Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
KLABU
ya soka ya Mbeya City ya jijini Mbeya imesema malengo yake ni kufanya
vizuri msimu huu licha ya kuwa msimu wa kwanza kwao kucheza michuano ya
ligi kuu soka Tanzania bara .
Akizungumza na mtandao wa FULLSHANGWE
kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi “Ferguson wa Mbeya” amesema
kuwa wameanza mechi tatu wakiwa nyumbani, wakishinda moja na kutoa sare
mbili, lakini wamejipanga kucheza mechi zote kwa kiwango cha juu sana
bila kujali wako wapi.
“Tumeanza
nyumbani mechi zote tatu, lakini hili sio tatizo kwetu, tunajua kuwa
lazima timu icheze nyumbani na ugenini, tumejiandaa kwa mechi zote na
tunaanza kibarua na Mtibwa wakiwa kwao, maandalizi yanakwenda vizuri na
hivi tuko njiani kuelekea Morogoro tayari kwa kazi moja ya kusaka
ushindi”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi
alisema timu yake imecheza mechi ngumu sana mwanzoni na kadri muda
unavyozidi kwenda kikosi chake kinaimarika na kucheza kitimu zaidi.
“Vijana
wangu wanashika maelekezo kwa haraka, najivunia hilo, kwasasa tatizo
kubwa ni ubutu wa safu ya ushambuliaji, kabla ya mchezo wa jumatano na
Mtibwa Sugar nitakuwa nimefanyia kazi tatizo hilo na nina matumaini ya
kufanya vizuri”. Alisema Mwambusi.
Kocha
huyo kipenzi kwa wana Mbeya aliweka wazi kufurahishwa na hamasa kubwa
ya mashabiki wa soka mkoani Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kuishangilia
timu yao na kuwapa moyo wachezaji wake ambapo katika mchezo wa jumamosi
kitita cha shilingi milioni 100 kilipatikana na kuvunja rekondi ya mechi
ya Yanga na Prisons mwaka jana.
“Mashabiki
ni mchezaji wa 12, hakika niwazi kuwa Mbeya City ni timu ya wananchi,
mashabiki wamekuwa wakiwapa nguvu sana wachezaji wangu, naamini tutafika
mbali na kutimiza malengo yetu kirahisi”. Alisema Mwambusi.
Mbeya
City ilianza ligi kuu kwa kucheza dhidi ya Kagera Sugar na kutoka
suluhu ya bila kufungana, mchezo wa pili walicheza na Ruvu Shooting na
kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na mwishoni mwa wiki walishuka dimbani
kukabiliana na mabingwa wa ligi hiyo, Yanga SC na kutoka sare ya 1-1.
Mpaka
sasa Mbeya City wamejikusanyia pointi 5 kibindoni na wapo nafasi ya
saba katika msimamo wa ligi kuu, huku JKT Ruvu wakiwa kileleni na mzigo
wa pointi 9, wakifuatiwa na Simba SC wenye pointi saba.
Yanga bado wapo Mbeya wakijiandaa na mchezo mwingine wa ligi kuu jumatano ya wiki hii dhidi ya vibonde, Tanzania Prisons.
0 comments:
Post a Comment