Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu kukamilika kwa awamu ya
kwanza ya Operesheni ‘Kimbunga’ ya kuwaondoa wahamiaji haramu. Kulia ni
Kaimu Kamishina wa Uraia na Pasipoti wa Uhamiaji, Victoria Lembeli.
Picha na Emmanuel Herman
………..
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania kuchukua
hadhari dhidi ya raia wa kigeni wakati huu ambao amani ya dunia ipo
shakani.
Tamko hilo limekuja wakati kundi
la kigaidi la Al-Shabaab limevamia jengo kubwa la biashara la Westgate
huko Nairobi, Kenya na kuua zaidi ya watu 60 huku mamia wakijeruhiwa na
wengine kadhaa kuendelea kushikiliwa mateka tangu Jumamosi iliyopita.
Hata hivyo, Dk Nchimbi hakugusia
tukio hilo kwenye maelezo yake lakini aliwataka Watanzania waache tabia
ya kuwapa hifadhi raia wa kigeni akisema ni hatari kwa usalama wa
taifa… “Watanzania lazima tuwe makini hasa nyakati hizi ambazo usalama
wa dunia upo shakani.”
Alisema Serikali kwa upande
wake, imekuwa ikijitahidi kuweka nchi katika hali ya usalama ikiwa ni
pamoja na kuendesha operesheni za kuwasaka wahamiaji haramu.
“Hakuna uhalali wa mtu kukaa
katika nchi nyingine bila kufuata taratibu za sheria,” alisema na
kuongeza: “Ni lazima vyombo vya usalama kujua nani kaingia na nani
anaondoka.”
Alisema operesheni inayoendelea
ya kuwabaini na kuwachukulia hatua wahamiaji haramu inayojulikana kwa
jina la Kimbunga, waziri huyo alisema imebainika kuwa baadhi ya
Watanzania wanawahifadhi raia wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Alitoa mfano wa raia wa
Uingereza ambaye alikuwa akitafutwa na nchi yake kutokana na vitendo vya
kigaidi lakini akakamatwa akiwa amehifadhiwa na Mtanzania ambaye
alikwishamfanyia mipango ya kupata vitambulisho kama kile cha mpiga
kura.
Alisema mkakati wa kuwaondoa
raia wa kigeni ulianza Julai 26, mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alipotoa
kipindi cha wiki mbili watu wanaoishi nchini kinyume cha taratibu
kuondoka kwa hiari yao.
“Katika agizo hilo la Mheshimiwa Rais (Jakaya) Kikwete, raia wa kigeni 21,758 waliondoka na kurejea makwao kwa hiari,” alisema.
Dk Nchimbi alisema operesheni ya
kuwaondoa wale ambao hawakutii amri ya Rais Kikwete ilianza Septemba 6,
mwaka huu na hadi ilipomalizika wiki hii, watu 12,604 walikuwa wametiwa
mbaroni.
“Kati ya hao Wanyarwanda ni
3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589, Wasomali 44, Myemeni
mmoja na Mhindi mmoja,” alisema Dk Nchimbi.
Kwenye
operesheni hiyo alisema pia waliwakamata watuhumiwa 212 wa unyang’anyi
pamoja na silaha mbalimbali zipatazo 61, baadhi zikiwa za kivita.
Alisema awamu ya pili ya
operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu ipo mbioni ingawa alisema
safari hii, idadi ya watakaounda timu ya uendeshaji wake itapungua.
Waziri
huyo alisema kuwa wale wote wanaoishi nchini wanaweza kuamua kuondoka,
kufanya mkakati wa kuomba uraia au kuwa na hati ya kusafiria pamoja na
kibali cha kuwaruhusu kuishi nchini.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment