tutafanya
kila tuwezalo kuhakikisha kuwa ardhi yetu haileti laana bali inabakia
kuwa baraka ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia. Ninawasihi wale wote wenye
mamlaka na utoaji wa ardhi wahakikishe kuwa wanatimiza wajibu wao
wanaposimamia masuala ya ardhi ili haki isipotee na hatimaye kuepusha
migogoro ya ardhi,” alisema.
“Ninawasihi
Watanzania iwe ni wanasiasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, wasomi
na umma wote kwa ujumla. Ninaomba tuitunze amani tuliyonayo na tutambue
kwamba Tanzania ndiyo nchi pekee tuliyojaliwa kuwa nayo. Madhara ya
ukosefu wa amani ni makubwa. Tuangalie nchi za wenzetu zenye migogoro
na tuone jinsi machafuko hayo yatatuathiri sisi wenyewe, watoto wetu na
wajukuu wetu,” alisisitiza.
Alisema
anatambua hofu ambayo imewakumba watu wengi kuhusiana na uwekezaji iwe
ni kwenye kilimo ama madini. “Ninatambua kwamba kuna hofu kubwa
imejengeka miongoni mwa wananchi wengi hasa wanaposikia suala la
uwekezaji hasa kwenye kilimo,” alisema.
Alisema
tangu wakati Mwalimu Nyerere akiwa madarakani, alishasema kuwa ardhi ni
rasilmali ya watu wote. “Aliweka mifumo ambayo hairuhusu mtu kumiliki
ardhi ambayo haina ukomo, kuna ukomo wa miaka kati ya 33 na 99. Na pia
kuliwekwa masharti kuwa ni lazima ukipata ardhi uiendeleze,
usipoiendeleza, unanyang’anywa,” aliongeza.
Alisema
kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999, imekataza mgeni (Mtanzania
ambaye si mzawa) kumiliki ardhi hapa nchini. “Ardhi inatolewa kwa
wawekezaji, chini ya sheria ya uwekezaji kwa muda maalum. Mwekezaji
akimaliza muda wake, anatuachia ardhi yetu, na ndiyo maana Serikali ya
Kijiji hairuhusiwi kutoa ardhi zaidi ya ekari 50,” alisema.
Alisema
chini ya sheria ya ardhi na sheria ya uwekezaji, hapa nchini kuna
wawekezaji wakubwa 122 ambao ni wa ndani na wa nje na kwa ujumla wao
wanamiliki kilometa za mraba 1,296 kati ya kilometa za mraba 945,087
ambazo ni ukubwa wa nchi nzima.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na wajumbe 200 wakiwemo Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof.
Anna Tibaijuka, wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi wa dini, washiriki kutoka
nchi za Ujerumani, Sweden, Burma, Finland, Norway na Afrika Kusini.
0 comments:
Post a Comment