California/Johannesburg.
Wakati
Rais Jakaya Kikwete akisema Serikali yake haitawatetea Watanzania
wanaokamatwa wakijishughulisha na biashara ya dawa za kulevya,
Watanzania wawili Agnes Masongange na mwenzake, Melisa Edward jana
walinyimwa dhamana na Mahakama Kuu ya North Gauteng katika kesi ya dawa
ya kukamatwa na dawa hizo.
Rais Kikwete alisema Serikali
yake itakabiliana na biashara hiyo kwa nguvu zote kwa kuwa ni haramu na
ni kinyume na sheria za nchi.
Alisema hayo juzi usiku
alipokutana na Watanzania wanaoishi katika Jimbo la California,
Marekani…“Serikali yangu haitawatetea watu wanaojishughulisha na ubebaji
wa dawa za kulevya na kusafirisha nje ya nchi. Hii ni biashara haramu
na inavunja sheria za nchi yetu.”
Masogange na Melisa walikamatwa
Julai 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini
wakituhumiwa kusafirisha kilo 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya
Sh6 bilioni.
Aidha, amesema hayo siku chache
baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na
maofisa forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily,
Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa ya kulevya aina ya
bangi zenye thamani ya Paundi za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Pia, Agosti 31, mwaka huu,
mshambuliaji nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph
Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa
Ndege wa Bole, Addis Ababa walipokuwa wakijiandaa kwenda Paris, Ufaransa
wakituhumiwa kubeba dawa za kulevya.
Juzi, Rais Kikwete alisema ni
wajibu wa Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa raia wema, kufuata na
kuheshimu sheria katika nchi wanazoishi kwa sababu wakizivunja, Serikali
yake haitawatetea.
“Ukikamatwa na dawa za kulevya
hatukutetei kwa sababu hata sheria za nchi yetu zinazuia biashara hiyo.
Sisi hatuwezi kuendelea kuwa na sifa ya kufanya biashara za ovyoovyo
kiasi hicho. Serikali itawatetea Watanzania wanaoishi nchi za nje ikiwa
wataonewa. Lakini ukifanya biashara ya dawa ya kulevya au kubaka watu
hatukutetei kamwe,” alisema.
Masogange, Melisa wakwama dhamana
Masogange na mwenzake Melisa
jana walikosa dhamana baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu
ya North Gauteng, Afrika Kusini kujibu mashtaka ya kusafirisha dawa
zinazodaiwa kutumika kutengenezea dawa aina ya amphetamine (maarufu kama
tik).
Taarifa kutoka Mahakama hiyo
zinaeleza kuwa, Masogange na Melissa walirudishwa rumande na kesi yao
itasikilizwa tena Novemba mwaka huu.
Mkuu
wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya cha Polisi nchini, Kamanda
Godfrey Nzowa alithibitisha kuwa watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana
kujibu mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na kwamba
wamerudishwa rumande hadi Novemba.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment