YANGA imemponza mwamuzi, Martin Saanya wa Morogoro aliyechezesha mechi yao na Coastal Union ambaye amefungiwa mwaka mmoja kwa kuchezesha mchezo huo chini ya kiwango.
Saanya
amepewa adhabu hiyo ya kutochezesha mechi yoyote ya soka ndani ya
kipindi hicho sawa na mshika kibendera namba moja wa mechi hiyo, Jesse
Erasmo ambaye alishindwa kutoa uamuzi sahihi wa adhabu ya penalti
waliyopewa Coastal ndani ya dakika za nyongeza kabla ya mpira kumalizika
na kusababisha sare ya bao 1-1.
Penalti
hiyo ndiyo ilisababisha vurugu ambazo zilifanywa na mashabiki wa Yanga
ambao , walimshambulia mwamuzi kwa chupa za maji na kuvunja kioo cha
basi la wachezaji wa Coastal na kumjeruhi kichwani beki wa timu hiyo,
Hamis Hamad aliyelazimika kuwahishwa hospitali.
Adhabu hizo zimekuja baada ya Bodi ya Ligi kupitia taarifa ya kamishna wa mechi hiyo, Omary Walii kutoka Arusha.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga
aliliambia Mwanaspoti kuwa: “Saanya na Erasmo wamefungiwa mwaka mmoja
kuchezesha mechi za ligi baada ya bodi kupitia ripoti ya kamishina wa
mchezo huo.
Saanya
ameadhibiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu ya penalti
iliyofungwa na Coastal akiwa mbali na tukio,” alisema Mwakibinga na
kufafanua kuwa posho za waamuzi wa mechi kwa sasa ni Sh 250,000 mbali na
nauli na teksi tofauti na zamani walipokuwa wanalipwa shilingi 170,000.
“Kwa
upande wa Erasmo ndiye alikuwa eneo la tukio ilipotokea penalti, lakini
alishindwa kumsaidia mwamuzi wa kati na kubaki ameduwaa kama asiye na
uhakika.”
Mwakibinga
alisema mbali na adhabu hizo kwa waamuzi, Kamati imemfungia kocha wa
makipa wa Coastal Union, Juma Pondamali muda wa miezi mitatu na faini ya
Sh1 milioni kwa kutoa lugha ya matusi kwa mashabiki wanaodaiwa ni wa
Simba.
Katika
hatua nyingine, Coastal imetozwa faini ya Sh100,000 kwa kuchelewa kikao
cha maandalizi ya mechi asubuhi kwa dakika 23 huku Yanga ikitozwa faini
ya Sh1 milioni kwa mashabiki wake kurusha chupa uwanjani na pia
kumvamia mwamuzi huku viongozi wakishindwa kuwadhibiti.
Kuhusu basi la Coastal hakukuwa na taarifa kwani tukio lilitokea nje ya uwanja.
SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI
0 comments:
Post a Comment