Katika
maisha ya kila siku ya binadamu suala la ulinzi na usalama wa mali na
maisha ni muhimu sana. Binadamu huishi kwa kutegemeana basi ndivyo
ilivyo hata katika suala la ulinzi wa mali na maisha yetu. Unaweza
kujiuliza je,ni nani mwenye jukumu la ulinzi?je,ni mimi au wewe? Au ni
sisi sote?
Basi
katika miaka ya hivi karibuni Jeshi la Polisi Nchini limeendeleza dhana
ya ulinzi shirikishi na ulinzi jirani kwa lengo la kushirikisha jamii
kwa karibu zaidi katika suala zima la ulinzi na usalama. Zana hii
imekuwa ikitoa fursa kwa jamii na wadau mbalimbali kutoa taarifa za
kuzuia uharifu hali inayofanikisha kudhibiti vitendo hivyo.
Ni
wazi kabisa kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki katika
ulinzi.Ushirikishwaji huu wa wananchi katika kuzuia na kudhibiti vitendo
vya uharifu ni mpana zaidi, kwani vitendo vya uvunjifu wa amani na
utovu wa nidhamu si vya kuvumilika katika jamii. Kila mmoja wetu
anapaswa kujua nini cha kufanya pale anapoona vitendo ambavyo si vya
kiungwana vikitendeka.
Katika
siku za hivi karibuni hususani katika mechi za ligi kuu Tanzania bara
kumekuwa kukitokea vitendo ambavyo si vya kiungwana wala kinidhamu
katika mchezo wa mpira wa miguu. Vurugu mbalimbali kutoka mashabiki wa
timu zinazoshiriki ligi kuu zimevuka mipaka kwani imefikia hatua hata ya
kurushiana mawe.Katika mechi ya hivi karibuni kati ya Mbeya City dhidi
ya Yanga mechi iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kulitokea
vitendo visivyo vya kiungwana katika medani ya michezo.
Ikumbukwe
kuwa suala la ulinzi katika sehemu mbalimbali ni jukumu letu sote. Kila
mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha amani na utulivu
vinachukua nafasi yake katika michezo ili kwa ujumla wananchi wapate
burudani.
Vurugu
na vitendo visivyo vya kimichezo vina athari kubwa si tu kwa timu bali
hata kwa mashabiki na wananchi wa mkoa husika kwani inapotokea timu
kufungiwa kutofanya michezo yake katika uwanja wa nyumbani ni athari
hata katika shughuli za kiuchumi pamoja na kuua mapato ya mlangoni. Pia
vurugu kama hizi ni athari pia katika shughuli za uwekezaji na kuzuia
upatikanaji wa fursa ya ajira kwa wananchi.
Yapo
mapendekezo mbalimbali ya wananchi juu ya suala hili la kudhibiti
vurugu katika michezo. Itambulike kuwa ni suala la kila mwananchi kwani
kama kila mmoja wetu ataona umuhimu wa kutoa taarifa pale anapotilia
mashaka mtu/watu kwa vyombo vya ulinzi na usalama, basi suala hili tunao
uwezo wa kulidhibiti na kulimaliza kabisa.Kila mwananchi atoe
ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha kudhibiti na kutokomeza
vitendo vya vurugu uwanjani na katika michezo kwa ujumla.
Pengine
kwa sasa ni muda muafaka kwa uongozi wa timu pamoja na shirikisho la
soka nchini ni kuliangalia suala hili kwa kina zaidi ili kujiepusha na
madhara makubwa zaidi. Kuwepo na adhabu kali zaidi kwa timu itakayo
shindwa kuwadhibiti mashabiki wake dhidi ya vitendo visivyo vya
kimichezo.
Ni
imani yangu kuwa kila mwanamichezo na wadau wote wa michezo watashiriki
kikamilifu kuzuia na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale waonapo
dalili za vurugu kutoka kwa mtu au kikundi cha watu kikipanga njama za
uvunjifu wa amani katika michezo hasa mechi za ligi kuu zinazoendelea.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Mbeya Kamishina msaidizi, DIWANI ATHUMANI
anawakumbusha mashabiki na wadau wote wa michezo kuwa “michezo ni
uchumi, michezo ni burudani, michezo ni upendo/amani na kila mmoja wetu
aone kuwa ana kila sababu ya kutekeleza hili”
Imetolewa na:
[DIWANI ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
0 comments:
Post a Comment