Shughuli
za uokozi zinaingia siku ya nne tangu jengo la maduka la Westgate
jijini Nairobi kushambuliwa na magaidi Jumamosi na kusababisha zaidi ya
watu 60 kuuwawa na wengine wengi kupata Majeraha.
Serikali
ya Kenya kupitia Waziri wa masuala ya ndani Joseph Ole lenku imesema
imelidhibiti jengo zima na kuwauwa baadhi ya wanachama wa kundi la Al
Shabaab waliokiri kutekeleza shambulizi hilo, lakini hii leo asubuhi
milio ya risasi ilisikika ndani ya jengo hilo, hali inayoashiria wazi
kuwa bado magaidi wapo ndani ya jumba la Westgate.
Hata
hivyo Waziri huyo amesema kwamba wamefanikiwa kuwauwa angalau
wapiganaji wawili wa kundi hilo la Al Shabaab lililo na mafungamano na
kundi la kigaidi la Al Qaeda.
Magaidi hao walifika katika jengo hilo na kuanza kuwamiminia risasi raia waliokuwa katika jengo hilo la biashara.
Kulingana na waandishi habari waliopiga kambi kilomita 70 nje ya jengo
hilo wanasema magari ya wazima moto, magari ya kusafirishia wagonjwa na
hata wafanyakazi wa Shirika la msalaba mwekundu walikusanyika katika
eneo hilo tayari kutoa usaidizi wao kwa majeruhi au matekwa wanaoaminika
bado wapo ndani ya jengo.
Wakati huo huo wakenya wamekuwa wakitiana moyo na kuhimiza uwepo wa
amani nchini na kuungana pamoja wakati huu ambapo taifa linaomboleza
kutokana na shambulizi hilo la kigaidi lililowajeruhi zaidi ya watu 200.
Al Shabaab wazungumzia shambulizi
Huku
hayo yakiarifiwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al Shabaab limesema
kwamba bado wanawashikilia watu kadhaa mateka ndani ya jengo hilo. Kundi
hilo la kigaidi limesema bado linashikilia msimamo wao.
Awali walisema kwamba iwapo Kenya inataka kuwa na amani katika taifa
hilo basi ni lazima waondowe jeshi lake nchini Somalia lililotumwa huku
kupambana dhidi ya magaidi hao.
Kutokana na ujumbe wao waliouwasilisha katika mtandao wa kijamii wa
Twitter kundi hilo limesema kwamba mateka wanaowashikilia wote wako hai.
Hata
hivyo maafisa wa usalama wanasema kwamba wamefanikiwa kuwaokoa mateka
kadhaa japo kwa sasa hawana idadi kamili ya wale waliobakia ndani ya
jengo nawapiganaji hao wa Al shabaab.
Fatou Bensouda alaani shambulizi la Westgate
Kwa
upande wake mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya uhalifu wa kivita ICC
ilioko The hague Uholanzi Fatou Bensouda amesema amelaani kitendo hicho
cha kigaidi na kusema kuwa ICC iko tayari kusaidia kuwafungulia
mashtaka wale walioshirikiana na magaidi kupanga shambulio la Westgate.
Bensouda
ametoa pole zake kwa waathiriwa .Jumatatu mahakama hiyo ya ICC
ilimruhusu makamu wa rais nchini Kenya William Ruto kurudi nyumbani kwa
muda wa wiki moja ili kuwa na wakenya katika wakati huu wa shambulizi.
Ruto
na mshitakiwa mwenzake mwandishi habari Joshua Arap Sang wanakabiliwa
na makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu wanayodaiwa kufanya katika
ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007.
Katika hotuba yake makamu wa rais william Ruto alisema kwamba serikali
itafanya kila liwezalo kuhakikisha kuwa kenya ni salama kwa wawekezaji,
watalii, na kila mkenya na kuwa nchi hiyo haitayumbishwa na mashambulizi
ya kundi la Al Shabaab linalojaribu kuwagawanya wakenya kwa misingi ya
kidini.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP/ The Standard/ Daily Nation
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman
CHANZO: IDHAA YA KISHWAHILI YA DW
0 comments:
Post a Comment