WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema angependa kuona mkoa wa Tabora unakuwa mkoa wa mfano katika kushirikisha vijana kwenye kazi za uzalishaji mali.
“Ninafurahi kwa sababu mmeanza, mmethubutu, mmeweza na sasa tunasubiri matokeo. Changamoto ni nyingi, maneno ni mengi, lakini cha msingi ni jamii mnayoihudumia inasemaje,” aliongeza.
Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 31, 2013) wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa wilaya ya Igunga, mkoani Tabora mara baada ya kupokea taarifa ya wilaya hiyo katika kijiji cha Simbo akiwa katika ziara fupi ya kukagua miradi ya uzalishaji inayofanywa na vijana mkoani humo.
“Mnalolifanya leo siyo geni, mmetumia ardhi ileile ya Igunga, mto Manonga ulikuwepo, bwawa la Bulenya lilikuwepo, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya walikuwepo, lakini mbona hawakufanya chochote? Ninyi mmethubutu, nawapongeza sana lakini nawaomba msiache kuvuta wananchi wanaozunguka mashamba ya vijana ili nao pia wafaidike na uwepo wa vikundi vya vijana hawa,” aliongeza.
Aliwataka viongozi wa wilaya hiyo wa serikali na wa vyama vya siasa washirikiane kulea vikundi hivyo bila kujali wanavikundi wanatoka chama gani na kusisitiza kwamba vikundi hivyo ni kiungo muhimu cha kuleta maendeleo.
Alisifia mpango wa kuanzisha kijiji cha vijana katika wilaya ya Sikonge ambacho alikiita ni ‘maisha plus plus plus’ kutokana jinsi walioamua kuanza maisha katika hali ya chini lakini wakiwa wamedhamiria kujiletea maendeleo kupitia kazi za uzalishaji za kilimo, ususi, uchongaji, ufugaji mifugo na ufugaji nyuki.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Igunga, Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Elibariki Kingu alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya yake imetenga maeneo matano yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 250 kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali zinazofanywa na vikundi vya vijana.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ya kilimo cha umwagiliaji cha alizeti, mahindi, vitunguu, matikiti maji na mboga za majani. Aliitaja miradi mingine kuwa nikikundi cha vijana kinachotengeneza vyombo vya nyumbani kama vile makarai, majiko na ndoo kwa kutumia vyuma chakavu pamoja na kikundi cha vijana wanaofanya shughuli ya kusafirisha abiria kwa pikipiki.
Alisema wilaya hiyo imeweka mpango mkakati wa kutumia fursa zilizopo kujenga mazingira ya upatikanaji wa ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo baada ya umebaini kuwa kilimo cha vitunguu kina tija kubwa kwa vile linalimika kwa urahisi na halihitaji matunzo makubwa kama madawa na pembejeo nyingine.
“Zao hili limekuwa halilimwi kwa wingi hapa wilayani kwa sababu ya watu wengi kukosa ufahamu wa matokeo katika kulima zao hili. Ijapokuwa Wilaya ya Igunga, ni kame, ina udongo wenye rutuba nyingi na kuna mabwawa mawili na malambo 51 ambayo pamoja na mahitaji mengine ya maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo, yanaweza kusaidia katika kilimo cha vitunguu na mbogamboga,” alisema.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa masoko, Bw. Kingu alisema bei ya vitunguu imekuwa juu wakati wote bila kujali msimu na kuna wakati inafika sh. 100,000/- kwa gunia moja. “Soko la vitunguu lipo kila wakati ndani na nje ya nchi. Wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo wamekuwa wakinunua zao hili toka Tanzania,” aliongeza.
“Wiki ijayo tutakwenda Kenya kukutana na wafanyabiashara kutoka Sudan na Kenya wanaohitaji vitunguu kwa wingi. Wanahitaji tani 200 hadi 300. Balozi wa Tanzania nchini Kenya amesema tutasaini hati ya makubaliano (MoU) Septemba 4, mwaka huu,” alisema,
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante ole Gabriel Laizer alisema katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga sh. bilioni sita zikiwa ni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Alisema idadi ya vijana nchini hivi sasa imefikia 16,195,370 na kwamba wanapaswa kubadilisha mtazamo wa fikra zao na kutambua kuwa wanaweza kuboresha maisha yao kwa kubainisha fursa zilizopo kwenye maeneo wanayoishi na kuangalia watazitumiaje fursa hizo badala ya kusubiri kazi za kuajiriwa ambazo hazipo.
Alisema ameanza mazungumzo na wenzake walioko Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kupata uhakika wa fedha vijana zinazopatikana kutoka kwenye Halmashauri.
0 comments:
Post a Comment