Na Mhe. Zitto Kabwe
Kwa
takribani wiki tatu sasa kumekuwa na sintofahamu kuhusu muswada wa
sheria uliopitishwa na Bunge ili kufanya marekebisho ya sheria ya
marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011.
Mjadala
na upitishaji wa sheria hii uliweka rekodi ya pekee katika nchi yetu
kwa vitendo vya kihuni kutokea Bungeni ambavyo nisingependa kuvirejea
kutokana na aibu kubwa ambayo Bunge liliingia.
Kiukweli kuna sintofahamu katika nchi kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya.
Hii imechangiwa na kurushiana maneno miongoni mwa wanasiasa wa pande
zote mbili, wanaopinga muswada ulivyo na wanaounga mkono muswada ulivyo.
Masuala
ya Tume imalize kazi yake lini, ushiriki wa Zanzibar na idadi ya
wajumbe kutoka Zanzibar kwenye Bunge la Katiba, Wajumbe wa Bunge Maalumu
wanapatikanaje na kadhalika ni masuala ambayo yanaweza kupatiwa mwafaka
kwa viongozi kukaa na kuzungumza.
Haya
sio masuala ya kushindwa kujenga mwafaka labda kuwe na nia mbaya dhidi
ya mchakato wa kuandika Katiba mpya. Katiba sio suala la kufanyia siasa.
Katiba ni uhai wa Taifa.
Ni wazi kuna kundi kubwa ambalo halijitokezi waziwazi ambalo lingependa pasiwe na katiba mpya ya Wananchi.
Kuna
kundi lingine ambalo lingependa mchakato wa kuandika Katiba uendelee
kwa miaka mingine zaidi ili kuweza kupata Katiba bora.
Kuna
kundi la Wabunge ambao kwa chinichini wanataka mchakato uendelee,
uchaguzi uahirishwe mpaka mwaka 2017 na wao waendelee kuwa wabunge.
Naamini watu hawa wanaota ndoto za mchana kwani hakuna mahusiano yeyote
kati ya uchaguzi mkuu na kuandika katiba mpya.
Kama
Bunge hili la sasa na Serikali hii itashindwa kukamilisha zoezi hili,
Bunge linalokuja na Serikali itakayoingia madarakani itaendelea nalo.
Hivyo
sio lazima kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. CHADEMA
imependekeza kuwepo na marekebisho ya mpito kwenye Katiba ya sasa ili
kuwezesha Tume huru ya Uchaguzi, masuala ya wagombea binafsi na
kadhalika. Vyama vingine vya siasa vinaweza kuwa na mapendekezo yao ya
mpito na hivyo kutoa nafasi ya kutosha kabisa wa kuandika Katiba makini.
Changamoto
kubwa sana ya siasa za Tanzania ni kelele. Wanasiasa hatuzungumzi
kwenye masuala yanayohusu uhai wa Taifa. Kila chama kinakuwa na misimamo
yake na kuishikilia na hatimaye kujikuta tunapoteza fursa ya kuzungumza
na kujadiliana kama Watanzania. Mwaka 2011 hali ilikuwa hivi hivi mpaka
kundi la Wazee viongozi wastaafu walipoingilia kati na kupelekea
wanasiasa kukaa na kuzungumza.
Bahati mbaya sana viongozi wale ndio sasa wamepewa usukani wa kuandika
Katiba kwa kuwa kwenye Tume. Hawawezi tena kufanya kazi ile ya kutafuta
suluhu iliyopelekea Rais kuzungumza na viongozi wa vyama vyote vya siasa
ikulu jijini Dar es Salaam.
Vyama
vya Upinzani nchini sasa vimeungana kupinga muswada wa marekebisho ya
Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2011. Waziri wa Sheria na
Katiba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais mahusiano na Uratibu, viongozi
waandamizi wa CCM wote nao wameungana kuunga mkono muswada kama ulivyo.
Badala
ya kutafuta mwafaka, kumekuwa na kurushiana maneno ya kejeli na
kadhalika. Taifa halijengwi namna hii. Taifa linajengwa kwa mwafaka na
Katiba ni moja ya nyenzo wa Mwafaka wa Taifa. Niliwahi kuandika huko
nyuma kuwa Katiba haiandikwi barabarani bali huandikwa mezani kwa watu
kukaa na kukubaliana masuala ya Taifa dhidi ya maslahi ya kivyama ya
wanasiasa.
Hakuna
kilichoharibika. Bado tunayo nafasi kama Taifa kukaa na kukubaliana.
Kwa hali ya sasa nafasi hii ipo mikononi mwa Mkuu wa Nchi, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais ana wajibu wa kikatiba wa
kuhakikisha umoja wa kitaifa unaendelea kuongoza mchakato huu wa katiba
ya nchi yetu. Hata hivyo ni vizuri kutahadharisha kuwa sio sahihi kwa
wanasiasa wa pande zote kujaribu kumlazimisha Rais kuridhia ama
kutoridhia sheria hiyo.
Si
sawa kisiasa kwa wanasiasa wa upinzani kujaribu kumlazimisha Rais
ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni kwenda
tofauti na wabunge wake na wakati huohuo ni utovu wa nidhamu kwa Waziri
wa Sheria kujaribu kumshauri hadharani Rais wake kuridhia sheria hiyo
kwani ni kinyume cha misingi ya uongozi na pia kinatafsirika kama
kumshurutisha (blackmail) Rais wake.
Kutosaini
muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge wa CCM na Rais.
Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba umoja wa
kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao. Pia
kikatiba Rais anasaini miswada kuwa sheria akiwa Mkuu wa Nchi na sio
Mkuu wa Serikali ya Jamhuri. Akiwa Mkuu wa Nchi maslahi mapana ni kuweka
mwafaka wa pamoja miongoni mwa wananchi. Rais Jakaya Kikwete anapaswa
kutumia mamlaka yake kama Mkuu wa Nchi kuiweka nchi pamoja kwa
kuurejesha muswada bungeni ili uweze kujadiliwa upya na wadau wote na
kupitishwa tena na Bunge. Ibara ya 97 ya Katiba ya sasa imeweka masharti
ya utaratibu wa kutunga sheria na iwapo Rais ataurudisha muswada huu
Bungeni pamoja na maelezo ya hatua hii, upitishwaji wake utahitaji
theluthi mbili ya wabunge wote. Hii itakuwa hatua muhimu sana katika
historia ya demokrasia yetu. Rais afuate ushauri huu kwani una manufaa
makubwa.
Hata
hivyo, ni lazima pawepo na mazungumzo miongoni mwa wanasiasa na makundi
ya kijamii kuhusu Katiba. Katiba nzuri itapatikana pale tu ambapo
mazingira ya kisiasa yanaonyesha nia njema kwa pande zote kisiasa.
Kukwepa kuangaliana machoni na kuzungumza tofauti zetu za kimitazamo ni
hatari zaidi. Juzi ngumi zimerushwa Bungeni. Kesho zitakua mitaani na
vijijini kwetu. Tunataka kujenga Taifa la namna hiyo?
0 comments:
Post a Comment