Press Conference
KAULI ZA KISIASA
Hivi
karibuni mnamo tarehe 21/09/2013 vyama vya siasa kadhaa vilifanya
mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani, Pamoja na mambo mengine
yaliyo zungumzwa, mimi kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto nimestushwa na baadhi ya ujumbe wa maneno uliopelekwa kwa
wananchi. Ambao unaweza kuleta madhara kwa jamii, hususan wanawake,
watoto, wazee, walemavu n.k.
Kwanza, Kauli ya Mhe. Lipumba
Mheshimiwa
huyu kati ya maneno yote aliyoyasema pale Jangwani, nadhani jamii
inahitaji kutafakari na kuhoji; maana ya kauli yake aliposema, “Vijana
msikubali wakati wa kufanya mazoezi umefika” Tujiulize, Je, ni mazoezi
ya aina gani? Yanafanyikia wapi? Yanalenga kufanya nini? Lakini mwisho
wa yote ni muhimu Watanzania wakajikumbusha mwenendo wa siku za nyuma za
hao wanaoitwa vijana wake!
Wito
wangu kwa vijana wasikubali kutumiwa katika mambo yanayo wahatarisha
wao na jamii kwa ujumla, kwani hayana tija. Wananchi kumbukeni kuwa
yanapotokea matatizo, akina mama ndio walezi wa majeruhi, wagonjwa na
pia walezi wa watoto wa walioathirika.
Pili, Kauli ya Mhe. Mbowe
Mheshimiwa
huyu kati ya maneno yote aliyoyasema, nilipatwa na butwaa kwa kauli
yake aliposema:- “Siku ya tarehe 10/10/2013 ni Siku Maalum ya Kitaifa ya
“Civil Disobedience”. Hii ni kauli hatari, yenye kuashiria uwepo wa
njama mbaya za kuwashawishi wananchi ili siku hiyo wajichukulie sheria
mkononi, kinyume cha katiba, sheria na haki za binadamu.
Tujiulize “Siku Maalum ya Kitaifa ya Civil Disobedience”
maana yake nini? Kwa Kiswahili maana yake ni Siku Maalum ya Kitaifa ya
Jamii Kutotii, kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa. Hayo yakitokea
itakuwa ni Siku ya Maangamizi. JAMII KUTOTII ni utovu wa Nidhamu, ambao
husababisha Uvunjaji wa Sheria na kuhamasisha kujenga Mazingira ya
Vurugu.
Kwa
nafasi yangu kama Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nasema
hii ni hatari. Na athari zake naziona kubwa kwa wanawake, watoto,
walemavu na wazee.
Tatu, Kauli ya Mhe. Mbatia
Mheshimiwa
huyu kati ya maneno yote aliyoyasema, nadhani jamii inahitaji
kutafakari na kumpongeza kwa kauli yake aliposema:- Bado anaamini kwamba
“Kuna fursa ya kukaa katika round table na kuyazungumza”. Hii
kauli ni ya kizalendo na ya kiungwana. Nampongeza sana. Inavyoonekana,
Mhe. Mbatia ni mtu mwenye kutambua kwamba ana dhamana ya kuilinda
familia yake na jamii ya Watanzania kwa ujumla.
Tahadhari ya kauli zenye kuashiria uvunjifu wa sheria na tabia za vurugu katika jamii
Mwenendo
wa kauli hizi, si mzuri kwa maendeleo na ustawi wa jamii yetu kijamii
na kiuchumi. Hii ina maana siku hiyo ya Civil Disobedience, Mama Lishe
na Wajasiriamali wengine hawatofanya biashara zao, watoto wetu
hawatoenda shule na huduma nyingine za kijamii zitakwama wakati wao
wakitekeleza mipango waliyopanga kwa tarehe hiyo.
Amani na usalama ni mtaji wa maendeleo
Kama
jamii tunapaswa kutambua kwamba amani na usalama, ndio mtaji namba moja
wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kidemokrasia. Ustawi wetu kama
jamii ya Watanzania au kama familia au mtu mmoja mmoja unahitaji uwepo
wa amani, utulivu na usalama. Kwa sababu kunapotokea vurugu/Civil
Disobedience wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto, wazee na walemavu.
Leo nimeona niongelee hili ambalo linawagusa wadau wangu moja kwa moja ambao wapo chini ya Wizara yangu.
Asanteni.
0 comments:
Post a Comment